Migongano ya taasisi, siasa inavyokwamisha mipango miji
5 mins read

Migongano ya taasisi, siasa inavyokwamisha mipango miji

Arusha. Migongano kati ya siasa na ushauri wa kitaalamu, mifumo ya Serikali kutounganishwa na ukosefu wa uratibu miongoni mwa taasisi zinazohusika na maendeleo ya miji ni miongoni mwa changamoto zinazokwamisha utekelezaji wa mipango miji na kuchangia ukuaji holela wa miji nchini.

Hayo yamesemwa leo Alhamisi, Oktoba 29, 2026 na mkufunzi na mtaalamu wa mipango miji na mifumo ya taarifa za kijiografia (GIS) katika Chuo Kikuu Ardhi (ARU), jijini Dar es Salaam, Amedeus Kimaro, alipokuwa  akizungumza katika mkutano wa 11 wa mwaka wa wataalamu wa mipango miji unaoendelea jijini Arusha.

Kimaro amesema changamoto hizo zinasababisha mipango inayoandaliwa na wataalamu kutotekelezwa ipasavyo, huku lawama zikielekezwa kwa upande mmoja, badala ya kutambua kuwa ukuaji wa miji unahusisha Serikali, wananchi na wataalamu.

Amesema kila upande una wajibu wake katika kuhakikisha miji inakua kwa mpangilio, akieleza kuwa wataalamu wanapaswa kuandaa mipango kwa kuzingatia taaluma zao, huku Serikali ikihakikisha rasilimali zinazotengwa kwa ajili ya mipango hiyo zinatumika ipasavyo.

“Tusilaumu upande mmoja tu, kuna majukumu ya kila upande. Kuna upande wa Serikali, wananchi, lakini pia kuna wataalamu,” amesema.

Hata hivyo, amesema changamoto hujitokeza pale mipango inayoandaliwa kwa kuzingatia ushauri wa kitaalamu inapokutana na ajenda za kisiasa na mahitaji ya muda mfupi.

Ameeleza kuwa mtaalamu anaweza kuandaa mpango unaotenga maeneo ya wazi, taasisi, makazi na barabara, lakini utekelezaji wake ukaathiriwa na maamuzi yanayofanywa kwa kuzingatia masilahi mengine.

“Wataalamu wanatengeneza mchoro mzuri uliopangwa sawasawa, una maeneo ya wazi, maeneo ya taasisi, makazi na barabara. Lakini mwanasiasa anaweza kuja na ajenda yake akitaka mpango huo utekelezwe kwa haraka kwa sababu anataka kuwafurahisha wananchi, bila kuzingatia kikamilifu ushauri wa kitaalamu. Hapo ndipo changamoto ya ukuaji holela wa miji inapoanzia,” amesema.

Kimaro amesema hali hiyo inaonyesha umuhimu wa kuweka utaratibu unaofafanua nafasi ya wanasiasa, wataalamu na wananchi katika hatua mbalimbali za kupanga na kutekeleza mipango ya miji.

Ametaja changamoto nyingine kuwa ni mifumo ya Serikali kutounganishwa ipasavyo, licha ya kuwepo kwa mipango mbalimbali inayolenga kukabiliana na ukuaji holela wa miji na majanga yanayotokana na hali hiyo.

Amesema kutokuwepo kwa uhusiano wa kutosha kati ya mifumo hiyo kunaweza kusababisha taasisi moja kutekeleza shughuli zake bila kuzingatia mipango ya taasisi nyingine.

Pia, amesema taasisi zinazohusika na maendeleo ya miji bado hazina lengo na mwelekeo wa pamoja, hali inayosababisha kila moja kutanguliza ajenda zake.

Kimaro amesema changamoto hizo hujitokeza zaidi wakati majanga yanapotokea, ambapo wataalamu hutafutwa baada ya madhara kutokea badala ya kushirikishwa tangu hatua za awali za kupanga na kutekeleza miradi.

“Mipango miji muda mwingi wamekuwa wakumbukwa pale ambapo majanga yanatokea.”

“Muhimu taasisi za Serikali na binafsi kukaa pamoja na kuamua lengo moja, kuwa na mfumo mmoja na kuwa na dira moja kwamba nchi tunaamua kufanya nini,” amesema.

Amesema hatua hiyo itasaidia kupunguza migongano kati ya taasisi, kuunganisha mifumo na kuhakikisha mipango ya miji inatekelezwa kwa kuzingatia mahitaji ya sasa na ya baadaye.

Kwa upande wake, Ofisa Mipangomiji kutoka Kamisheni ya Ardhi Zanzibar, Mary Mageta amesema matumizi ya mifumo ya kidijitali katika usimamizi wa ardhi yanaweza kusaidia kupunguza migogoro ya ardhi na kuongeza uwazi katika usimamizi wa rasilimali hiyo.

Amesema Zanzibar inaendelea na mradi wa Mfumo wa Usimamizi wa Usajili wa Taarifa za Ardhi nchini (LARIS), unaolenga kuweka taarifa za ardhi katika mfumo wa kidijitali ili kurahisisha upatikanaji wake.

“Kwenye maeneo ambayo yamejengwa kiholela, changamoto kubwa ni huduma kufikiwa huko, unaweza kuwaza barabara utaipeleka vipi huko, shule unaweka wapi, wakati maeneo yameshajaa,” amesema.

Amesema hali hiyo pia inaweza kuathiri mazingira na usimamizi wa taka, huku gharama za kupeleka huduma zikiongezeka pale makazi yanapojengwa bila mpangilio.

“Ukipanga vizuri, unakuwa na maeneo ya huduma, unakuwa na barabara na unakuwa na maeneo ambayo yanaweza kutumika kwa shughuli mbalimbali za kijamii,” amesema.

Akizungumzia hali ya Zanzibar, Mageta ametolea mfano wa maeneo ya Jang’ombe na Mbweni, akieleza kuwa tofauti za miundombinu na upatikanaji wa huduma za jamii huathiri namna wananchi wanavyoendeleza makazi na shughuli zao.

“Kwa mfano tukizungumzia Zanzibar, tunazungumzia maeneo ya Jang’ombe, mazingira ni hali duni. Lakini tukizungumzia Mbweni, tunaona watu wa hali fulani,” amesema.

Amesema upatikanaji wa miundombinu kama maji, umeme na maeneo ya biashara huathiri mtazamo wa wananchi kuhusu maendeleo ya maeneo wanayoishi.

“Wananchi wanapokaa eneo fulani ambalo lina huduma za jamii nzuri, wanakuwa nao pia wanafikra ya kuendeleza mji wao,” amesema.

Mmoja wa wakazi wa eneo la Ngaramtoni ya Chini, Arusha, Joseph Lomayan amesema ujenzi holela wa makazi umekuwa kikwazo cha upatikanaji wa huduma muhimu, zikiwemo barabara, maji na mifumo ya maji taka.

“Kuna maeneo nyumba zimejengwa bila mpangilio, barabara ni nyembamba na nyingine hazipitiki kirahisi, hivyo hata magari ya huduma za dharura yanapata shida kufika. Serikali inapaswa kusimamia mipango ya makazi kabla maeneo hayajajaa nyumba,” amesema.

Source link

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *