Wanafunzi wanane MUST mbaroni kwa tuhuma za udanganyifu wa mitihani
Mbeya. Wanafunzi wanane wa Chuo Kikuu cha Sayansi na Teknolojia Mbeya (MUST) wanashikiliwa na Jeshi la Polisi mkoani humo kwa tuhuma za udanganyifu wa mitihani kwa kuingia darasani na kuwafanyia wenzao.
Watuhumiwa hao walikamatwa Oktoba 27, 2026 wakiwa katika Chuo cha Ufundi Moravian kilichopo Mtaa wa Kadege jijini humo baada ya msimamizi mkuu wa mitihani kituo hicho kuwabaini kupitia mfumo wa picha zilizotumika.
Akizungumza leo Oktoba 30, 2026, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Benjamin Kuzaga amesema baada ya uhakiki katika mfumo, ilibainika kuwa picha zilizotumika kubandika kwenye barua ni tofauti na zinazoonekana katika mfumo.
Amesema imebainika kuwa watuhumiwa hao walilipwa Sh100,000 kila mmoja kufanya mitihani, huku akiwataja watuhumiwa hao kuwa ni Rashid Mkwandam aliyemfanyia mtihani Shazir Bakari na Danie Zakaria aliyemfanyia mtihani Erasto Ng’holo.
“Wengine ni Rhino Bikura aliyemfanyia Nehemiah Tukonge, Jilala Mathias aliyemfanyia Felix Shibanda, Isac Kasiri aliyemfanyia Jeremia Sanga, Andrew Ngewe aliyemfanyia Benard Mgala, Marine Chembea aliyemfanyia Hamis Mwenga na James Masanja aliyemfanyia Leonard Mgala.
“Mkuu wa kituo cha mitihani alibaini wanafunzi hao wameingia chumba cha mitihani kwa lengo la kuwafanyia wenzao kwani baada ya uhakiki katika mfumo ilibainika picha zilizotumika kubandika kwenye barua ni tofauti na zinazoonekana katika mfumo,”amesema Kuzaga.
Katika tukio jingine, jeshi hilo linamshikilia Alphonce Isaya (29) mkazi wa Ilomba jijini humo kwa tuhuma za kumbaka mtoto wa kike (15) ambaye ni mwanafunzi wa kidato cha pili.
Kuzaga amesema tukio hilo lilitokea Oktoba 28, 2026 baada ya mtuhumiwa kumlaghai mtoto huyo kuwa anahitaji huduma dukani na alipoingia ndani alifunga mlango na kumbaka.
“Chanzo cha tukio hili ni tamaa za kimwili na upelelezi unaendelea ili mtuhumiwa afikishwe mahakamani kwa hatua zaidi za kisheria,” amesema kamanda huyo.
Katika hatua nyingine, Kuzaga ameongeza kuwa wakati ikielekea mwishoni mwa kampeni za usalimishaji silaha haramu kwa hiari, silaha mbili aina ya gobole na risasi 23 zimesalimishwa.
“Silaha hizo zilikutwa zimesilimishwa katika eneo la Sabasaba pembezoni mwa barabara, huku risasi 23 zikisalimishwa wakati wa mkutano wa hadhara wilayani Kyela kupitia kampeni ya ‘Ongea na Kamanda,” amesema Kuzaga.
Kamanda huyo amewataka baadhi ya wananchi wenye tabia za uhalifu kuacha mara moja kwani Jeshi hilo halitasita kumkamata na kumchukulia sheria yeyote kwa mujibu wa sheria.

