ZDCEA, Posta kukabili tishio dawa za kulevya
4 mins read

ZDCEA, Posta kukabili tishio dawa za kulevya

Unguja. Mamlaka ya Kudhibiti na Kupambana na Dawa za Kulevya Zanzibar (ZDCEA) na Shirika la Posta Tanzania, zimesaini hati ya makubaliano ya ushirikiano (MoU) kwa lengo la kuimarisha udhibiti na kuzuia matumizi ya mtandao wa usafirishaji wa mizigo katika biashara haramu ya dawa za kulevya.

Ushirikiano huo unalenga kukabiliana na tishio linaloongezeka la uingizaji wa dawa haramu na mabadiliko ya mbinu zinazotumiwa na wasafirishaji wa dawa hizo.

Akizungumza wakati wa utiaji saini wa makubaliano hayo leo Alhamisi, Oktoba 29, 2026, Kamishna Mkuu wa ZDCEA, Kanali Burhani Zuber Nassor, amesema mbinu za kusafirisha dawa za kulevya zimebadilika kutoka njia za kawaida na kuhamia kwenye mifumo ya kidijitali na mitandao.

Amesema mabadiliko hayo yameongeza tishio la uingizaji wa dawa za kulevya zinazotengenezwa viwandani, mimea inayotumika kutengeneza dawa hizo na kemikali bashirifu katika jamii.

“Mbinu za usafirishaji wa biashara haramu ya dawa za kulevya zimebadilika, zikitoka kwenye njia za asili na kuhamia kwenye mifumo mipya au njia mpya za kidijitali, teknolojia na mitandao,” amesema.

Ameongeza: “Lengo kuu la makubaliano haya ni kuwa na huduma salama za posta kutokana na tishio kubwa la uingizaji wa dawa za kulevya za viwandani na kemikali bashirifu kwenye jamii yetu.”

Kwa mujibu wa Kanali Burhani, ushirikiano huo pia unalenga kuwalinda wafanyakazi wa posta wanaokabiliwa na hatari za kiafya wanapokagua vifurushi vinavyoweza kuwa na sumu au dawa haramu.

Amesema duniani kote zimegunduliwa takriban aina 755 za dawa mpya ambazo bado hazijabainika katika jamii.

“Ushirikiano huu si wa kisheria tu, bali ni wa kulinda maisha ya raia wetu na kuwalinda wafanyakazi wa posta wanaokabiliwa na hatari za kiafya. Malengo yetu ni kubadilishana taarifa za kiintelijensia, kuweka mifumo thabiti ya taarifa za hatari na kujengeana uwezo,” amesema Kanali Burhani.

Naye Postamasta Mkuu wa Shirika la Posta Tanzania, Macrice Mbodo, amesema shirika hilo limepewa jukumu la kisheria la kusafirisha nyaraka, vifurushi na mizigo ndani na nje ya mipaka ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kwa mujibu wa Kifungu cha 8(1) cha Sheria, Sura ya 303.

Amesema pia mkataba wa Umoja wa Posta Duniani (UPU), chini ya Ibara ya 8(1), unazitaka nchi wanachama kuhakikisha mtandao wa posta hautumiki kusafirisha bidhaa haramu.

“Shirika la Posta Tanzania ni mtoa huduma mteule kwa niaba ya nchi. Mkataba wa Umoja wa Posta Duniani unazitaka nchi zote wanachama kuhakikisha mtandao wa posta hautumiki kusafirisha bidhaa haramu, ikiwemo dawa za kulevya,” amesema Mbodo.

Amesema makubaliano hayo yataimarisha miundombinu, uwezo wa kitaalamu na matumizi ya teknolojia katika ukaguzi wa vifurushi na kuchukua hatua stahiki.

Mbodo amewaonya watu wanaokusudia kutumia mtandao wa posta kusafirisha dawa za kulevya, akibainisha kuwa mtandao huo umeunganishwa na nchi 192 duniani.

“Kwa wale wenye mpango au nia ya kutumia mtandao wetu kusafirisha dawa za kulevya, niwape taarifa tu, msijaribu. Hakuna mbinu ambayo hatuijui, tumejipanga vizuri na tutawabaini na kuwafikisha kwenye vyombo husika vya sheria,” ameonya.

Ukaguzi wa pamoja kuimarishwa

Kwa upande wake, Kamishna wa Sheria, Mashtaka na Urejeshaji Mali wa ZDCEA, Saidi Idrisa Ikaji, amesema Shirika la Posta ni mdau muhimu katika mapambano dhidi ya dawa za kulevya kutokana na jukumu lake la kupokea, kuhifadhi na kusafirisha vifurushi na barua.

Amesema huduma hizo zinaweza kutumiwa vibaya na baadhi ya watu kuficha na kusafirisha dawa za kulevya, hivyo ushirikiano wa taasisi hizo ni muhimu katika kuzuia vitendo hivyo.

“Tunatambua kwamba huduma hizi zinaweza kutumiwa vibaya na baadhi ya watu kuficha na kusafirisha dawa za kulevya. Ushirikiano wetu unahusisha kubadilishana taarifa za vifurushi vinavyotia shaka, ukaguzi wa pamoja na utoaji wa mafunzo,” amesema Ikaji.

Ameongeza kuwa katika kutekeleza makubaliano hayo, taasisi hizo zitazingatia sheria na kuheshimu haki za wananchi huku zikihakikisha huduma zinaendelea kutolewa kwa ufanisi.

Waziri ataka makubaliano yatekelezwe

Akihitimisha, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Kwanza wa Rais, Anna Athanas Paul, ambaye alikuwa mgeni rasmi katika hafla hiyo, amesema biashara haramu ya dawa za kulevya imeendelea kubadilika kutokana na maendeleo ya teknolojia na kuongezeka kwa shughuli za usafirishaji wa mizigo na vifurushi.

Amesema hali hiyo inahitaji kuimarishwa kwa mifumo ya ukaguzi, ubadilishanaji wa taarifa na uwezo wa wataalamu ili kuziba mianya inayoweza kutumiwa na wahalifu.

“Biashara haramu ya dawa za kulevya imeendelea kubadilika kutokana na maendeleo ya teknolojia na kuongezeka kwa shughuli za usafirishaji wa mizigo na vifurushi.

“Hali hii inatukumbusha umuhimu wa kuimarisha mifumo ya ukaguzi, kubadilishana taarifa na kujenga uwezo wa wataalamu wetu ili kuziba mianya inayoweza kutumiwa na wahalifu,” amesema Waziri Anna.

Ametumia fursa hiyo kuziagiza taasisi hizo kuhakikisha makubaliano yaliyosainiwa yanatekelezwa kwa vitendo kwa kuweka mpango wa utekelezaji, majukumu yaliyo wazi na utaratibu wa kufuatilia na kutathimini maendeleo ya ushirikiano huo mara kwa mara.

Source link

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *