Sh70 milioni kuinua wakulima wa mwani Mtwara
3 mins read

Sh70 milioni kuinua wakulima wa mwani Mtwara

Mtwara. Wakulima wa mwani katika Kata ya Msangamkuu, Halmashauri ya Wilaya ya Mtwara mkoani Mtwara, wamenufaika na mikopo ya zaidi ya Sh70 milioni inayolenga kuboresha kilimo hicho, kuongeza uzalishaji na kuimarisha kipato chao.

Mikopo hiyo iliyotolewa kupitia asilimia 10 ya mapato ya ndani ya halmashauri katika mwaka wa fedha 2025/2026, imewezesha vikundi mbalimbali vya wajasiriamali kuongeza mitaji na kununua vifaa vinavyorahisisha shughuli za kilimo na kuongeza thamani ya zao la mwani.

Miongoni mwa vikundi vilivyonufaika ni Tujikombowe, Mzalendo na Ukakamavu, ambavyo vimeeleza kuwa fedha hizo zimekuwa chachu ya kuboresha shughuli zao na kuongeza uwezo wa uzalishaji.

Akizungumzia manufaa ya mkopo huo, Amina Mmanga, mwanachama wa Kikundi cha Tujikombowe, amesema wamepanua mashamba yao na kununua vifaa vya kisasa, ikiwemo boti zinazorahisisha usafiri kwenda kwenye mashamba ya mwani wakati wa uvunaji.

“Mkopo huu unatunufaisha sana sisi wakulima wa mwani kwa sababu tumeweza kuongeza mashamba na kununua vifaa vya kisasa, kama vile boti zinazoturahisishia kufika kwenye mashamba yetu kwa ajili ya kuvuna mwani, kwa kuwa yapo mbali,” amesema Amina.

Amesema mbali na kununua vifaa hivyo, wamefanikiwa pia kutengeneza chanja za kukaushia mwani, ili kuhakikisha zao hilo linakaushwa katika mazingira yanayodumisha usafi na ubora wake.

Amina ameishukuru Serikali kwa kuendelea kuwawezesha wakulima kupitia mikopo hiyo, akieleza kuwa msaada huo umewapa nafasi ya kuboresha shughuli zao na kuimarisha hali zao za kiuchumi.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kikundi cha Mzalendo, Saidi Hamisi, amesema wanachama wote saba wa kikundi hicho wamenufaika na mkopo huo, ambao umewawezesha kununua vifaa mbalimbali, vikiwemo kamba na turubai kwa ajili ya kuendeleza shughuli zao za kilimo cha mwani.

Ameushukuru uongozi wa kata na halmashauri kwa kuwezesha upatikanaji wa mikopo hiyo, akisema imewasaidia kuongeza uwezo wa kuendesha shughuli zao.

“Wanachama wote saba wa kikundi chetu wamenufaika na mkopo huo, ambao umetuwezesha kununua vifaa mbalimbali ikiwemo kamba na turubai kwa ajili ya kuboresha shughuli zetu za kilimo cha mwani,” amesema Saidi Hamisi, mwenyekiti wa Kikundi cha Mzalendo.

Akizungumzia utekelezaji wa mpango huo katika kata hiyo, Ofisa Mtendaji wa Kata ya Msangamkuu, Belinda Mpina amesema vikundi 15 vilinufaika na mikopo yenye thamani ya zaidi ya Sh70 milioni katika mwaka wa fedha 2025/2026.

Amesema wanufaika wengi ni wakulima wa mwani na wavuvi, huku mikopo hiyo ikitumika kwa shughuli mbalimbali, ikiwemo ununuzi wa boti, mashine za kusagia mwani na vifaa vya kuongeza thamani ya zao hilo.

“Kikundi kimoja kimepata mkopo kwa ajili ya kununua boti, huku vingine vikinunua mashine za kusagia mwani. Vikundi vingi vimepata mikopo kwa ajili ya kuongeza thamani ya zao la mwani,” amesema Belinda.

Ameongeza kuwa katika mwaka wa fedha 2026/2027, halmashauri inaendelea na mchakato wa kuwezesha vikundi vingine kupata mikopo hiyo ili kuongeza wigo wa wanufaika.

Belinda amesema halmashauri itaendelea kutoa elimu kwa vikundi na kusimamia urejeshaji wa mikopo kwa wakati ili fedha hizo ziweze kunufaisha vikundi vingine na kuendeleza shughuli za kiuchumi katika jamii.

Source link

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *