ACT-Wazalendo kuanza ziara ya siku 20 mikoa minane
Dar es Salaam. Chama cha ACT-Wazalendo kinatarajia kuanza ziara ya siku 20 katika mikoa minane ya Tanzania Bara.
Ziara hiyo itaanza Novemba Mosi, 2026, ikiwa ni sehemu ya kuimarisha mawasiliano na wananchi na kujadili masuala mbalimbali yanayohusu maslahi ya umma.
Ziara hiyo itahusisha mikutano ya hadhara itakayowakutanisha viongozi wa kitaifa wa chama hicho na wananchi, kwa lengo la kusikiliza kero zao, kujadili changamoto zinazowakabili na kutoa nafasi ya kuzungumzia ajenda mbalimbali za kitaifa.
Akizungumza leo Ijumaa, Oktoba 30, 2026, Naibu Katibu wa Habari, Uenezi na Uhusiano na Umma wa ACT-Wazalendo, Shangwe Ayo amesema ziara hiyo itaongozwa na Makamu Mwenyekiti wa chama hicho Tanzania Bara, Isihaka Mchinjita, akiambatana na Naibu Waziri Mkuu kivuli ambaye pia ni Waziri Mkuu kivuli wa chama hicho, Luhaga Mpina.
Amesema viongozi hao watatembelea maeneo ya Kanda ya Ziwa, Magharibi na Nyanda za Juu Kusini, ikiwemo Simiyu, Kahama, Geita, Kagera, Kigoma, Rukwa, Mbeya na Morogoro.
“Viongozi hao watatembelea mikoa ya Kanda ya Ziwa, Magharibi na Nyanda za Juu Kusini, ikiwemo Simiyu, Kahama, Geita, Kagera, Kigoma, Rukwa, Mbeya na Morogoro,” amesema.
Shangwe amesema katika ziara hiyo, chama kitatumia fursa ya mikutano ya hadhara kupima na kutathmini uwajibikaji wa Serikali ya CCM katika kutekeleza majukumu yake.
Amesema miongoni mwa ajenda zitakazojadiliwa ni masuala yaliyoibuliwa katika ripoti mbalimbali za Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), madai ya ufisadi nchini pamoja na uwajibikaji wa Serikali kufuatia vifo vya wananchi vilivyotokea wakati wa vurugu za Oktoba 29, 2025.
Ajenda ya matukio ya Oktoba 29 inakuja mwaka mmoja baada ya Uchaguzi Mkuu ulioambatana na vurugu zilizochangia vifo, majeruhi na uharibifu wa mali.
Wakati huo, Rais Samia Suluhu Hassan tayari ameunda Tume ya kuchunguza chanzo cha matukio ya kabla na baada ya uchaguzi iliyoongozwa na Jaji Othman Chande, pamoja na tume nyingine ya jinai iliyokuwa na jukumu la kuchunguza wahusika wa matukio hayo, iliyoongozwa na Jaji Shabani Lila.
Kwa mujibu wa Shangwe, ziara hiyo itahusisha viongozi mbalimbali wa kitaifa wa chama, akiwemo Mwenyekiti wa ACT-Wazalendo Tanzania Bara, Dorothy Semu, wajumbe wa Sekretarieti, viongozi wa ngazi za mikoa, Umoja wa Vijana na Umoja wa Wanawake, pamoja na mawaziri kivuli.
Amesema msafara wa viongozi hao utagawanywa katika makundi mawili yatakayokuwa na jukumu la kutembelea maeneo tofauti ili kufikisha ujumbe wa chama na kuzungumza na wananchi.
Akizungumzia ziara hiyo, mchambuzi wa masuala ya siasa, Tumaini Mnale, amesema changamoto kwa chama hicho ni kuhakikisha mikutano hiyo haibaki kuwa majukwaa ya kutoa matamko ya kisiasa, bali inakuwa sehemu ya kusikiliza wananchi na kujenga hoja zinazotokana na ushahidi.
“Ziara hiyo ni nafasi ya chama kujenga mawasiliano ya moja kwa moja na wananchi nje ya mijadala ya viongozi wa kitaifa. Umuhimu wake hautapimwa kwa idadi ya mikutano itakayofanyika pekee, bali pia uwezo wa viongozi kusikiliza kero za wananchi na kuziunganisha na hoja za kisera zenye majibu yanayoeleweka,” amesema.

