Wajasiriamali 653 kusaka fursa maonyesho ya Sido Kahama
Kahama. Wajasiriamali zaidi ya 650 wamekusanyika katika maonyesho ya tano ya kitaifa ya Shirika la Kuhudumia Viwanda Vidogo (Sido), yanayoendelea wilayani Kahama, mkoani Shinyanga, kutafuta fursa za kukuza biashara zao, kupata ujuzi na kuunganishwa na huduma muhimu za kibiashara.
Mkurugenzi wa mafunzo na usimamizi wa mikoa wa Sido, George Kasinga, amesema maonyesho hayo yamewakutanisha wajasiriamali kutoka mikoa mbalimbali nchini na nje ya nchi, huku washiriki hao wakipata nafasi ya kuonyesha bidhaa zao na kutafuta fursa za kibiashara.
Amesema hadi asubuhi ya leo Oktoba 27, 2026, wajasiriamali 353 walikuwa wamewasilisha bidhaa zao katika viwanja vya maonyesho hayo, na kuungana na washiriki wengine kufikisha zaidi ya 650.
Kasinga ameyasema hayo alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maendeleo ya maonyesho hayo, akieleza kuwa Sido inaendelea kuwawezesha wajasiriamali kupitia mafunzo, ushauri wa kibiashara na huduma zinazolenga kuimarisha shughuli zao za uzalishaji na biashara.
Amesema katika mwaka wa fedha 2025/2026, shirika hilo lilitoa mafunzo kwa wajasiriamali 11,220, ushauri kwa wajasiriamali 17,283 na kuchangia uzalishaji wa ajira 11,000.
“Haya maonyesho yamefana sana. Kwa mwaka uliopita wa fedha, tumetoa mafunzo kwa wajasiriamali 11,220, tumewapa elimu kwa maana ya ushauri wajasiriamali 17,283 na tumezalisha ajira 11,000,” amesema Kasinga.
Ameongeza kuwa fursa za ajira zinaendelea kuongezeka, hususan kwa vijana na wanawake, kupitia shughuli za ujasiriamali zinazowezeshwa na shirika hilo.
Sido yaeleza fursa kwa wajasiriamali
Kasinga amewataka vijana, wanawake na wananchi wengine wenye nia ya kuanzisha au kukuza biashara kutembelea ofisi za Sido zilizopo katika mikoa mbalimbali nchini ili kunufaika na mafunzo na huduma zinazotolewa.
Amesema mafunzo hayo yanahusisha usindikaji wa vyakula, utengenezaji wa vipodozi, batiki na sabuni, pamoja na elimu ya ujasiriamali, usimamizi wa fedha na mikopo.
“Vijana na akina mama wafike kwenye mikoa yote ya Sido nchini wapate mafunzo ya kusindika vyakula, kutengeneza vipodozi, batiki na sabuni. Tunatoa elimu ya ujasiriamali, fedha na mikopo, lakini pia tunawakopesha,” amesema.
Amesema mbali na mafunzo, Sido huwasaidia wajasiriamali kurasimisha biashara zao kwa kuwaunganisha na taasisi husika, ikiwamo Wakala wa Usajili wa Biashara na Leseni (Brela) na Shirika la Viwango Tanzania (TBS).
Kwa mujibu wa Kasinga, hatua hiyo inalenga kuwawezesha wajasiriamali kukamilisha taratibu zinazohitajika katika uendeshaji wa biashara zao na kujenga msingi imara wa ukuaji.
Ameeleza kuwa shirika hilo pia lina programu za kulea wajasiriamali kupitia vituo vya uatamizi wa biashara, pamoja na kuwakaribisha wabunifu wanaotengeneza teknolojia mbalimbali ili kuwasaidia kuendeleza mawazo yao hadi kufikia hatua ya kuanzisha kampuni.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Manispaa ya Kahama, Masudi Kibetu, ameipongeza Sido kwa kuandaa maonesho hayo, akiwataka wananchi, hususan vijana, kuyatumia kupata maarifa na kutambua fursa za kujikwamua kiuchumi.
“Niwapongeze waandaaji wa maonyesho haya pamoja na wananchi wanaoendelea kuyatembelea. Wakati natembelea nimeona fursa mbalimbali zipo hapa. Vijana waje wapate elimu inayotolewa hapa. Hii ni fursa ya kipekee ndani ya Manispaa ya Kahama, tuitumie,” amesema.

