Yasijirudie tena: Viongozi, wanaharakati wataka ukweli na uwajibikaji
8 mins read

Yasijirudie tena: Viongozi, wanaharakati wataka ukweli na uwajibikaji

Dar es Salaam. Viongozi wa dini, mabalozi na wanaharakati wa haki za binadamu wametoa wito wa kuzuia kujirudia kwa ghasia zilizohusishwa na Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025, wakisisitiza umuhimu wa ukweli, uwajibikaji, maridhiano na hatua za kulinda uhai wa wananchi.

Wito huo umetolewa leo, Oktoba 29, 2026, wakati Watanzania wakiwakumbuka watu waliopoteza maisha katika ghasia hizo, huku familia za waathirika zikiendelea kuomboleza na kutafuta majibu kuhusu yaliyotokea, ambapo watu 518 walipoteza maisha.

Katika kumbukizi hiyo, viongozi wa dini wamehimiza maombi, toba na mshikamano wa kitaifa, huku Kituo cha Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC) kikitoa mapendekezo 10 ya hatua zinazopaswa kuchukuliwa ili kuzuia matukio kama hayo kujirudia.

Kwa upande wa viongozi wa Kanisa Katoliki, Katibu Mkuu wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Padri Charles Kitima amewataka Watanzania kulitafakari tukio la Oktoba 29, 2025, kama fundisho kuhusu kuheshimu uhai wa binadamu na kujenga upya mshikamano wa kitaifa.

Akizungumza katika misa ya kuwaombea waliofariki, Padri Kitima amesema maaskofu wanahimiza Watanzania kumrudia Mungu, kukiri makosa na kujirekebisha ili kuzuia matukio yanayohatarisha maisha ya wananchi yasijirudie.

Amesema kumbukizi ya waathirika inapaswa kwenda sambamba na mabadiliko ya matendo, akiwataka wananchi kuacha kulaumiana na badala yake kuanza kufanya mema katika maeneo yao ya uwajibikaji.

“Wema tukizidisha, uovu tutaushinda. Yesu anasema, ‘Tubuni’, nataka tubadilike; wewe mwenyewe anza kwa kutenda mema katika sekta unayoona inaleta madhara makubwa,” amesema.

Padri Kitima ambaye katikati ya misa hiyo aliwataja baadhi ya watu waliotekwa na wengine kukutwa wamefariki dunia, wakiwemo Ally Kibao na Deusdedith Soka, amesema kuwaombea waliopoteza maisha katika vurugu za Oktoba 29, kunapaswa kwenda sambamba na hatua za kujirekebisha, akiwataka Watanzania kuacha tabia zinazochochea uovu na badala yake kujenga utamaduni wa upendo, unyenyekevu na kusameheana.

Amesema tukio la Oktoba 29, 2025 linapaswa kuwa nafasi ya Watanzania kukiri makosa, kuomba msamaha na kushirikiana katika kujenga taifa linaloheshimu haki na uhai wa kila mtu.

Padri Kitima ameonya dhidi ya kutumia tofauti za kisiasa na masuala ya uongozi kama sababu ya Watanzania kuumizana, akisisitiza umuhimu wa kuhifadhi historia ya nchi ya kuishi pamoja licha ya tofauti.

Katika wito wake, Padri Kitima aliwataka Watanzania kuacha kulaumiana na badala yake kuanza mabadiliko kwa kutenda mema katika maeneo yao ya uwajibikaji.

Amesema toba ya kweli inapaswa kuambatana na matendo, akiwataka wananchi kutambua mambo yanayoweza kuleta madhara katika jamii na kuyafanyia kazi.

Katika kumbukizi hiyo, Kardinali Protase Rugambwa ameeleza umuhimu wa kuwaombea watu waliopoteza maisha, akisema kuwakumbuka ni kutambua uhusiano wao wa kifamilia, kijamii na kiimani na watu waliowaacha.

Amesema marehemu hawawezi kusahaulika kwa sababu ya mchango wao katika familia na jamii, akirejelea mfano wa Yesu Kristo aliyeutoa uhai wake kwa ajili ya wengine.

“Tunawakumbuka kwa sababu wamekaa nasi katika damu, mwili na imani, wakiacha alama ya pekee kabisa katika maisha yetu,” amesema.

Ukweli dhidi ya kupotosha

Kwa upande wake, Rais wa TEC, Askofu Wolfgang Pisa, ametoa wito kwa Watanzania kukubali kuongozwa na ukweli na kuacha kuupotosha, akisisitiza kuwa ukweli unapaswa kuwa msingi wa maamuzi ya kitaifa, ikiwemo masuala ya uchaguzi, haki na usalama.

Akizungumza wakati wa maadhimisho la misa ya kuwaombea marehemu hao, iliyofanyika katika Parokia ya Mtakatifu Andrea Kaggwa, Kanisa Kuu la Jimbo Katoliki Lindi, Askofu Pisa amesema ukweli unaongoza.

“Sisi hatuna ukweli, ila ukweli una sisi, sisi hatuwezi kumiliki ukweli, ila ukweli unaweza kutumiliki sisi, ukweli unaongoza,” amesema.

Amesema ukweli hauhitaji kupotoshwa au kulazimishwa ili ukubalike, akitumia mfano wa msalaba kueleza kuwa baadhi ya mambo yana uhalisia wake ambao hauhitaji mtu kuubadilisha ili kuufanya ukubalike.

“Kwa hiyo, tukubali kumilikiwa na ukweli, uongozi unao ukweli, tusijaribu kupotosha ukweli,” amesisitiza.

Akirejea Injili ya Marko 6: 17- 29, Askofu Pisa ameeleza umuhimu wa kusimamia ukweli hata pale ambapo kufanya hivyo kunahitaji kujitoa mhanga.

Amesema simulizi hiyo inaonyesha namna Yohana Mbatizaji alivyokabiliana na suala la ukweli licha ya gharama kubwa aliyolazimika kulipa.

Askofu huyo alitumia pia simulizi la Herodia kuonya dhidi ya kupotosha ukweli kwa lengo la kulinda uovu, akisisitiza kuwa watu wanapaswa kuchagua kusimamia yaliyo mema badala ya kutetea makosa.

Katika muktadha huo, aligusia suala la uchaguzi na Katiba, akisema kuna hoja kuhusu mfumo wa sasa wa uchaguzi na uwezo wake wa kuhakikisha uchaguzi wa haki, wa kweli na salama zinapaswa kutazamwa kwa kuzingatia ukweli.

“Tukisema sheria ya sasa ya uchaguzi, Katiba ya sasa haiwezi kutoa uchaguzi wa haki, wa ukweli na usalama, kwenye ukweli ni ukweli ambao unapaswa kutuongoza,” amesema.

Mbali na kusisitiza ukweli, Askofu Pisa ametoa wito kwa watu wenye ushawishi katika taasisi mbalimbali kutumia nafasi zao kuhimiza hatua zinazoweza kuzuia maovu na kusaidia jamii kuepuka kurudia matukio yanayosababisha madhara.

Akitumia mfano wa Malkia Esta katika Biblia, ameeleza jinsi watu wenye nafasi na ushawishi wanavyoweza kutumia nafasi zao kusaidia wengine na kuzuia maafa.

Alisema kama ilivyokuwa kwa Esta, ambaye alitumia nafasi yake kusaidia kuokoa Wayahudi waliokuwa hatarini kuuawa, watu wenye ushawishi katika taasisi mbalimbali wanapaswa kutimiza wajibu wao kwa manufaa ya jamii.

Katika sehemu nyingine ya mahubiri yake, Askofu Pisa aliwataka Watanzania kuendelea kutafuta yaliyo mema na kuacha uovu, akisisitiza umuhimu wa huruma, haki na amani katika maisha ya jamii na kutoa wito wa kuendelea kuliombea taifa na viongozi ili waongozwe katika kufanya maamuzi yanayozingatia mapenzi ya Mungu na masilahi ya wananchi.

Kwa upande wake Askofu Mkuu wa Jimbo Katoliki la Mwanza, Ranatus Nkwande amesema katika kuadhimisha mwaka mmoja baada ya matukio hayo, si vyema kubaki kulaumiana bali kupiga magoti kumlilia Mungu kama Taifa.

“Taifa lisilomtegemea Mungu ni Taifa ovu, watu wasiomtegemea Mungu na kumweka mbele, wapo katika maisha ya uovu wakati yeye ametuambia utafuteni kwanza ufalme wa mbingu na mengine yatakuja kwa ziada,” amesema.

Amesema ni vyema kumtafuta Mungu ili kuishi kwa haki na amani kwani kutafuta vitu na sifa za ulimwengu matokeo yake yanaweza kuwa mabaya kwa mmoja au kwa wote.

Uingereza, Marekani wakumbuka waathirika

Katika ujumbe wake wa Oktoba 29, 2026 uliowekwa kwenye akaunti ya X, Ubalozi wa Uingereza nchini Tanzania umesema unawakumbuka wote waliopoteza maisha kutokana na ghasia hizo mwaka 2025, huku ukitoa pole kwa familia na wengine walioathirika.

Ubalozi huo umesema Uingereza itaendelea kuunga mkono juhudi za kujenga Tanzania yenye amani, ustawi na umoja kwa manufaa ya Watanzania wote.

Kwa upande wake, jamii ya Ubalozi wa Marekani nchini Tanzania imewakumbuka marehemu na familia zinazoendelea kuomboleza na kutafuta majibu kuhusu yaliyotokea.

Katika ujumbe wake uliwekwa kwenye mtandao wa X wa ubalozi huo, mwakilishi huyo wa Marekani amesisitiza kuwa suala hilo halipaswi kufunikwa, akirejelea kauli aliyotoa wakati wa kusikilizwa na Seneti ya Marekani kabla ya kuthibitishwa kushika wadhifa wake.

Akizungumza kuhusu kumbukizi hiyo, Mratibu wa Kitaifa wa Mtandao wa Waytetezi wa Haki za Binadamu (THRDC), Onesmo Ole Ngurumwa amesema kuna haja ya kuchukua hatua za kitaifa zitakazosaidia kujenga mazingira ya amani, kulinda haki za binadamu na kuzuia kurudiwa kwa ghasia.

Miongoni mwa mapendekezo ya taasisi hiyo ni kuharakisha mchakato wa Katiba mpya kwa kuweka ratiba inayoeleweka na kuwashirikisha wananchi, vyama vya siasa, asasi za kiraia na wadau wengine.

THRDC pia imetaka kuwepo kwa utaratibu wa kuwasaidia waathirika kupata matibabu endelevu, huduma za afya ya akili, ushauri nasaha na msaada wa kisheria, pamoja na mfumo wa fidia kwa familia zilizopoteza wapendwa wao, majeruhi na walioathiriwa na uharibifu wa mali.

Kwa upande wake, Naibu Katibu Mkuu wa Shura ya Maimamu Tanzania, Abubakari Mngodo, akizungumza kwenye mkutano huo wa THRDC na wanahabari, amesema ni muhimu matukio ya Oktoba 29 yakakumbukwa kwa sababu yaliwaumiza wananchi.

“Kuwa na siku ya kukumbuka yaliyotokea ni muhimu. Matukio yale yalituumiza, tunashauri tuwe wakweli; uongo hautufikishi kokote. Serikali iwe na ukweli kuhusu yaliyotokea Oktoba 29,” amesema.

 Imeandikwa na Imani Makongoro na Baraka Loshilaa.

Source link

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *