Uhaba wa maji wakwamisha machinjio ya kuku majengo
3 mins read

Uhaba wa maji wakwamisha machinjio ya kuku majengo

Dodoma. Uhaba wa maji na kukatika kwa umeme vinakwamisha shughuli za machinjio ya kuku katika Soko Kuu la Majengo, Dodoma, huku mamlaka ya maji ikieleza kubaini hitilafu kwenye mtandao wa mabomba katika eneo hilo.

Machinjio hayo yanayosimamiwa na kikundi cha Jogoo Group, huchinja kuku kati ya 300 na 700 kwa siku kulingana na soko na  wanahudumia wafanyabiashara, wateja binafsi na hoteli zinazochukua kuku kwa wingi.

Katibu wa Jogoo Group, Ezra Nyagalu amesema licha ya kulipa bili  ya maji  inayofikia hadi Sh600,000 kwa mwezi, lakini bado  uhaba wa maji unawalazimisha waendeshaji kukodi gari na kwenda kuchota maji maeneo mengine ili kuhakikisha shughuli zinaendelea.

Nyagalu amesema pamoja na kuhifadhi maji kwenye mapipa, mara nyingi huisha mapema hasa nyakati za biashara inapochangamka kwani kiwango wanachokuwa nacho kama akiba huisha mapema.

“Hatuwezi kufanya kazi bila maji, asilimia kubwa ya shughuli zetu zinahitaji maji. Tunakodi gari mapema, tunachota maji na kujaza kwenye mapipa, lakini kutokana na shughuli kuwa nyingi, kufikia saa mbili au saa tatu maji yanaisha,” amesema Nyagalu.

Katibu ametaja changamoto nyingine ni kukatika kwa umeme kunakosababisha mashine za kunyonyoa kuku kushindwa kufanya kazi, hivyo kuwalazimu wafanyakazi kufanya kazi hiyo kwa mikono.

Amesema hali hiyo huongeza muda wa kuhudumia wateja, hasa wanaoleta kuku wengi, huku mteja mwenye kuku wachache akihudumiwa ndani ya dakika 10 hadi 15 wakati si kawaida yao.

Ametaja gharama ya kuchinja kuku mmoja kuwa ni Sh500 kwa mteja anayeleta kuku watano, huku wanaoleta kuku kuanzia 10 au zaidi  wanatozwa Sh300 kwa kuku.

Akizungumzia suala la maji, Mkurugenzi wa usambazaji Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Dodoma (Duwasa), Bernard Rugayi amekiri kuwepo kwa tatizo hilo kwenye mifumo ya Maji ndani ya soko la majengo.

Amesema hitilafu inatoka kwenye mtandao wa mabomba unaopeleka maji katika eneo la machinjio na tayari imeanza kuishughulikia.

Rugayi amesema wataalamu wa mamlaka hiyo walitembelea eneo hilo kuchunguza chanzo cha tatizo na kubaini kuwa hitilafu hiyo ndiyo inayosababisha maji kukatika mara kwa mara.

“Soko la Majengo ni mojawapo ya maeneo nyeti ambayo hayapaswi kukatika maji kama ilivyo maeneo mengine yaliyopo katikati ya jiji, lakini tumebaini kuna hitilafu inayosababisha hali hiyo ambayo tumeshaanza kuifanyia kazi,” amesema Rugayi.

Ameeleza kuwa maeneo mengine ya soko hilo hupata maji kuanzia asubuhi hadi saa nane mchana, lakini eneo la machinjio limekuwa likikabiliwa na hali tofauti kutokana na hitilafu hiyo.

Wakati huo huo, mteja wa machinjio hayo, Benedict Ngoe, amesema kwa sasa wameanza kuona ufanisi ukipungua tofauti na Mwanza hasa kwenye suala la usafi kutokana na kupungua kwa maji.

Ngoe anasema damu na maji yanayomwagika katika eneo la machinjio yanapaswa kudhibitiwa, huku akishauri kuongeza wafanyakazi na mashine za kunyonyoa kuku ili kupunguza muda wa kusubiri kipindi ambacho maji yanakosekana.

Hata hivyo, mkazi wa Maili Mbili, Lusia Samuel, amesema anaridhishwa na huduma anazopata katika machinjio hayo, akitaja ukarimu wa wahudumu na kasi ya huduma kuwa miongoni mwa mambo yanayomvutia.

Source link

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *