Wamiliki wa viwanda wapewa siku 14 kurekebisha uchafuzi wa mazingira
3 mins read

Wamiliki wa viwanda wapewa siku 14 kurekebisha uchafuzi wa mazingira

Kibaha. Mstahiki Meya wa Manispaa ya Kibaha, Dk Nicas Mawazo amevipa siku 14 viwanda viwili vilivyopo katika manispaa hiyo kurekebisha changamoto za kimazingira zinazolalamikiwa na wananchi, ikiwemo kutiririsha maji taka katika maeneo ya makazi na uchafuzi wa hewa.

Viwanda vilivyopewa maelekezo hayo ni A-One Production & Bottlers Limited, kilichopo Kata ya Visiga, na China Boda Technical Group Co Ltd, kinachotengeneza betri na kilichopo Kata ya Tangini.

Akizungumza wakati wa ziara ya kukagua viwanda hivyo leo Ijumaa, Oktoba 30, 2026, Dk Mawazo amekielekeza kiwanda cha A-One kuacha mara moja kutiririsha maji taka katika maeneo ya makazi ya watu kutokana na athari zinazoweza kujitokeza kwa afya za binadamu na viumbe hai.

Amesema kiwanda hicho kinapaswa kujenga mfumo sahihi wa kuchakata na kutibu maji taka ndani ya siku 14, huku kikihakikisha kinapata kibali kutoka Bonde la Wami-Ruvu kabla ya kuruhusiwa kutiririsha maji hayo.

Amesisitiza kuwa hata baada ya kupata kibali, maji yanayotolewa ni lazima yawe yametibiwa na kuthibitishwa kuwa hayana madhara kwa wananchi na mazingira yanayozunguka kiwanda hicho.

Mstahiki Meya Wa Manispaa ya Kibaha Mkoa wa Pwani, Dk Nicas Mawazo, akiwa na baadhi ya maafisa wa manispaa hiyo wakati akikagua mazingira ya viwanda. Picha na Sanjito Msafiri

“Wawekezaji tunawataka sana, lakini afya za wananchi ni muhimu zaidi. Ni lazima taratibu za mazingira zifuatwe ili wawekezaji walipe kodi na jamii iwe salama. Ndani ya siku 14 wanapaswa wawe wamefanya marekebisho,” amesema.

Kiwanda cha A-One kinajishughulisha na ununuzi wa chupa za plastiki na kuzichakata ili kupata malighafi inayoweza kutumika kutengeneza bidhaa nyingine za plastiki au kuuzwa kwa viwanda vinavyohitaji malighafi hiyo.

Ofisa Mazingira wa Manispaa ya Kibaha, Byson Mpogoza amesema kiwanda hicho kimekuwa kikipatiwa maelekezo kuhusu utunzaji wa mazingira zaidi ya mara mbili, lakini hakijayatekeleza ipasavyo.

Kutokana na hali hiyo, amesema Meya ameagiza kiandikiwe ilani na kukipa wiki mbili kurekebisha kasoro zilizobainika kabla ya kuchukuliwa hatua zaidi kwa mujibu wa taratibu.

Mstahiki Meya Wa Manispaa ya Kibaha Mkoa wa Pwani, Dk Nicas Mawazo, akiwa na baadhi ya maafisa wa manispaa hiyo wakati akikagua mazingira ya viwanda. Picha na Sanjito Msafiri

Kwa upande wake, Meneja wa kiwanda cha A-One, Kumar Earla amesema wamepokea maelekezo yaliyotolewa na Meya na watafanyia kazi ndani ya muda waliopewa.

Katika ziara hiyo, Dk Mawazo pia alikagua kiwanda cha China Boda Technical Group Co Ltd, kinachotengeneza betri na kilichopo Kata ya Tangini. Kiwanda hicho kimepewa siku 14 kurekebisha changamoto za kimazingira zinazohusiana na moshi na maji taka.

Ofisa mwajiri wa kiwanda hicho, Anna Edward, amesema wamepokea maelekezo ya Meya na watahakikisha wanayatekeleza ndani ya siku 14 walizopewa.

Naye Ofisa Mtendaji wa Kata ya Visiga, Saumu Hassan, amesema wamekuwa wakifanya ukaguzi wa viwanda mbalimbali kwa kushirikiana na maafisa mazingira na kutoa maelekezo kuhusu namna ya kuzingatia taratibu za utunzaji wa mazingira.

Hata hivyo, amesema baadhi ya viwanda vimekuwa havitekelezi maelekezo yanayotolewa, hali inayofanya changamoto hiyo kujirudia na kuhitaji ufuatiliaji wa karibu ili kulinda mazingira na afya za wananchi.

Source link

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *