Wadau watakiwa kuimarisha ushirikiano kuongeza uzalishaji wa chakula
Arusha. Wadau wa sekta ya kilimo nchini wametakiwa kuimarisha ushirikiano kati ya Serikali na sekta binafsi, ili kuongeza uzalishaji wa chakula, kuboresha upatikanaji wa mbegu bora na kuhakikisha wakulima wanapata huduma za ugani zinazowawezesha kukabiliana na changamoto za uzalishaji.
Wito huo umetolewa leo Ijumaa, Oktoba 30, 2026 na viongozi wa taasisi mbalimbali za kilimo katika mkutano uliojadili ubunifu na ushirikiano katika kuimarisha mfumo wa chakula nchini.
Wamesisitiza kuwa usalama wa chakula hauwezi kupatikana kwa kuongeza uzalishaji pekee, bali unahitaji mifumo imara ya pembejeo, teknolojia, elimu, masoko na uhifadhi wa mazao.
Akizungumza katika mkutano huo, Mwakilishi wa Bayer Tanzania na nchi za Kusini mwa Afrika, Mwinyi Sango, alisema kampuni hiyo inaendelea kuwekeza katika utafiti na teknolojia zinazolenga kuwasaidia wakulima kuongeza mavuno na kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Amesema Bayer imewekeza katika uzalishaji wa mbegu bora za mahindi zinazostahimili ukame na magonjwa, huku nyingine zikiwa na uwezo wa kutoa mavuno mengi. Aliongeza kuwa mbegu hizo zinapatikana katika masoko mbalimbali ya Afrika Kusini mwa Jangwa la Sahara, ikiwemo Tanzania.
Sango amesema kampuni hiyo pia inatoa mafunzo ya bure kwa wakulima kuhusu kanuni bora za kilimo baada ya kubaini tofauti kubwa ya uzalishaji kati ya mashamba ya maonesho na mashamba ya wakulima.
“Kupitia mpango wa Better Life Farming, Bayer inashirikiana na wadau mbalimbali kusogeza teknolojia na vifaa vya kilimo karibu na wakulima ili kupunguza gharama za upatikanaji wake,” amesema.
Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Taifa wa Huduma za Ugani wa Kilimo (NAESA), Dk Wilhelm Mafuru, amesema Serikali imeanzisha wakala huo kuimarisha uratibu, usimamizi na uwajibikaji wa maafisa ugani nchini.
Mkaguzi wa mbegu kutoka taasisi ya Tosci Kanda ya Kaskazini, Erick Nangududa, akizungumza kwenye Bohari ya mbegu ya kampuni ya Bayer Tanzania leo ijumaa, Oktoba 30,2026. Picha na Filbert Rweyemamu
Amesema majukumu yake ni kufuatilia utendaji wa maafisa ugani, kuwezesha upatikanaji wa maarifa na huduma wanazohitaji kutekeleza majukumu yao, pamoja na kuweka mfumo wa uwajibikaji kuhakikisha wanatoa huduma zinazotarajiwa na wakulima.
Dk Mafuru ametaja mabadiliko ya tabianchi, wadudu na magonjwa ya mimea, gharama za pembejeo, upotevu wa mazao baada ya kuvuna na changamoto za masoko kuwa miongoni mwa vikwazo vinavyowakabili wakulima.
Amesisitiza umuhimu wa Serikali, sekta binafsi, taasisi za utafiti, wadau wa maendeleo, wakulima na vyombo vya habari kushirikiana ili kuepusha urudufu wa majukumu na kuhakikisha huduma zinawafikia walengwa.
Akizungumzia mchango wa sekta binafsi, Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Wafanyabiashara wa Mbegu Tanzania (TASTA) amesema chama hicho kilianzishwa mwaka 2002 na kampuni 10 za mbegu, lakini sasa sekta hiyo imepanuka na kuwa na kampuni takribani 60 zenye leseni pamoja na mawakala zaidi ya 12,000 wa pembejeo za kilimo.
Amesema TASTA inalenga kuongeza matumizi ya mbegu bora kutoka hekta milioni tatu hadi milioni sita ifikapo mwaka 2030 kupitia uhamasishaji, mashamba ya maonesho na redio za jamii.
Amesisitiza kuwa upatikanaji wa masoko ya uhakika ni muhimu ili kuwahamasisha wakulima kutumia mbegu bora badala ya kupanda mbegu walizovuna wenyewe.
Naye Erick Nangududa kutoka Mamlaka ya Udhibiti wa Ubora wa Mbegu Tanzania (TOSCI) amesema mamlaka hiyo huchunguza sampuli za mbegu maabara ili kuthibitisha ubora na uwezo wake wa kuota kabla ya kupewa lebo maalumu za utambuzi.
Ametoa wito kwa wadau kuhamasisha matumizi ya mbegu zilizothibitishwa, akisema hatua hiyo itasaidia kuongeza mavuno, kupunguza upungufu wa chakula na kuwezesha Tanzania kuwa na ziada ya kuuza nje.
Amesisitiza kuwa usalama wa mbegu ni msingi wa usalama wa chakula na taifa, hivyo wadau wanapaswa kuhakikisha wakulima wanapata mbegu bora kwa wakati na kwa gharama wanazoweza kumudu.

