Tume ya Haki za Binadamu Kenya yataka uchunguzi kutoweka Mwaipaya
Kenya. Tume ya Taifa ya Haki za Binadamu Kenya (KNCHR) imetaka Serikali ya nchi hiyo kuchukua hatua za haraka kubaini aliko mwanaharakati wa kisiasa Mtanzania, Twaha Mwaipaya, anayedaiwa kutekwa na watu wasiojulikana katika Kaunti ya Machakos, Jumapili, Oktoba 25, 2026.
Katika taarifa yake leo Oktoba 29,2026 tume hiyo imesema Mwaipaya alikuwa akisafiri kwa teksi kwenda kuwatembelea marafiki zake eneo la Kamulu, Machakos, alipodaiwa kuzuiwa na watu wasiojulikana saa 8 mchana.
Tayari Serikali ya Kenya na Tanzania zimesema zinafuatilia tukio hilo ambapo Balozi wa Tanzania nchini Kenya, Dk Bernard Kibesse alipozungumza na Mwananchi Oktoba 26, 2026 alisema ubalozi unafuatilia kwa kina tukio hilo.Msemaji wa Serikali ya Kenya, Charles Owino alisema wanafuatilia tukio hilo.
Kwa mujibu wa taarifa ya tume ya haki za bunadamu, watu hao walimshusha kwa nguvu kutoka kwenye gari hilo na kumchukua kwa msafara wa magari matatu na hadi sasa, alikokuwa mwanaharakati huyo hakujulikana.
Mwaipaya anaripotiwa kukimbilia Kenya mwaka 2025 akitokea Tanzania, akihofia usalama wa maisha yake.
“Tume inasikitishwa na tukio hilo, linaweza kuwa sehemu ya mwenendo unaotia wasiwasi wa watu kutoweshwa kwa nguvu, kutekwa na kuhamishwa kuvuka mipaka kinyume cha sheria,” amesema.
Tume hiyo imesema katika kipindi cha miaka miwili iliyopita, raia wengine wa Tanzania, akiwamo Maria Tsehai Sarungi na Mshabaha Hamza, waliripotiwa kutekwa kwa kutumia silaha jijini Nairobi.
Pia, tume hiyo imetaja tukio la Oktoba 2024, ambapo Katibu Mkuu katika Wizara ya Mambo ya Nje na Diaspora ya Kenya alikiri hadharani kuwa Serikali ilikuwa imewarejesha nchini kwao wakimbizi wanne kutoka Uturuki, ambao awali walikuwa wametoweka baada ya kutekwa jijini Nairobi.
Aidha, mwanasiasa wa upinzani kutoka Uganda, Dk Kizza Besigye, anaripotiwa kutekwa jijini Nairobi na kuhamishwa kwa nguvu kwenda Uganda Novemba 2024.
Kwa mujibu wa KNCHR, matukio hayo yanazua maswali kuhusu ulinzi wa watu walio katika hatari, uzingatiaji wa utawala wa sheria na utekelezaji wa wajibu wa Kenya katika kulinda haki za binadamu.
“Matukio hayo yanatishia sifa ya Kenya kama eneo salama kwa watu wanaokimbia mateso, ukandamizaji wa kisiasa na vitisho dhidi ya maisha yao kutoka mataifa mbalimbali ya ukanda huu na kwingineko,” amesema.
Imesisitiza kuwa Kenya ina wajibu wa kikatiba na kimataifa wa kuheshimu, kulinda na kutekeleza haki za binadamu za kila mtu aliye ndani ya mamlaka yake, bila kujali uraia au hadhi yake ya uhamiaji.
Wajibu huo, kwa mujibu wa tume hiyo, unajumuisha masharti ya Ibara za 26, 28, 29 na 49 za Katiba ya Kenya ya mwaka 2010, zinazohusu haki ya kuishi, utu wa binadamu, uhuru na usalama wa mtu pamoja na haki za watu wanaokamatwa.
KNCHR imesema pale mazingira ya tukio yanapoashiria uwezekano wa mtu kutoweshwa kwa nguvu, Serikali inapaswa kuhakikisha uchunguzi wa haraka, huru na wenye ufanisi unafanyika ili kubaini aliko mtu huyo na kilichompata, huku wahusika wakifikishwa kwenye vyombo vya sheria.
“Serikali ya Kenya inapaswa kuzingatia wajibu wake chini ya sheria za kimataifa za wakimbizi na haki za binadamu, ikiwamo Mkataba wa Wakimbizi wa mwaka 1951 na kanuni ya kutomrejesha mtu katika eneo ambako anakabiliwa na hatari ya mateso au ukiukwaji mkubwa wa haki zake,” amesema.
Tume hiyo imesisitiza kuwa hakuna mtu anayepaswa kuhamishwa, kurejeshwa au kukabidhiwa kinyume cha sheria katika eneo ambako anaweza kukabiliwa na mateso au ukiukwaji mwingine mkubwa wa haki za binadamu.
Katika hatua nyingine, tume hiyo imeitaka Serikali kuhakikisha wakimbizi, waomba hifadhi, wakimbizi wa kisiasa na watu wengine walio katika hatari wanalindwa wakiwa ndani ya Kenya.

