Tanzania, Angola zachukua hatua kuimarisha ushirikiano
5 mins read

Tanzania, Angola zachukua hatua kuimarisha ushirikiano

Dar es Salaam. Tanzania na Angola zimesaini mikataba minne ya ushirikiano katika sekta mbalimbali, hatua inayolenga kuimarisha uhusiano wa muda mrefu wa nchi hizo katika masuala ya kiuchumi na kijamii.

Nchi hizo zimekuwa na uhusiano tangu kipindi cha harakati za ukombozi wa mataifa ya Afrika. Baada ya Angola kupata uhuru mwaka 1975, zilianzisha rasmi uhusiano wa kidiplomasia.

Rais wa kwanza wa Angola, Hayati Agostinho Neto, alifanya ziara nchini Tanzania mwaka 1979, ikiwa ni ziara ya kwanza ya kitaifa ya kiongozi huyo nchini humo.

Leo Alhamisi, Oktoba 29, 2026, Rais Samia Suluhu Hassan amempokea mgeni wake Rais wa Angola, João Lourenço, Ikulu jijini Dar es Salaam. Viongozi hao wameshuhudia utiaji saini wa mikataba hiyo baada ya kufanya mazungumzo na baadaye kuzungumza na vyombo vya habari.

Mikataba iliyosainiwa inahusu kubadilishana wafungwa, ushirikiano katika sekta ya usafiri wa anga, mawasiliano na masuala ya hali ya hewa.

Akizungumza katika hafla hiyo, Rais Samia amesema ziara ya Rais Lourenço inaonyesha upendo wake kwa Tanzania, akieleza kuwa kiongozi huyo alimwalika mara mbili kutembelea Angola kabla ya yeye kukubali mwaliko wa kumtembelea Tanzania.

Kwa kuzingatia historia na uhusiano wa nchi hizo, Rais Samia amesema Tanzania imeamua kufungua tena ubalozi wake nchini Angola na kwamba hivi karibuni atateua balozi wa kuiwakilisha nchi katika kituo hicho.

Kuhusu ushirikiano wa kiuchumi, amesema nchi hizo zinataka kuanzisha safari za moja kwa moja kati ya Dar es Salaam na Luanda, hatua inayotarajiwa kufungua fursa zaidi katika sekta ya usafiri wa anga na kurahisisha safari baina ya nchi hizo.

“Tanzania na Angola ni nchi marafiki, zinazoongozwa na marais ambao wana dhamira ya kuimarisha uhusiano na ushirikiano kati ya mataifa yetu.

“Tangu Rais João Lourenço aingie madarakani, Serikali yake imechukua hatua mbalimbali katika sekta ya usafiri. Tanzania iko tayari kushirikiana na Angola katika eneo hili ili kubadilishana uzoefu na kuimarisha huduma za usafiri,” amesema.

Katika sekta ya mafuta, Rais Samia amesema wamekubaliana kuimarisha ushirikiano, akieleza kuwa Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) limeanza juhudi za kushirikiana na upande wa Angola katika eneo hilo.

Amesema Tanzania pia ina taasisi zinazohusika na utafiti wa kijiolojia na uchunguzi wa madini ambazo zinaweza kusaidia kuongeza thamani ya rasilimali zilizopo katika nchi hizo.

“Nimemweleza Mheshimiwa Rais João Lourenço kwamba Tanzania ina taasisi za madini, zikiwemo taasisi zinazohusika na utafiti wa kijiolojia na uchunguzi wa madini, ambazo zinaweza kusaidia kuongeza thamani ya rasilimali zetu.

“Pia, tumesisitiza umuhimu wa kutumia Kituo cha Madini cha Afrika, ambacho makao yake yako hapa Dar es Salaam. Kituo hiki ni muhimu sana kwa maendeleo ya sekta ya madini barani Afrika,” amesema.

Rais Samia amesema viongozi hao pia wamejadiliana kuhusu masuala ya kikanda na kimataifa, yakiwemo usalama na amani kusini mwa Afrika.

Amesema wamesikitishwa na hali ya usalama katika baadhi ya maeneo yenye migogoro, ikiwemo Mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), eneo la Maziwa Makuu na maeneo mengine ya bara la Afrika.

Aidha, amesema amemweleza Rais Lourenço kuhusu nafasi yake katika masuala ya afya ya mama na mtoto ndani ya Umoja wa Afrika (AU), ambako anahudumu kama kinara wa masuala hayo.

“Nimeomba Angola kuunga mkono ajenda hiyo na kufuata malengo ya Umoja wa Afrika ya kuhakikisha kuwa hakuna mama anayefariki wakati wa kujifungua, hakuna mtoto anayefariki wakati wa kuzaliwa, na kupunguza vifo vya watoto wachanga vinavyoweza kuzuilika,” amesema.

Lourenço ataka ushirikiano

Kwa upande wake, Rais Lourenço amezitaka Tanzania na Angola kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi na kibiashara ili kukuza maendeleo ya nchi hizo na kuboresha maisha ya wananchi.

Amesema mataifa ya Afrika hayapaswi kutanguliza ushirikiano na nchi za mbali huku yakipuuza fursa zinazopatikana ndani ya bara hilo.

Amesema licha ya Tanzania na Angola kuwa na uhusiano wa kihistoria na kidugu, bado kuna umuhimu wa kuimarisha ushirikiano wa kiuchumi ili nchi hizo zinufaike kwa pamoja kupitia rasilimali, uwezo na fursa zilizopo.

Rais Lourenço amesema hakuna nchi inayoweza kufikia malengo ya maendeleo ya kiuchumi na ustawi wa wananchi kwa kutegemea uwezo wake pekee, hivyo ni muhimu kujenga ushirikiano imara na mataifa mengine, hususan ya Afrika.

“Angola na Tanzania zikizidisha uhusiano huu, nina uhakika Angola itanufaika kwa kiasi kikubwa na Tanzania pia itanufaika,” amesema.

Ameeleza kuwa nchi hizo zimekuwa zikisaini mikataba ya ushirikiano na hati za makubaliano katika maeneo mbalimbali. Amesema mikataba iliyosainiwa wakati wa ziara hiyo itaweka msingi wa kisheria utakaorahisisha ushirikiano kati ya serikali hizo na wadau wengine.

Rais Lourenço amesema ziara yake imefanyika miaka 47 baada ya Rais wa kwanza wa Angola, Hayati Neto, kufanya ziara ya kwanza ya kitaifa nchini Tanzania. Amesema kipindi hicho kilikuwa kirefu kwa mataifa yenye uhusiano wa kindugu kama Tanzania na Angola.

Amesema ziara yake pia ni mwendelezo wa ziara mbili alizofanya Rais Samia nchini Angola, ikiwemo ziara ya kitaifa na nyingine ya kushuhudia heshima iliyotolewa kwa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, kwa kuipa jina lake hospitali mpya iliyojengwa nchini humo.

Ameeleza kuwa Tanzania na Angola zina nafasi ya kuongeza manufaa yatokanayo na uhusiano wao kwa kuimarisha ushirikiano katika maeneo yenye masilahi ya pamoja.

Source link

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *