CoRI yataka uchunguzi vifo vya waandishi watatu Uchaguzi Mkuu 2025
Dar es Salaam. Umoja wa Haki ya Kupata Taarifa (CoRI), umetaka uchunguzi wa haraka na wa haki kuhusu vitisho na mashambulizi dhidi ya waandishi wa habari, ambapo wanahabari watatu walifariki wakiwa kazini wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025.
Wito huo umetolewa leo Alhamisi, Oktoba 29, 2026, na Mwenyekiti wa CoRI, Ernest Sungura, wakati wa maadhimisho ya awali ya Siku ya Kimataifa ya kutokomeza uonevu dhidi ya waandishi wa habari yaliyofanyika jjini Dar es Salaam.
Sungura amesema kwa mujibu wa taarifa mbalimbali, zaidi ya wananchi 500 walipoteza maisha katika kipindi cha Uchaguzi Mkuu wa mwaka jana, akisisitiza umuhimu wa ukweli kujulikana na haki kutendeka kwa waathirika.
“Hatupo hapa leo kutafuta nani alaumiwe, tupo hapa kuomboleza pamoja kama Watanzania,” amesema Sungura.
Amesema kila maisha yaliyopotea ni pigo kwa demokrasia na kwamba kutowajibishwa kwa wahusika wa vitendo vya ukiukwaji, hakupaswi kuendelea.
“Kwa ajili ya familia, kwa ajili ya taaluma ya habari, na kwa ajili ya uponyaji wa Taifa, kupata ukweli kwa njia ya uwazi na haki bado ni muhimu sana,” amesema.
Amesema shambulio dhidi ya mwandishi wa habari si suala linalomhusu mwandishi pekee, bali pia linaathiri haki ya wananchi kupata taarifa na uwezo wa vyombo vya habari kutekeleza wajibu wake kwa jamii.
Kwa mujibu wa tathmini ya Baraza la Habari Tanzania (MCT) matukio 12 yaliyothibitishwa ya ukiukwaji dhidi ya waandishi wa habari, yameripotiwa mwaka 2026, ikilinganishwa na matukio 51 mwaka 2025 na 33 mwaka 2024
Amesema matukio hayo yanahusisha kukamatwa, vitisho na kuzuiwa kwa waandishi kutekeleza majukumu yao, huku akifafanua kuwa takwimu hizo ni za matukio yaliyothibitishwa na huenda zisiwe jumla kamili ya ukiukwaji wote.
Aidha, ameeleza kuwa waandishi wanaoripoti masuala ya siasa, uchaguzi na uchunguzi wako katika hatari zaidi, wakiwamo waandishi wa kujitegemea, wa mtandaoni na wanawake wanaokabiliwa na vitisho vya kijinsia na kidijitali.
Katika hatua nyingine, Sungura amesema Tanzania imeshuka kutoka nafasi ya 95 mwaka 2025 hadi nafasi ya 117 kati ya nchi 180 katika Ripoti ya Uhuru wa Habari Duniani ya mwaka 2026 iliyotolewa na shirika la Reporters Without Borders (RSF)
Sungura amesema hatua za kulinda waandishi zinapaswa kwenda zaidi ya kurekodi matukio ya ukiukwaji na kutoa taarifa, kwa kuhakikisha uchunguzi unafanyika na wahusika wanawajibishwa.
“Mtihani halisi ni uchunguzi, upatikanaji wa haki, na uwajibikaji wa hatari aliyokutana nayo mwandishi na kupatiwa haki yake,” amesema.
Amevitaka vyombo vya sheria kuchunguza kwa haraka na haki vitisho na mashambulizi dhidi ya waandishi wa habari ili kuhakikisha waathirika wanapata haki.
Pia amezitaka mamlaka za udhibiti kutoa sababu za kisheria zilizo wazi zinapochukua hatua dhidi ya wanahabari na kuheshimu haki yao ya kusikilizwa na kukata rufaa.
Kwa upande wa Serikali na Bunge, amesema ni muhimu kupitia sheria zinazoathiri uhuru wa habari na haki ya kupata taarifa ili ziendane na Katiba na mikataba ya kimataifa.
Aidha, amewataka wamiliki wa vyombo vya habari kuimarisha usalama wa waandishi kazini, kufanya tathmini ya hatari wanazoweza kukutana nazo wanaporipoti na kuhakikisha wanapata msaada wa kisheria na kisaikolojia wanapokumbwa na madhila.
Mbali na hilo, Sungura amesema CoRI inaunganisha wadau 22 wenye lengo la kulinda haki ya wananchi kupata taarifa kwa kuhakikisha waandishi wanafanya kazi katika mazingira salama.
Amesema umoja huo si jukwaa la upinzani, bali ni la ushirikiano katika utetezi wa pamoja, kushirikiana na wenye wajibu na kutafuta suluhisho kuhusu uwazi, uwajibikaji na usalama wa waandishi.
“CoRI si sauti ya upinzani, ni jukwaa la ushirikiano,” amesema
Ameeleza kuwa umoja huo utaendelea kusaidia ufuatiliaji wa kesi zinazohusu ukiukwaji dhidi ya waandishi wa habari na kushirikiana na wadau mbalimbali kuhakikisha masuala hayo yanapatiwa ufumbuzi.
Sungura ametangaza kuwa maadhimisho hayo yataendelea mkoani Iringa Novemba 2, 2026, akisisitiza kuwa waandishi wanaofanya kazi nje ya miji mikubwa wanastahili ulinzi sawa na wenzao walioko mijini
Amesema ahadi za kulinda waandishi wa habari zinapaswa kutekelezwa kwa vitendo ili kukomesha kutowajibishwa kwa wahusika, kuimarisha demokrasia na kulinda haki ya kila raia kupata taarifa.
