Mtwara waeleza matumaini ongezeko la gesi asilia
4 mins read

Mtwara waeleza matumaini ongezeko la gesi asilia

Mtwara. Wakati Tanzania ikitangaza kugundua gesi asilia inayokadiria kufikia futi za ujazo bilioni 223, wananchi wa Mtwara wameeleza matumaini yao wakitaka rasilimali hiyo iwanufaishe pia wakazi wa mkoa huo.

Kiwango hicho cha gesi kimegunduliwa katika kitalu cha Mnazi Bay mkoani Mtwara ikiwa ni ugunduzi mpya baada ya miaka 10, hatua itakayoongeza upatikanaji wa nishati hiyo muhimu katika ukuaji wa uchumi. 

Oktoba 27, 2026, Waziri wa Nishati, Dk Juma Homera alisema kiwango hicho kipya cha gesi kiligunduliwa baada ya kuchoronga kisima kiitwacho Kasa-1X ST2, kinachoendeshwa kwa ubia kati ya Shirika la Maendeleo ya Petroli Tanzania (TPDC) na kampuni ya mafuta ya Ufaransa ya Maurel & Prom (M&P).

Ugunduzi huo mpya uliobainika Kusini mwa Tanzania utaongeza kiwango cha hifadhi ya gesi asilia kufikia zaidi ya futi za ujazo trilioni 57.76. Kabla ya ugunduzi huo mpya, Tanzania ilikuwa na hifadhi ya gesi asilia futi za ujazo wa trilioni 57.54.

Wakizungumzia hilo, wananchi wa Mtwara wameeleza matumaini yao kuhusu ugunduzi mpya wa gesi katika eneo la Mnazi Bay, wakisema hatua hiyo ni chachu ya kukuza uchumi wa mkoa huo na kuboresha maisha ya wananchi, endapo fursa zitakazotokana na rasilimali hiyo zitatumika ipasavyo.

Hata hivyo, wamesisitiza kuwa uwepo wa rasilimali hiyo unapaswa kwenda sambamba na kuboreshwa kwa huduma za kijamii, ikiwamo maji, afya, barabara na upatikanaji wa ajira kwa wananchi wa maeneo yanayozunguka miradi ya gesi.

Amina Hamis, mkazi wa Msimbati, amesema ugunduzi huo ni hatua inayoongeza matumaini kwa wananchi wa eneo hilo ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakitarajia kuona rasilimali ya gesi ikichochea maendeleo ya kijamii na kiuchumi.

Amesema pamoja na uwepo wa shughuli za gesi katika eneo hilo, bado wananchi wanahitaji kuona manufaa yake yakigusa maisha yao ya kila siku kupitia huduma bora za kijamii na fursa za kiuchumi.

“Nimefurahishwa na taarifa za ugunduzi wa gesi, lakini tunachotamani ni kuona wananchi wa Msimbati wakinufaika moja kwa moja. Tunahitaji barabara nzuri, maji, ajira na huduma bora za kijamii,” amesema Amina.

Naye, Hafidhi Abdallah, mkazi wa Ruvula, amesema ugunduzi huo ni fursa muhimu kwa Mkoa wa Mtwara, hususan kwa vijana wanaohitaji ajira na nafasi za kujiajiri kupitia shughuli mbalimbali zinazohusiana na sekta ya gesi.

Amesema ni muhimu Serikali na wawekezaji kuweka mikakati ya kuwaandaa vijana kwa kuwapatia mafunzo ya ufundi na ujuzi mbalimbali ili waweze kushiriki kikamilifu katika shughuli za uzalishaji na huduma zinazohusiana na sekta hiyo.

“Tunatarajia ugunduzi huu utaleta ajira kwa vijana wa Mtwara. Ni vizuri vijana wakapewa kipaumbele, lakini pia wapatiwe mafunzo yatakayowawezesha kupata nafasi katika sekta hii,” amesema Hafidhi.

Kwa upande wake, Singizi Juma, mkazi wa Mtwara Mjini, amesema ugunduzi huo ni fursa ya kuimarisha uchumi wa mkoa huo kwa kuvutia wawekezaji, kukuza biashara na kuongeza shughuli za uzalishaji zitakazochangia maendeleo.

Amesema uwepo wa rasilimali hiyo unaweza kuufanya Mkoa wa Mtwara kuwa kitovu muhimu cha shughuli za kiuchumi na uwekezaji, hivyo ni muhimu kuweka mazingira yatakayowawezesha wananchi na wafanyabiashara wa ndani kunufaika.

“Tunatarajia ugunduzi huu utakuwa mwanzo wa mabadiliko makubwa ya kiuchumi kwa Mtwara. Serikali ihakikishe gesi hii haibaki kuwa rasilimali iliyopo hapa, bali manufaa yake yaonekane katika maisha ya wananchi,” amesema Singizi.

Mtalaamu wa masuala ya uchumi kutoka Chuo Kikuu cha Kilimo cha Sokoine (SUA), Dk Charles Malaki amesema anaiona Tanzania ikipigia hatua kuwa mzalishaji na muuzaji mkubwa wa gesi ndani na nje ya nchi, endapo kiwanda cha kusindika nishati hiyo kitajengwa.

“Tanzania itaendelea kukua kiuchumi, na kuwa muuzaji mkubwa nje ya nchi. Kile kiwanda cha Madimba kikiongezewa uwekezaji na kwa miji mikubwa ya Dar es Salaam, Dodoma na Arusha kunatakiwa kuwe na mifumo inayoletewa matenki ya gesi na kuisambaza,” amesema Malaki.

Mbali na hilo, uwepo wa gesi hiyo utaendelea kuipa sifa Tanzania katika sekta ya utunzaji wa mazingira hasa kwa wananchi wa vijijini watakaondokana na matumizi ya kuni na kuhamia katika nishati safi ya kupikia.

Source link

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *