Serikali kupiga marufuku pipi kwenye mikutano
Dodoma. Serikali imeagiza kuanzishwa kwa benki za mazao ya asili katika kila Mkoa nchini, huku ikipiga marufuku matumizi ya pipi katika maeneo yasiyo ya lazima ikiwemo kumbi za mikutano, sherehe na maeneo yenye mikusanyiko ya watu wengi.
Agizo hilo limetolewa leo Alhamisi, Oktoba 29, 2026, na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Dk Grace Magembe wakati akizungumza katika maadhimisho ya Siku ya Lishe kitaifa iliyofanyika jijini Dodoma.
Dk Magembe amesema marufuku ya matumizi ya pipi itaanza kutekelezwa kwa hatua wakianza na kupunguza idadi ya pipi katika mikutano ya taasisi inayohusisha watu wengi na matumizi ya bidhaa hizo katika mikutano au matukio yenye idadi ndogo ya watu.
Katibu mkuu wa wizara ya afya Dk Grace Magembe akizungumza jijini Dodoma leo.
Dk Magembe amesema lengo la zuio hilo ni kuondoa hatari ya magonjwa yanayoweza kusababishwa na matumizi ya bidhaa zenye sukari kwa Watanzania ikiwemo magonjwa ya moyo, figo na presha huku ikihimiza matumizia ya vyakula vya asili kwa lengo la kuipunguzia Serikali gharama za kuongeza virutubisho.
“Tuzingatie mlo kamili kulingana na mahitaji ya mwili, na tuanzee kukemea wamiliki wa hoteli tuwaambie watuwekee vyakula, afya Kama karanga, korosho, ili kupunguza athari zinaletwa na matumizi ya bidhaa zenye sukari ikiwemo pipi, amesema Dk Grace.
Amesema hatua hiyo pia itaondoa mzigo na gharama kwa Serikali za ununuzi wa virutubisho ambavyo huongezwa katika vyakula vinavyotengenezwa au mazao ya kisasa ili kuwewezesha wananchi kupata milo kamili.
Mkurugenzi Mtendaji Chama cha Wanasheria Wanawake Tanzania (Tawla), Tike Mwambipile amewataka Watanzania kuzingatia mwongozo wa matumizi ya virutubisho inayotolewa na wataalamu wa afya ili kuepuka madhara yanayosababishwa na ukosefu wa virutubisho hivyo katika vyakula wanavyokula.
Mwambipile amesema, miongozo hiyo ni nyezo muhimu ya wananchi kuepuka magonjwa ikiwa wataizingatia na itawawesha kufanya maamuzi sahihi ya chakula na si kununua magonjwa kwa fedha zao mwenyewe.
“Ushiriki wa taasisi katika kampeni za lishe utawezesha jamii za Kitanzania kuepukana na matatizo yanayotokana na ukosefu wa lishe bora inayohitajika katika kila kundi lililopo kwenye Jamii” amesema Mwambipile.
Ofisa utetezi sera ya kilimo hai Paul Chilewa, akizungumza jijini Dodoma leo
Kwa upande wake Ofisa utetezi sera za kilimo hai, Paulo Chilewa amesistiza matumizi ya mazao ya asili kwa Watanzania ikiwemo mahindi mekundu huku akieleza kuwa kinachokwamisha matumizi hayo ni ukosefu wa uelewa wa kutosha kususu virutubisho vinavyopatikana katika mazao hayo.
Chilewa pia ameshauri utolewaji wa elimu ya manufaa ya mazao hayo na mbinu za ukulima ili kuhamasisha watanzania mazao hayo.
