Mchakato kumpata Mkurugenzi Mkuu WHO waanza, saba wakitajwa
2 mins read

Mchakato kumpata Mkurugenzi Mkuu WHO waanza, saba wakitajwa

Dar es Salaam. Shirika la Afya Duniani (WHO) limetangaza wagombea saba wanaowania nafasi ya Mkurugenzi Mkuu, huku mchakato wa kumpata kiongozi mpya wa taasisi hiyo ukitarajiwa kukamilika Mei 2027.

Wagombea hao wamependekezwa na nchi wanachama na wanatarajiwa kushindania nafasi hiyo yenye dhamana ya kuongoza juhudi za kimataifa katika kulinda na kuboresha afya za watu duniani.

Kwa mujibu wa taarifa ya WHO iliyotolewa leo Ijumaa Oktoba 30, 2026, wagombea hao ni Dk Hanan Mohammed Al-Kuwari, Dk Hanan Balkhy, Dk Hans Henri P Kluge, Dk MarĂ­a P Neira, Budi Gunadi Sadikin, Dk Li Song na Dk Gevorg Tamamyan.

Dk Gevorg Tamamyan ni mgombea pekee kutoka Bara la Afrika aliyependekezwa akitokea Botswana, lakini uraia wake ni wa Armenia.

WHO imesema wagombea hao watakutana na nchi wanachama na wanachama washirika Novemba 18 na 19, mwaka huu, katika makao makuu ya shirika hilo mjini Geneva, Uswisi.

Mkutano huo utakaokuwa wa kwanza wa wagombea utatangazwa mubashara kupitia tovuti ya WHO kwa lugha sita rasmi, ambazo ni Kiarabu, Kichina, Kiingereza, Kifaransa, Kirusi na Kihispania.

Katika hatua inayofuata, Bodi ya Utendaji ya WHO, yenye wajumbe 34, itakutana mapema mwaka 2027 na kuchagua wagombea watano kati ya saba.

Wagombea hao watano watafanyiwa mahojiano na wajumbe wa Bodi hiyo, kabla ya kupendekeza hadi majina matatu yatakayowasilishwa kwa Baraza la Afya Duniani.

WHO pia imepanga kufanya jukwaa la pili la wagombea Machi 15, 2027, kwa wale watakaopitishwa na Bodi ya Utendaji.

Uamuzi wa mwisho utafanywa katika Mkutano wa 80 wa Baraza la Afya Duniani utakaofanyika Mei 2027.

Baraza hilo ndilo chombo kikuu cha maamuzi cha WHO, chenye jukumu la kuamua sera za shirika, kusimamia masuala ya fedha na kumteua Mkurugenzi Mkuu.

Mkurugenzi Mkuu atakayechaguliwa anatarajiwa kuanza rasmi kazi Agosti 16, 2027.

Atakuwa na jukumu la kuongoza mikakati ya WHO katika kukabiliana na magonjwa, kuimarisha mifumo ya afya na kuratibu ushirikiano wa kimataifa katika kuboresha huduma za afya.

Dk Tedros Ghebreyesus raia wa Ethiopia amekuwa Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Afya Duniani (WHO) tangu Julai 1, 2017, akiongoza kwa mihula miwili ya miaka mitano.

Muhula wake wa kwanza ulianza mwaka 2017 hadi 2022, kabla ya kuchaguliwa tena kwa muhula wa pili unaotarajiwa kumalizika Agosti 15, 2027. Hivyo, atakuwa ameiongoza WHO kwa jumla ya miaka 10 kabla ya kukabidhi madaraka kwa mrithi wake Agosti 16, 2027.

Source link

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *