EU yaahidi kushirikiana na Tanzania kutatua changamoto za wananchi
4 mins read

EU yaahidi kushirikiana na Tanzania kutatua changamoto za wananchi

Mwanza. Umoja wa Ulaya (EU) umesema utaendelea kushirikiana na Serikali ya Tanzania kutatua changamoto za wananchi kupitia uwekezaji katika huduma za maji, usafi wa mazingira, maendeleo endelevu ya miji na kukuza fursa za kiuchumi.

Akizungumza jijini Mwanza leo Ijumaa, Oktoba 30, 2026, Balozi wa Umoja wa Ulaya nchini Tanzania, Jean-Marc Pisani amesema ushirikiano kati ya pande hizo unalenga kuunganisha uwekezaji na utaalamu wa Ulaya na vipaumbele vya Tanzania ili kuleta suluhisho la changamoto zinazowakabili wananchi.

“Ushirikiano wetu na Tanzania umejengwa katika maslahi ya pamoja na manufaa kwa pande zote. Kupitia mpango wa Global Gateway, tunaunganisha uwekezaji na utaalamu wa Ulaya na vipaumbele vya Tanzania ili kuleta suluhisho la vitendo, kutengeneza fursa za kiuchumi na kusaidia ukuaji endelevu unaozinufaisha Tanzania na Ulaya,” amesema Pisani.

Amesema hayo wakati wa ziara ya kikazi jijini Mwanza akiwa ameambatana na Balozi wa Ufaransa nchini Tanzania, Jean Baptiste Jeangene pamoja na washirika wengine wa timu Europe ambapo walitembelea miradi inayotekelezwa kwa ushirikiano wa Umoja wa Ulaya, Serikali ya Tanzania na washirika wa maendeleo.

Balozi wa Umoja wa Ulaya nchini Tanzania, Jean-Marc Pisani (wa kwanza kushoto) akipata maelezo kuhusu uendeshaji na upanuzi wa chanzo cha maji cha Butimba jijini Mwanza wakati wa ziara yake ya kutembelea mradi huo. Picha na Saada Amir     

Katika ziara hiyo, Pisani ametembelea mtambo wa kutibu maji wa Butimba na kueleza kuwa mradi huo ni sehemu ya uwekezaji wa Global Gateway unaotekelezwa kwa awamu tatu, ukitumia teknolojia ya Ulaya na ushirikiano wa nchi wanachama wa Umoja wa Ulaya.

Amesema kwa sasa mtambo huo unanufaisha takribani watu 300,000 huku mpango wa upanuzi wake ukilenga kuongeza idadi ya wanufaika hadi kufikia watu 800,000.

“Nilipata fursa ya kutembelea mtambo huu wa maji na kusikiliza maelezo ya wahandisi kuhusu malengo na mipango ya mradi, ikiwemo matumizi ya teknolojia iliyotolewa na kampuni za Ulaya. Mradi huu unaendelea vizuri na tunatarajia kwamba utakapopanuliwa utaweza kuwahudumia watu wengi zaidi, hadi kufikia takribani 800,000,” amesema.

Amesema utekelezaji wa miradi hiyo unahusisha Umoja wa Ulaya kwa kushirikiana na nchi wanachama wake, ikiwemo Ufaransa, Ubelgiji na Ujerumani, pamoja na Benki ya Uwekezaji ya Ulaya (EIB), chini ya mfumo wa Team Europe.

Amesema ushirikiano huo unalenga kuhakikisha uwekezaji unaofanyika unaleta mabadiliko katika maisha ya wananchi, hususan kwa kuongeza upatikanaji wa maji safi na salama na kuboresha huduma za msingi.

Mbali na miradi ya maji, Pisani amesema mpango wa Green and Smart Cities SASA ni sehemu nyingine ya uwekezaji wa Global Gateway unaotekelezwa Mwanza, Tanga na Pemba, wenye thamani ya Euro milioni 75, sawa na Sh224.72 bilioni.

Amesema mpango huo una maeneo manne ya utekelezaji, yakiwemo kuboresha huduma za maji, kuwezesha mamlaka za Serikali za mitaa kutumia mifumo ya kidijitali katika kupanga na kusimamia miji, kuimarisha shughuli za maendeleo ya uchumi wa maeneo husika na kujenga ujuzi kwa wananchi.

Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mwanza (Mwauwasa), Leonard Msenyele, akitoa maelezo kwa ujumbe wa EU kuhusu hali ya upatikanaji wa huduma ya maji jijini Mwanza na jitihada za mamlaka hiyo kukabiliana na ongezeko la mahitaji ya maji. Picha na Saada Amir

Akitoa taarifa kwa kuhusu utekelezaji wa miradi ya maji, Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Majisafi na Usafi wa Mazingira Mwanza (Mwauwasa), Leonard Msenyele amesema ongezeko la watu na kupanuka kwa jiji kumeongeza mahitaji ya maji, hivyo kuweka shinikizo katika huduma hiyo.

Amesema kwa sasa mahitaji ya maji jijini Mwanza ni takribani lita milioni 293 kwa siku, wakati uzalishaji ni takribani lita milioni 155 kwa siku.

“Mahitaji ya maji jijini Mwanza ni takribani lita milioni 293 kwa siku, lakini kwa sasa tunazalisha takribani lita milioni 155 kwa siku. Ongezeko la watu linaongeza mahitaji ya maji, lakini miradi inayoendelea kutekelezwa itasaidia kupunguza changamoto hiyo,” amesema Msenyele.

Amesema upanuzi wa mtambo wa Butimba unatarajiwa kuongeza uzalishaji wa maji kutoka lita milioni 48 hadi lita milioni 170 kwa siku, hatua itakayosaidia kuongeza upatikanaji wa maji katika maeneo ya Nyamongolo, Kisesa na Usagara.

Ameongeza kuwa uwekezaji unaofuata utahusisha pia miundombinu ya kusafirisha na kusambaza maji, uunganishaji wa wateja na huduma za majitaka.

Amesema mikataba ya ufadhili wa miradi hiyo imesainiwa na utekelezaji wake unatarajiwa kusaidia kupunguza changamoto ya mgao wa maji jijini Mwanza.

Source link

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *