Dhamira ya CRDB kuifikisha Tanzania uchumi wa Dola 1 trilioni kupitia kilimo, uvuvi na mifugo
8 mins read

Dhamira ya CRDB kuifikisha Tanzania uchumi wa Dola 1 trilioni kupitia kilimo, uvuvi na mifugo

Kwenye udongo mwekundu unaotimua vumbi asubuhi katika Nyanda za Juu Kusini na kwenye mawimbi yanayopiga fukwe za Bahari ya Hindi kuanzia Tanga hadi Mtwara, kuna sauti mpya inayosikika huku ikitoa mutumaini ya kesho iliyobora.

Tofauti na zamani sauti ya sasa si sauti ya simanzi ya mkulima aliyetawaliwa na hofu ya mvua, wala si kilio cha mvuvi anayerudi mikono mitupu baharini. Ni mdundo wa mashine za kisasa, kishindo cha matrekta na kicheko cha uzalishaji unaobadilisha maisha ya mamilioni ya Watanzania.

Kwa miaka mingi, kuta za mabenki zilionekana kuwa ndefu na zenye baridi kali kwa mzalishaji wa vijijini; kauli ya, kilimo hakibenkinki, ilitawala kama wimbo wa kukatisha tamaa kwenye masoko na mikutano ya kifedha.

Wakulima, wafugaji na wavuvi walionekana kama wawekezaji wa bahati nasibu wanaotawaliwa na utegemezi wa kujikimu.

Hata hivyo, ukitembelea makao makuu ya Benki ya CRDB na kukutana na Mkuu wa Kitengo cha Kilimo Biashara Benki ya CRDB, Maregesi Shaabani unabaini kuwa changamoto hiyo imekuwa historia.

Benki ya CRDB haikitazami kilimo kama sekta ya kuisaidia kwa hisani, bali kama mgodi wa dhahabu ya kijani unaosubiri sayansi, bima, teknolojia na mtaji ili kulipua uwezo wake wote.

Hivi sasa, huku ikishikilia asilimia 45 ya soko lote la mikopo ya kilimo nchini na kuwekeza Sh4.3 trilioni kwa mwaka huu pekee, CRDB haitoi tu fedha bali inaweka historia mpya na kuleta tabasamu kwenye maisha ya wakulima, wafugaji, wavuvi na Taifa kwa jumla.

Hii ni safari ya kimapinduzi inayolenga kubadilisha jembe la mkono kuwa teknolojia ya kisasa na mtumbwi wa kupiga makasia kuwa mradi wa vizimba vya samaki katikati ya Ziwa Victoria, ikitengeneza barabara kuu kuelekea Dira ya Taifa ya Maendeleo ya mwaka 2050.

Mkakati wa kuhakikisha kilimo kinabenkika

Shaabani anafafanua kuwa mtazamo wa kwamba kilimo hakibenkiki unatokana na mchakato wa mpito ambao nchi inapitia.

Kwa miaka mingi, Watanzania wengi wamekuwa wakijihusisha na kilimo, uvuvi na ufugaji wa kujikimu.

Jukumu la CRDB limekuwa ni kubadilisha mtazamo huo ili kuwavusha wazalishaji kutoka kwenye kilimo cha kujikimu kuingia kwenye uwekezaji himilivu wa kibiashara.

Sababu kubwa inayofanya taasisi nyingi za fedha kusita kuwekeza kwenye kilimo ni uwepo wa viashiria vya hatari nyingi (risks) ikiwamo, gharama na thamani ndogo ya dhamana za vijijini kwani sehemu kubwa ya kilimo iko vijijini ambako thamani ya ardhi na nyumba za wakulima iko chini pindi inapotathminiwa ukilinganisha na mali zilizopo maeneo ya mijini, hata kama mradi wenyewe ni mzuri na unahitaji mtaji mkubwa.

Kukosekana kwa kumbukumbu na rekodi za kifedha nayo ni changamoto, hii ni kutokana kuwa, wakulima wengi hawatunzi kumbukumbu za mauzo, mavuno na matumizi, jambo linalofanya uandaaji wa maandiko ya miradi kuwa mgumu.

Ukosefu wa mpango wa urithi

 Hii ni kwa sababu biashara nyingi za kilimo ni za kifamilia hivyo bila usimamizi endelevu, baba au mama anapougua au kufariki, biashara hufa.

Athari za mabadiliko ya tabianchi kama vile mvua zisizotabirika, ukame au mafuriko hufanya kilimo kuonekana kama mchezo wa bahati nasibu.

Ili kukabili changamoto hizi, CRDB imeweka mikakati thabiti kwa kutoa mafunzo ya usimamizi wa biashara na kuweka misingi ya mipango ya urithi. Katika suala la dhamana, benki inatumia dhamana mbadala ili kuongezea thamani ya mtaji unaohitajika.

Kwenye upande wa mabadiliko ya tabianchi, benki hiyo inatumia kampuni yake tanzu ya bima ya CRDB Insurance Company (CIC) pamoja na kitengo cha CRDB Bank Assurance ili kukinga miradi ya wakulima dhidi ya majanga.

Zaidi ya hapo, benki inatoa bima maalumu ya ‘Keyman Insurance Cover’ ambayo inamlinda mwekezaji, anapougua au kufariki, bima hiyo inalipa deni la benki bila kufilisi mali za familia au mradi.

Ufumbuzi wa changamoto ya masoko

Kilio kikubwa cha mkulima wa kitanzania mara zote kimekuwa ni ukosefu wa soko la uhakika baada ya kuvuna.

Shaabani anasema CRDB imetatua mtihani huo kupitia mfumo wa Mkataba wa Pande Tatu (tripartite agreement) unaosainiwa kati ya mkopaji/mzalishaji (mkulima, mvuvi au mfugaji), benki, na mnunuzi.

“Kupitia mkataba huu, mnunuzi anaahidi kuchukua mazao yote yatakayozalishwa, huku malipo yote yakipitishwa moja kwa moja kwenye akaunti ya mteja iliyopo Benki ya CRDB,” anasema Shaabani.

Mfumo huu unakinga mtiririko wa fedha, unampa mkulima uhakika wa soko, unaiondoa benki kwenye hofu ya urejeshaji wa mkopo na pia unatumika kama sehemu ya dhamana ya mkopo huo.

Tanzania imejaliwa rasilimali nyingi ambazo bado hazijatumiwa kikamilifu ikiwamo ardhi kwani nchi ina eneo la kilomita za mraba 945,000, zaidi ya asilimia 80 inafaa kwa kilimo cha mazao ya kimkakati.

Rasilimali za maji na uchumi wa bluu. Pwani ya Bahari ya Hindi yenye urefu wa kilomita 1,400 (kutoka Tanga hadi Mtwara), eneo la uvuvi la Bahari ya Hindi lisilopungua kilomita za mraba 223,000, maziwa, mito pamoja na vijito vyenye ujazo wa kutosha.

Kwa upande wa sekta ya mifugo; Tanzania ni nchi ya pili barani Afrika kwa kuwa na idadi kubwa ya wanyama ikiongozwa na Ethiopia pekee.

Hivi sasa, asilimia 65 ya Watanzania wameajiriwa moja kwa moja kwenye sekta ya kilimo

Hata hivyo, mchango wa kilimo kwenye Pato la Taifa bado uko chini ya asilimia 30 (ukicheza kati ya asilimia 26 na 29).

Shaabani anasisitiza kuwa, ili kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya 2050 ya kujenga uchumi wa Dola 1 trilioni, mchango wa kilimo kwenye Pato la Taifa lazima upande na kufikia angalau asilimia 50.

Pembejeo za kidijitali, viwanda na teknolojia

CRDB imeweka nguvu kubwa katika kuhakikisha kuwa sekta zote za mnyororo wa thamani zinanufaika kwa kuweka mifumo na zana za kuchechemua mnyororo huo ikiwemo:

Mfumo wa kidijitali wa mbolea na pembejeo; kwa kushirikiana na Wizara ya Kilimo na Mamlaka ya Usimamizi wa Mbolea Nchini (TFRA), benki hiyo imetengeneza mfumo wa kidijitali (digital supply chain) unaomsajili kila mkulima, eneo lake, ukubwa wa shamba, aina ya mazao na mahitaji halisi ya mbolea. Mfumo huo umeipa nchi takwimu sahihi zilizosaidia kuagiza na kusambaza mbolea kwa wakati.

Zana za kisasa za kilimo; benki inawasaidia wakulima kupata matrekta, zana za kupandia za kuvunia na mitambo ya umwagiliaji. Benki imeingia makubaliano na wauzaji wa mashine, mteja anachangia asilimia 20 na benki inakopesha asilimia 80.

Dhamana inakuwa ni trekta lenyewe. Mfumo huu umeweka nidhamu ya hali ya juu na kuzuia mikopo chechefu.

Kuchochea uchumi wa viwanda; zaidi ya asilimia 80 ya viwanda vya Tanzania vinategemea mali ghafi kutoka shambani, kwenye mifugoni na uvuvi.

CRDB inawezesha viwanda vya kukoboa kahawa, viwanda vya sukari (ikituunganisha wawekezaji wakubwa na wakulima wadogo wa miwa (outgrowers), pamoja na viwanda vya kubangua korosho.

Pia, benki imepata ithibati kutoka Mfuko wa Umoja wa Mataifa wa Mabadiliko ya Tabianchi (Green Climate Fund) na kupata ufadhili wa zaidi ya Dola 200 milioni kuwezesha kilimo himilivu cha mazao ya chakula.

Ufugaji wa kisasa na uchumi wa bluu

Kwa sasa CRDB inawezesha miradi ya unenepeshaji mifugo na kuiuzia viwanda vya nyama.

Kwenye maziwa, imezindua mpango wa Kopa Ng’ombe Lipa Maziwa,  anakopeshwa ng’ombe mwenye mimba, anazaa ndani ya miezi 3-4, na maziwa yanayokwenda kiwandani yanatumika kulipa mkopo kupitia mkataba wa pande tatu.

CRDB inashirikiana na Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar (SMZ) kupitia programu ya Inuka na Uchumi wa Bluu, ikilenga kuwafikia wavuvi 50,000 na kaya kati ya 300,000 hadi 400,000 ndani ya miaka mitatu kwa kuwapa maboti ya kisasa na vifaa vya uvuvi.

Uvuvi wa kisasa bara na vizimba

Benki inatoa mitambo ya kubaini samaki walipo  na kufadhili uwekezaji wa vizimba katika Ziwa Victoria (kuanzia vizimba 3-5 kwa wakulima wadogo hadi vizimba 1,000-2,000 kwa wawekezaji wakubwa).

“Tumewawezesha wazawa kujenga viwanda vya chakula cha samaki nchini ili kuondoa utegemezi wa kuagiza chakula kutoka Brazil, Vietnam na Kenya. Katika Ziwa Tanganyika, tukishirikiana na FAO kupitia programu ya FISH4ACP, CRDB tumewawezesha wavuvi wadogo kutumia majiko sanifu na mahema ya jua ya kukaushia samaki,” anasema Shaabani. 

Source link

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *