Jumuiya za kiraia zafikia maazimio manane kuimarisha umoja na amani
Dar es Salaam. Jumuiya za kiraia nchini zimefikia maazimio manane yanayolenga kuimarisha umoja na mshikamano wa kitaifa, kudumisha amani, kukabiliana na mmomonyoko wa maadili na kutumia fursa za kiuchumi kujitegemea, huku Serikali ikitakiwa kuendelea kusimamia utangamano wa kidini.
Maazimio hayo yamefikiwa katika mkutano wa siku tatu wa kuadhimisha miaka 70 ya Usajili wa Jumuiya za Kiraia nchini, uliofunguliwa Oktoba 28, 2026 na kuhitimishwa leo Oktoba 30, 2026 jijini Dar es Salaam.
Miongoni mwa maazimio hayo ni jumuiya za kiraia kuendelea kushirikishwa katika jitihada za Serikali za kujenga umoja wa kitaifa na mapambano dhidi ya mmomonyoko wa maadili.
Maazimio mengine ni kutumia rasilimali na fursa zilizopo kuanzisha miradi itakayoongeza ajira na kuimarisha uwezo wa kifedha wa jumuiya hizo, pamoja na kupatiwa elimu endelevu kuhusu utakatishaji wa fedha, ufadhili wa ugaidi na biashara haramu ya silaha za maangamizi.
Aidha, jumuiya hizo zimeitaka Serikali kuendelea kusimamia utangamano na ustahimilivu wa kidini, huku ikisimamia upangaji wa maeneo ya ujenzi wa nyumba za ibada, hususan za Kikristo, katika maeneo ya umma.
Maazimio mengine yanahusu viongozi wa dini kuzungumza na waumini wao kuhusu amani na haki, pamoja na ushauri wa kufanyika kwa mkutano wa jumuiya hizo angalau mara moja kila mwaka.
Akizungumza katika kilele cha maadhimisho hayo, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Ayoub Mohammed Mahmoud, amesema maazimio hayo yanapaswa kuwa msingi wa mabadiliko katika uendeshaji wa jumuiya hizo ili ziweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi zaidi na kuchangia maendeleo ya taifa.
Amesema mafunzo yaliyotolewa katika mkutano huo yamewasaidia washiriki kuelewa historia na majukumu ya Ofisi ya Msajili wa Jumuiya za Kiraia, fursa za uwekezaji na ukuaji wa uchumi, nafasi ya jumuiya katika mapambano dhidi ya utakatishaji wa fedha haramu na ufadhili wa vitendo vya ugaidi, pamoja na umuhimu wa kulinda amani na utulivu.
Naibu waziri huyo amesema elimu hiyo inapaswa kutumika kuimarisha uendeshaji wa jumuiya hizo na kuhakikisha hazitumiki na watu au mataifa yenye nia ya kuvuruga umoja na mshikamano wa Watanzania.
“Niwaombe sana jumuiya zetu hizi, kwa elimu hii mliyopata, muitumie kuhakikisha kwamba watu wa namna hiyo au mataifa ya namna hiyo hayapati fursa kupitia kwenu,” amesema.
Akizungumzia umuhimu wa kulinda amani, Mahmoud amesema Tanzania inapaswa kuendelea kutunza sifa yake ya kuwa kisiwa cha amani, akieleza kuwa changamoto za kiusalama zinazozikabili nchi nyingine zinaonyesha umuhimu wa kulinda hali hiyo.
Ametoa mfano wa ziara yake katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), ambako alikutana na gavana mmoja wa Nyasa aliyemweleza hofu yake kuhusu matukio yaliyotokea Tanzania wakati na baada ya Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, 2025.
Amesema kiongozi huyo alimweleza kuwa Watanzania walikuwa mfano ambao wananchi wa Congo waliutegemea kujifunza kuhusu amani na utulivu.
“Mnafahamu Tanzania ina wakimbizi zaidi ya 89,000 kutoka Congo? Hiyo ni kutokana na machafuko yanayoendelea nchini humo, hivyo jumuiya za kiraia zina wajibu wa kushiriki katika kulinda utulivu na mshikamano wa taifa,” amesema.
Mahmoud pia amezitaka jumuiya hizo kuwasilisha changamoto zake kupitia Ofisi ya Msajili wa Jumuiya za Kiraia, ambayo ndiyo mlezi wake, badala ya kutumia njia zisizo rasmi zinazoweza kusababisha migogoro na kutokuelewana.
Amesema Serikali iko tayari kushirikiana na jumuiya hizo kutafuta ufumbuzi wa changamoto zinazozikabili, huku akisisitiza umuhimu wa kuimarisha maadili katika jamii.
Kwa upande wake, Msajili wa Jumuiya za Kiraia, Emmanuel Kihampa amesema maazimio hayo yamefikiwa baada ya washiriki kujadiliana kuhusu nafasi ya jumuiya hizo katika maendeleo ya taifa na changamoto zinazokabili uendeshaji wake.
Amesema maadhimisho hayo yalilenga kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali na jumuiya za kiraia za kidini na zisizo za kidini, pamoja na kuwajengea viongozi uwezo kuhusu wajibu wao katika jamii.
“Mkutano huo umewezesha kuongezeka kwa uelewa kuhusu sheria na taratibu za uendeshaji wa jumuiya, uwajibikaji na utawala bora, pamoja na kutambua fursa za uwekezaji zinazoweza kuziwezesha jumuiya kujitegemea kifedha,” amesema.
Ameongeza kuwa mkutano huo umeimarisha mawasiliano na kubadilishana uzoefu kati ya Serikali na jumuiya za kiraia, huku washiriki wakipata nafasi ya kueleza changamoto zao na kujadili namna ya kuzitatua.
Awali, Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk Franklin Rweyemamu, aliwashukuru viongozi wa jumuiya za kiraia na wadau kwa kushiriki maadhimisho hayo kuanzia siku ya ufunguzi hadi kilele chake.
Amesema ushiriki wao umeonyesha umuhimu wa ushirikiano kati ya Serikali na jumuiya za kiraia katika kutekeleza majukumu yanayolenga maendeleo ya jamii.

