Sagini amtaka mkandarasi kupunguza vumbi Mbeya
3 mins read

Sagini amtaka mkandarasi kupunguza vumbi Mbeya

Mbeya. Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Jumanne Sagini amemtaka mkandarasi anayejenga barabara ya njia nne kutoka Nsalaga hadi Songwe kuongeza kasi ya ujenzi na kumwaga maji mara kwa mara ili kupunguza vumbi linaloathiri shughuli za kiuchumi za wananchi.

Sagini ametoa maelekezo hayo leo Oktoba 29, 2026, wakati wa ziara ya kukagua utekelezaji wa agizo la Makamu wa Rais, Deogratius Ndejembi, la kufungua njia za pembezoni mwa barabara hiyo ili kupunguza msongamano wa magari na kurahisisha usafiri na usafirishaji.

Amesema licha ya hatua zilizochukuliwa kufungua njia hizo, mkandarasi anapaswa kuhakikisha kero ya vumbi inayowakabili wafanyabiashara na wananchi wanaoishi kando ya mradi huo inatatuliwa haraka.

“Mkandarasi ahakikishe anamwaga maji mara kwa mara ili kupunguza vumbi linaloathiri shughuli za kiuchumi za wananchi wanaofanya biashara pembezoni mwa mradi wa ujenzi wa barabara ya njia nne kutoka Nsalaga hadi Songwe, Wilaya ya Mbeya,” amesema.

Sagini amesema vumbi limekuwa kero kubwa, hasa kwa wamiliki wa hoteli na maduka yaliyo kando ya barabara hiyo, hivyo ni muhimu kuchukua hatua za haraka wakati ujenzi ukiendelea.

Oktoba 16, mwaka huu, Ndejembi aliiagiza Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads) mkoani humo kufungua njia za pembezoni mwa barabara hiyo, akieleza umuhimu wa kuboresha upitishaji wa magari wakati ujenzi ukiendelea.

CCM yaridhishwa na utekelezaji

Mjumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama cha Mapinduzi (CCM) Taifa, Ndele Mwaselela amesema chama hicho kimeridhishwa na hatua zilizochukuliwa na Serikali kutekeleza agizo hilo.

Mwaselela amesema wananchi wanatarajia kuona mradi huo ukikamilika na barabara kuwekwa lami ili kurahisisha usafiri na kuchochea shughuli za kiuchumi.

“Matamanio ya wananchi ni kuona barabara hii ikiwekwa lami. Nimeona maendeleo ni mazuri, hivyo niwapongeze Serikali ya Mkoa na timu nzima ya Tanroads kwa usimamizi wa mradi huu unaoendelea kwa kasi,” amesema.

Ameongeza kuwa jukumu la viongozi wa chama hicho ni kuisimamia Serikali na kufuatilia utekelezaji wa miradi ya maendeleo ili kuhakikisha inakamilika kwa wakati na kwa viwango vinavyotakiwa.

Tanroads yafungua maeneo 106

Akitoa taarifa ya utekelezaji wa agizo hilo, Meneja wa Tanroads Mkoa wa Mbeya, Seleman Bishanga amesema maeneo 106 ya pembezoni mwa barabara hiyo tayari yamefunguliwa.

Amesema ujenzi wa makaravati umeanza pia katika maeneo korofi, yakiwemo Mlima Simike na Iwambi, kwa lengo la kuboresha upitishaji wa maji ya mvua na kuimarisha usalama wa watumiaji wa barabara.

Mradi wa ujenzi wa barabara ya njia nne kutoka Nsalaga hadi Songwe, Wilaya ya Mbeya Vijijini, una urefu wa kilometa 29.

Bishanga amesema kukamilika kwa kazi zinazoendelea kutasaidia kupunguza msongamano wa magari na kurahisisha usafiri wa wananchi, huku kumwagwa kwa maji kukitarajiwa kupunguza kero ya vumbi.

Wananchi waeleza matumaini

Wakazi wa eneo la Simike jijini Mbeya wamesema ziara za viongozi kufuatilia utekelezaji wa mradi huo zinawapa matumaini ya kufunguka kwa fursa za kiuchumi na kupungua kwa muda wanaotumia barabarani kutokana na changamoto za ujenzi.

Tatu Joel amesema pamoja na viongozi wa Serikali kuendelea kutembelea mradi huo, wananchi pia wanashuhudia jitihada za Tanroads kuongeza kasi ya utekelezaji, ikiwemo kuongeza nguvu kazi katika baadhi ya maeneo.

Amesema hatua hizo zinawapa matumaini ya kuona mradi huo ukikamilika na kuondoa changamoto zinazowakabili watumiaji wa barabara pamoja na wafanyabiashara wanaofanya shughuli zao pembezoni mwa barabara hiyo.

Source link

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *