TRA Zanzibar yakusanya Sh216.3 bilioni
2 mins read

TRA Zanzibar yakusanya Sh216.3 bilioni

Zanzibar. Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) Zanzibar imekusanya Sh216.3 bilioni katika robo ya kwanza ya mwaka wa fedha, ikiwa ni pungufu ya zaidi ya Sh29 bilioni ya lengo la Sh245.6 bilioni, hali iliyotajwa kuhitaji kuimarishwa kwa mikakati ya ukusanyaji wa mapato.

Aidha, kutokana na mwenendo huo, Waziri wa Fedha, Balozi Khamis Mussa Omar ameitaka TRA kuboresha usimamizi wa forodha, kutumia takwimu sahihi na kuimarisha ushirikiano na wadau wa biashara ili kuongeza ufanisi wa makusanyo na kuwezesha Serikali kutekeleza mipango ya maendeleo.

Akizungumza wakati wa ziara yake katika ofisi za TRA Zanzibar, Waziri wa Fedha alisema uchambuzi wa kina wa takwimu ni muhimu katika kubaini sababu za kupanda au kushuka kwa mapato na kuchukua hatua zinazolingana na hali halisi ya biashara.

Makusanyo ya Sh216.3 bilioni ni sawa na asilimia 88 ya lengo lililowekwa kwa kipindi hicho, yakiacha pengo la zaidi ya Sh29 bilioni.

Balozi Omar alisema uchambuzi huo unapaswa kuzingatia aina, kiasi na thamani ya bidhaa zinazoingia Zanzibar, pamoja na mabadiliko ya shughuli za kiuchumi na miradi ya maendeleo.

“Katika mwenendo wa makusanyo, uchambuzi wa kina wa takwimu ni muhimu katika kubaini mabadiliko ya biashara na sababu zinazochangia kupanda au kushuka kwa mapato,” alisema.

Aidha, alisisitiza kuwa ushirikiano kati ya TRA na Shirika la Bandari Zanzibar (ZPC) ni muhimu katika kulinganisha takwimu za mizigo na mwenendo wa mapato ili Serikali ipate taarifa sahihi za biashara.

Alitaka Idara ya Forodha kuimarisha mifumo ya ukaguzi na uthamini wa bidhaa pamoja na uhakiki wa nyaraka za uingizaji na uuzaji nje ya nchi, ili kuhakikisha kodi zinazostahili zinakusanywa kwa usahihi na kwa wakati.

Alisema hatua hizo zinapaswa kuambatana na matumizi ya takwimu na teknolojia ili kuboresha utendaji na kuongeza ufanisi wa ukusanyaji wa mapato.

Naye, Naibu Kamishna Mkuu wa TRA, Mcha Hassan Mcha alisema mamlaka hiyo itaendelea kufanyia kazi maelekezo ya Serikali kuhusu uboreshaji wa ukusanyaji wa kodi ili kusaidia kufikia malengo ya maendeleo.

“Ofisi ya TRA Zanzibar imewekewa lengo la kukusanya Sh1.144 trilioni, kiasi kinacholingana na asilimia 34 ya mapato ya kodi na yasiyo ya kodi yaliyopangwa katika bajeti ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar,” alisema.

Aidha, alisema mamlaka hiyo itafanya jitihada kuhakikisha lengo hilo linafikiwa, huku mapato hayo yakitarajiwa kutumika katika shughuli za maendeleo.

Ziara ya Waziri wa Fedha imelenga kutathmini mwenendo wa makusanyo, kujadili changamoto zilizopo na kubaini fursa za kuboresha utendaji katika kipindi kilichosalia cha mwaka wa fedha.

Source link

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *