Washtakiwa watano, akiwamo Polisi kuanza majadiliano na DPP
2 mins read

Washtakiwa watano, akiwamo Polisi kuanza majadiliano na DPP

Dar es Salaam. Aliyekuwa askari polisi, Sajenti John Kaposwe (46) na washtakiwa wenzake wanne, wanaokabiliwa na kesi ya uhujumu uchumi yenye mashtaka 26, wanatarajiwa kuanza majadiliano na Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) Novemba 3, 2026, baada ya kuomba kukiri mashtaka yanayowakabili.

Hatua hiyo imefikiwa baada ya upande wa mashtaka kupitia barua za washtakiwa hao, ambao wameomba kukiri mashtaka na kujadiliana na DPP kuhusu uwezekano wa kupunguziwa adhabu ili kumaliza kesi hiyo.

Wakili wa Serikali, Monica Matwe ameeleza hayo leo Jumanne, Oktoba 27, 2026, mbele ya Hakimu Mkazi Mkuu, Aaron Lyamuya, katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam, wakati kesi hiyo ilipotajwa.

Mbali na Kaposwe, ambaye ni mkazi wa Kurasini, washtakiwa wengine walioandika barua kwa DPP ni wafanyabiashara Damson Mnyilenga (59), Simon Aloyce (60), Vernand Liberio (29) na aliyekuwa askari wa polisi mwenye namba WP 10050, PC Julieth Moshi (30).

Hata hivyo, washtakiwa wengine wanne hawajaandika barua ya kuomba majadiliano na DPP. Hao ni aliyekuwa Mkaguzi wa Polisi Fredrick Malekela (45), mwenye namba PF 19931, pamoja na Sajenti Kalemwa Kaunga (54), mwenye namba E.4627, mkazi wa Chanika; Sajenti Edger Mlogo (54), mwenye namba E.7855, mkazi wa Kibamba; na Sajenti Robert Titus (47), mwenye namba F.1126, mkazi wa Kisarawe.

Akitoa taarifa mahakamani hapo, Wakili Matwe amesema upelelezi wa kesi hiyo bado unaendelea, lakini upande wa mashtaka umepokea na kupitia barua za washtakiwa hao watano.

“Shauri hilo limeitwa kwa ajili ya kutajwa, upelelezi wake bado unaendelea,” amesema Matwe.

Ameongeza: “Pia tumepokea barua za washtakiwa watano, wakiomba kukiri mashtaka na kufanya majadiliano na Mkurugenzi wa Mashtaka nchini, hivyo barua hizo tumezipitia na tunaomba mahakama itupangie tarehe kwa ajili ya kuanza vikao vya majadiliano.”

Kutokana na ombi hilo, Hakimu Lyamuya amepanga Novemba 3, 2026 kuwa siku ya kuanza kwa majadiliano kati ya washtakiwa hao na upande wa mashtaka, kisha kuahirisha kesi hadi tarehe hiyo.

Washtakiwa wote tisa wamerudishwa rumande kutokana na kukabiliwa na shtaka la utakatishaji fedha, ambalo halina dhamana kwa mujibu wa sheria.

Katika kesi ya msingi, washtakiwa hao wanadaiwa kuwa kati ya Aprili 2021 na Juni 2025, ndani ya Tanzania, waliendesha genge la uhalifu lililohusika na utakatishaji fedha.

Pia, wanadaiwa kujipatia Sh10 milioni kutoka kwa Mikidadi Hamad kwa njia ya udanganyifu, wakimuahidi kumpatia leseni ya kumiliki silaha huku wakijua kuwa ahadi hiyo ilikuwa ya uongo.

Katika mashtaka mengine, wanadaiwa kujipatia Sh75 milioni kutoka kwa watu 23 kwa kutumia ahadi kama hiyo, na kufanya jumla ya fedha zinazodaiwa kupatikana kwa njia ya udanganyifu kufikia Sh85 milioni.

Shtaka la mwisho linawahusu wote tisa, wakidaiwa kutakatisha Sh85.2 milioni kati ya Aprili 2021 na Juni 2025, wakijua fedha hizo zilitokana na kosa la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu.

Kwa jumla, washtakiwa hao wanakabiliwa na mashtaka 26, yakiwemo 24 ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu, moja la kuongoza genge la uhalifu na moja la utakatishaji fedha.

Source link

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *