Wachimbaji Chunya wataja vikwazo vinavyowakabili
2 mins read

Wachimbaji Chunya wataja vikwazo vinavyowakabili

Chunya. Uhaba wa mikopo, changamoto ya umeme na ushindani na kampuni kubwa ni miongoni mwa vikwazo kwa wachimbaji dhahabu wilayani Chunya Mkoa wa Mbeya katika kutekeleza shughuli zao.

Wachimbaji hao wameomba kufanyike utafiti wa maeneo wanayochimba ili kurahisisha upatikanaji wa mikopo kutoka taasisi za fedha, kuongezwa kwa jengo la usajili katika soko la dhahabu ili kuboresha huduma kwa wafanyabiashara.

Wakizungumza wakati wa kikao kati ya watendaji wa Serikali na wanachama wa Chama cha Wachimbaji Madini (Mberema), hivi karibuni, wamesema baadhi ya maeneo yanahitaji kuboreshwa ili kuruhusu shughuli kufanyika vema.

Mchimbaji Geofrey Philipo amesema endapo Serikali itasikia kilio chao, sekta ya madini itafanya vizuri katika changizo la mapato ya Taifa na kuwekeza kwenye mradi ya maendeleo ya kimkakati.

Mwenyekiti wa Chama cha Wachimbaji Madini Mkoa wa Mbeya, Sadam Kyando amesema utafiti wa maeneo ya uchimbaji ni miongoni mwa hatua muhimu zinazoweza kuwasaidia kupata mikopo kutoka taasisi za fedha.

“Ujenzi wa kiwanda cha kusafisha dhahabu ni hitaji jingine la wachimbaji, upo umuhimu wa kuendelea kutoa elimu kwa wanaofanya shughuli zao katika maeneo ya hifadhi ili waelewe taratibu zinazopaswa kufuatwa,” amesema.

Ofisa Madini Mkazi wa Mkoa wa Kimadini wa Chunya, Laurent Mayala amesema shughuli za uchimbaji zinaongozwa na aina mbalimbali za leseni, zikiwamo za utafiti, uchimbaji mdogo, wa kati na mkubwa.

Amesema kila aina ya leseni ina masharti na taratibu zake, hivyo wachimbaji wanapaswa kuzingatia sheria na miongozo inayosimamia sekta hiyo na kwamba leseni mbili haziwezi kutolewa katika maeneo yanayopishana.

Mchimbaji wa madini ya dhahabu wilayani chunya Keneth Mwakyusa akiwasilisha kero zao kwa upande wa Serikali katika mkutano maalumu wa kusikiliza kero zao.

“Leseni mbili haziwezi kutolewa katika maeneo yanayopishana kinyume na taratibu zilizowekwa, akiahidi kuwa ofisi ya madini itaendelea kushughulikia kero zinazowasilishwa na wachimbaji kwa mujibu wa sheria,” amesema Mayala.

Mkuu wa Wilaya ya Chunya, Sozi Ngate amesema wachimbaji ni wadau muhimu katika ukuaji wa uchumi kutokana na mchango wao kwenye mapato ya halmashauri na Taifa kwa ujumla.

“Tunatarajia kuongeza uzalishaji wa madini ya dhahabu kutoka kilo 300 hadi 400 kwa mwezi sambamba na kuhakikisha wachimbaji wanakuwa katika mazingira wezeshi ya kiusalama,” amesema.

Naye, Mwenyekiti Halmashauri ya Wilaya ya Chunya, Kelvini Shinshi amesema halmashauri inategemea kwa kiasi kikubwa mapato yatokanayo na sekta ya madini.

“Katika mwaka wa fedha 2026/27, halmashauri imepanga kukusanya Sh3.5 bilioni kutoka kwenye sekta ya madini, huku wachimbaji wakiendelea kuchangia miradi ya maendeleo kupitia Mfuko wa Maendeleo Chunya (Chudef),” amesema.

Source link

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *