Bandari ya Mbamba Bay kufungua fursa za biashara, ajira
5 mins read

Bandari ya Mbamba Bay kufungua fursa za biashara, ajira

Nyasa. Ajira, ujuzi wa ufundi na fursa za biashara ni miongoni mwa manufaa ambayo wananchi wameanza kupata kupitia ujenzi wa Bandari ya Mbamba Bay huku uwekezaji wa zaidi ya Sh75 bilioni ukitarajiwa kuimarisha usafirishaji wa mizigo na biashara kati ya Tanzania na nchi jirani.

Ujenzi wa bandari hiyo iliyopo wilayani Nyasa, Mkoa wa Ruvuma, umefikia asilimia 78 na unatarajiwa kukamilika Februari 26, 2027 kwa mujibu wa Mhandisi Msimamizi wa Mradi wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), John Paul.

Mradi huo unalenga kuimarisha usafirishaji wa madini, mazao ya kilimo, samaki na bidhaa za viwandani katika ukanda wa Ziwa Nyasa, na kuongeza fursa za biashara kati ya Tanzania, Malawi, Msumbiji na Zambia.

Manufaa ya awali yameanza kuonekana kwa baadhi ya wananchi wanaoshiriki shughuli za ujenzi na wafanyabiashara wanaohudumia wafanyakazi wa mradi huo baada ya kuanza kuona fursa na kuimarika kwa vipato vyao.

Mwananchi ilitembelea eneo la mradi huo juzi Oktoba 27, mwaka huu ambapo baadhi ya wafanyakazi walisema wamepata kipato cha kuendesha familia zao na kujifunza stadi za ufundi ambazo wanatarajia kuzitumia hata baada ya ujenzi kukamilika.

Cosmas John, mzaliwa wa Tukuyu mkoani Mbeya ni miongoni mwa wanufaika hao ambaye anaeleza kuwa ajira aliyonayo imemsaidia kupata kipato cha kila mwezi huku akijifunza uchomeleaji wa vyuma na matumizi ya baadhi ya mashine.

“Mradi huu umefungua fursa za ajira kwa vijana wengi ambao hawakuwa na kazi mitaani. Kupitia ajira hizi wamekuwa wakipata mishahara inayowasaidia kuendesha maisha yao pamoja na kuanzisha biashara ndogo ndogo,” alisema John.

Alisema alipoanza kazi hiyo hakuwa na maarifa mengi ya ufundi lakini alipata ujuzi anaoweza kutumia kujiajiri baada ya mradi kukamilika.

John alisema akifanikiwa kupata eneo dogo anaweza kuanzisha karakana ya uchomeleaji na kuendeleza maisha yake kwa kutumia maarifa aliyopata.

Naye, Gabriel Ndomba mkazi wa Nyasa alisema aliingia kwenye mradi huo bila kuwa na ujuzi wa useremala lakini sasa amejifunza kazi hiyo na anatarajia kujiajiri baada ya ujenzi kukamilika. “Naweza kusema hata tukimaliza hapa, nakwenda kufungua eneo langu na kuendelea na maarifa niliyoyapata, bila huu mradi ningeendelea kusota kitaa,” alisema Ndomba.

Biashara ndogo zapata wateja

Mbali na ajira na mafunzo ya ufundi, biashara ndogo zinazofanyika karibu na eneo la ujenzi zimeanza kunufaika na uwepo wa wafanyakazi.

Yosepha Mbunda, mama lishe anayefanya biashara karibu na mradi huo alisema biashara yake imechangamka ikilinganishwa na ilivyokuwa kabla ya ujenzi kuanza huku akitarajia wateja kuongezeka zaidi baada ya bandari kukamilika na kuanza kutoa huduma.

“Nina amini kama bandari ikikamilika na kuanza kufanya kazi, basi biashara yangu itaongezeka zaidi na zaidi kuliko ilivyo sasa,” alisema Mbunda.

Janeth Mapunda anayefanya biashara ya kukaanga samaki katika eneo hilo pia anasema hali ya biashara imebadilika ikilinganishwa na kipindi cha nyuma.

Anaiomba Serikali kuhakikisha mradi unakamilika kwa wakati ili wafanyabiashara wadogo wanufaike zaidi na fursa zitakazotokana na shughuli za bandari.

Miundombinu itakayojengwa

Akieleza kuhusu maendeleo ya mradi huo, Paul alisema eneo la Mbamba Bay lilichaguliwa baada ya upembuzi yakinifu uliofanyika mwaka 2023 kubaini umuhimu wake katika kuimarisha huduma za kibandari.

Alisema bandari hiyo itakuwa na gati lenye urefu wa mita 115 na upana wa mita 20, litakaloweza kuhudumia meli mbili zenye uwezo wa tani 5,000 kila moja kwa wakati mmoja.

Mradi pia unahusisha yadi ya mizigo yenye ukubwa wa mita za mraba 20,000, itakayokuwa na uwezo wa kuhifadhi makontena 4,000 kwa wakati mmoja. Ujenzi huo unatekelezwa na Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), kupitia mkandarasi M/s Xiamen Ongoing Construction Group Co. Ltd.

Pia kutakuwa na maghala yenye ukubwa wa mita za mraba 2,000, barabara ya zege inayounganisha bandari na barabara kuu, jengo la utawala na jengo la abiria lenye uwezo wa kuhudumia watu 400 kwa wakati mmoja.

Paul alisema miundombinu ya gati inalenga kuwezesha vyombo vya majini kupaki wakati wote bila kuathiriwa na mabadiliko ya kina cha maji ziwani.

“Kukamilika kwa miundombinu hiyo kutapanua uwezo wa bandari kuhudumia mizigo na kuimarisha usafirishaji wa bidhaa katika ukanda huo,” alisema.

Kuunganisha ushoroba wa kusini

Paul alisema uwekezaji huo unatarajiwa kuimarisha Mtwara Corridor kwa kuunganisha Bandari ya Mtwara kupitia Songea na Mbamba Bay na hivyo kuwezesha mizigo kuelekea masoko ya nchi jirani.

Alisema njia hiyo itatoa fursa ya kuimarisha biashara katika ukanda wa Ziwa Nyasa na kuongeza matumizi ya bandari katika usafirishaji wa mizigo.

Kwa upande wake, Mhandisi Mkazi wa Kampuni ya Anova, Agathon Mwenda alisema kazi zinaendelea vizuri na wana dhamira ya kukamilisha ujenzi ifikapo Februari 26, 2027 kwa mujibu wa mkataba. “Mradi huu umekuwa fursa kwa vijana wa Kitanzania kupata ajira, uzoefu na ujuzi kupitia ushiriki wao katika shughuli mbalimbali za ujenzi,” alisema.

Kwa mujibu wa Mwenda, takribani asilimia 70 ya wataalamu walioshiriki katika mradi huo ni wazawa na Watanzania ambao wamepata uzoefu wa kutekeleza miradi mikubwa ya miundombinu ya bandari.

Mbarawa ataja manufaa ya bandari

Julai 11, 2026, Waziri wa Uchukuzi, Profesa Makame Mbarawa alipotembelea mradi huo alisema Bandari ya Mbamba Bay ni mradi wa kimkakati wa taifa unaolenga kuunganisha Tanzania na nchi jirani kupitia Ziwa Nyasa.

Alisema Serikali itaendelea kuwekeza katika miundombinu ya kimkakati ili kukuza uchumi, biashara na utalii huku akisisitiza umuhimu wa kukamilisha mradi kwa wakati na kuzingatia ubora na thamani ya fedha za umma.

“Serikali kupitia Kampuni ya Meli Tanzania (Tashico) inaendelea kuimarisha usafiri wa majini katika Ziwa Nyasa huku meli ya MV Njombe ikitarajiwa kusafirisha makaa ya mawe kutoka Mbamba Bay kwenda Monkey Bay nchini Malawi,” alisema.

Source link

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *