Nchi zinazozunguka Ziwa Tanganyika zakumbushwa jukumu la uhifadhi wa rasilimali
Dar es Salaam. Nchi zinazozunguka Ziwa Tanganyika zimetakiwa kuimarisha ushirikiano wa kikanda, kuhakikisha upatikanaji wa fedha za uhifadhi na kuboresha usimamizi wa rasilimali ili kulinda mfumo wa ikolojia wa ziwa hilo na kudumisha maisha ya takribani watu milioni 13 wanaotegemea bonde la ziwa hilo.
Mamlaka ya Ziwa Tanganyika (LTA) inaundwa na nchi nne zinazolizunguka ziwa hilo ambazo ni pamoja na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Tanzania, Zambia na Burundi.
LTA imepewa jukumu la kusimamia uendelevu za ziwa na kulihifadhi kwa manufaa ya mataifa hayo.
Wito huo umetolewa leo Alhamisi, Oktoba 29, 2026, na mwenyekiti wa mkutano wa mawaziri wa Mamlaka ya Ziwa Tanganyika, Dk Douty Chibamba wakati wa ufunguzi wa mkutano wa maandalizi kuelekea mkutano wa 14 wa mawaziri, utakaofanyika jijini Dar es Salaam.
Dk Chibamba amesema mkutano huo umelenga kuhakikisha nyaraka muhimu za kiufundi, kitaasisi na kifedha zinachambuliwa kwa kina kabla ya kuwasilishwa kwa mawaziri kwa ajili ya kujadiliwa na kuidhinishwa.
Amesema mkutano huo wa maandalizi umefuatia azimio lililopitishwa katika mkutano wa 13 wa mawaziri uliofanyika Livingstone, Zambia, mwaka jana.
Azimio hilo limetaka kufanyika kwa mkutano wa maandalizi ili kupitia nyaraka muhimu na kuwezesha mawaziri kufanya uamuzi wenye taarifa na uchambuzi wa kutosha katika mkutano unaofuata.
“Kazi yetu si kupitia nyaraka pekee, bali kuhakikisha masuala yanayowasilishwa yanachambuliwa ipasavyo na hatua zinazopendekezwa zinawezekana kutekelezwa na kufikiwa,” amesema Dk Chibamba.
Ameongeza kuwa, mapendekezo yatakayowasilishwa kwa mawaziri yanapaswa kuzingatia tathmini sahihi na kuakisi masilahi ya pamoja ya nchi zote nne zinazopakana na ziwa hilo.
Miongoni mwa masuala muhimu yanayojadiliwa ni mpango kazi na bajeti ya mwaka 2027 ya Mamlaka ya Ziwa Tanganyika.
Dk Chibamba amesema shughuli zinazopangwa zinapaswa kuendana na Mkataba wa Usimamizi Endelevu wa Ziwa Tanganyika pamoja na Mpango Mkakati wa Utekelezaji ulioboreshwa.
“Ni muhimu pia kuhakikisha vipaumbele vyetu vinaendana na upatikanaji wa fedha za kutosha na zinazotabirika, ikiwamo kutekelezwa kwa wakati kwa wajibu wa kifedha wa nchi wanachama,” amesema.
Ameonya kuwa bila rasilimali za kutosha za kifedha na rasilimali watu, utekelezaji wa programu zilizokubaliwa na kufikiwa kwa malengo ya uhifadhi utaendelea kuwa changamoto.
Mkutano huo pia unapitia ripoti ya mwaka ya mamlaka hiyo ili kutathmini maendeleo ya utekelezaji wa programu zilizokubaliwa, kubaini changamoto ambazo bado hazijatatuliwa na kupendekeza maboresho ya utendaji wa taasisi hiyo.
Suala jingine muhimu ni pendekezo la kufanya uchimbaji wa tope na mchanga katika Mto Luga, pamoja na upembuzi yakinifu wa ujenzi wa bwawa la kudhibiti viwango vya maji katika Ziwa Tanganyika na kukabiliana na hatari ya mafuriko.
Dk Chibamba amesema mapendekezo hayo yanahitaji tathmini ya kina kutokana na athari zinazoweza kujitokeza kwa jamii, miundombinu, mifumo ya ikolojia na shughuli za kiuchumi katika bonde la ziwa hilo.
“Tathmini yetu inapaswa kuongozwa na ushahidi wa kisayansi, uwezekano wa utekelezaji wa kiufundi, hatua za kulinda mazingira na jamii, pamoja na kuhakikisha uendelevu wa muda mrefu wa hatua zozote zitakazopendekezwa,” amesema.
Wajumbe, pia, wanatarajiwa kupitia tathmini za kisayansi kuhusu akiba ya samaki katika ziwa hilo na nyaraka nyingine zinazohusiana na uvuvi.
Matokeo ya tathmini hizo yanatarajiwa kusaidia majadiliano kuhusu uhifadhi wa samaki, uvuvi endelevu na ulinzi wa maisha ya watu wanaotegemea rasilimali za majini.
Aidha, Dk Chibamba ametaka kuboreshwa kwa utawala wa mamlaka hiyo, uwajibikaji, rasilimali watu, uratibu baina ya nchi wanachama na mikakati ya kupata fedha.
“Mamlaka imara na yenye ufanisi ni muhimu katika kubadilisha ahadi za kikanda kuwa matokeo yanayopimika katika utekelezaji,” amesema.
Amewataka wajumbe kubaini changamoto zinazoikabili taasisi hiyo na kuandaa mapendekezo ya vitendo yanayotegemea ushahidi.
“Lazima tuwe wakweli katika kubaini changamoto zinazoikabili mamlaka, tuwe na uhalisia katika kupendekeza suluhisho na tuungane katika dhamira yetu ya kulinda Ziwa Tanganyika kwa manufaa ya vizazi vya sasa na vijavyo,” amesema Dk Chibamba.
Naibu Waziri katika Ofisi ya Makamu wa Rais anayeshughulikia Muungano na Mazingira, Reuben Kwagilwa amesema Tanzania itaendelea kushirikiana na nchi nyingine wanachama kulinda ziwa hilo na kukuza maendeleo ya kiuchumi endelevu.
Amelitaja Ziwa Tanganyika kuwa rasilimali muhimu ya asili, akibainisha kuwa bioanuwai yake na rasilimali za majini zinawezesha mamilioni ya watu wanaoishi katika bonde lake kujipatia kipato na kuendesha maisha yao.
“Tanzania, kama nchi mwanachama, itaendelea kushirikiana na nchi zote wanachama kuhakikisha Mkataba wa Usimamizi Endelevu wa Ziwa Tanganyika unatekelezwa kikamilifu na kwa vitendo,” amesema Kwagilwa.
Ameongeza kuwa Tanzania iko tayari kushirikiana na nchi wanachama pamoja na wadau wengine kulinda mfumo wa ikolojia wa ziwa hilo huku ikikuza uchumi wa buluu endelevu.
Mapendekezo yatakayopatikana yanatarajiwa kusaidia uamuzi wa mawaziri kuhusu kuimarisha utendaji wa mamlaka hiyo na kuhakikisha usimamizi endelevu wa Ziwa Tanganyika kwa manufaa ya vizazi vijavyo.
LTA ni Mamlaka ya Ziwa Tanganyika inayoratibu ushirikiano wa nchi nne zinazomiliki kwa pamoja rasilimali za ziwa hilo.
Jukumu lake kuu ni kuhakikisha Ziwa Tanganyika na bonde lake vinasimamiwa kwa njia endelevu, huku rasilimali zake zikitumika kwa manufaa ya watu wa sasa na vizazi vijavyo.
LTA imeanzishwa ili kuratibu utekelezaji wa mkataba wa kikanda unaolenga usimamizi wa pamoja wa ziwa na bonde lake.
Sababu kuu ni kwamba shughuli zinazofanyika katika nchi moja zinaweza kuathiri nchi nyingine kupitia maji, uchafuzi, uvuvi na mabadiliko ya mazingira.
Mkataba huo unatambua changamoto kama uvuvi kupita kiasi na kupungua kwa akiba ya samaki, uchafuzi wa maji kutokana na shughuli za binadamu, mmomonyoko wa ardhi na taka zinazoingia ziwani, uharibifu wa mazalia ya samaki na kupungua kwa bioanuwai na shughuli za maendeleo zinazoweza kuwa na athari zinazovuka mipaka ya nchi.
Majukumu ya msingi ya LTA ni pamoja na usimamizi endelevu wa uvuvi, kuratibu sera na hatua za pamoja za kulinda samaki, kudhibiti uvuvi usio endelevu na kuimarisha ufuatiliaji wa shughuli za uvuvi na kulinda ubora wa maji.
Majukumu mengine ni kusaidia juhudi za kuzuia uchafuzi, kupunguza mashapo na kushughulikia shughuli zinazohatarisha mfumo wa ikolojia, kuhifadhi bioanuwai na kuratibu juhudi za kulinda viumbe vya majini, makazi yake na rasilimali nyingine za asili.
