TBL, Veta kufadhili mafunzo ya vijana 300
3 mins read

TBL, Veta kufadhili mafunzo ya vijana 300

Dar es Salaam. Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) kwa kushirikiana na Mamlaka ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi Stadi (VETA), imeanzisha mpango wa ufadhili wa mafunzo ya ufundi stadi katika sekta ya kilimo utakaowanufaisha vijana 300 kutoka familia zenye kipato cha chini.

Mpango huo unaojulikana kama Ujuzi-Kwanza, utatekelezwa kwa miaka mitatu ukiwa na lengo la kuwajengea vijana uwezo wa kujiajiri, kuajiriwa na kuanzisha shughuli za kiuchumi zinazohusiana na kilimo.

Ushirikiano huo umewekwa rasmi kupitia Hati ya Makubaliano iliyosainiwa na Mkurugenzi Mtendaji wa TBL, Michelle Kilpin na Mkurugenzi Mkuu wa Veta, Anthony Kasore.

Kupitia makubaliano hayo, TBL itagharamia mafunzo, huku Veta ikitoa mafunzo yaliyoidhinishwa na utaalamu wa kiufundi unaotambulika kitaifa.

Mafunzo hayo yatajumuisha uzalishaji wa mazao, matengenezo ya vifaa, ufundi wa mitambo ya kilimo na stadi nyingine zinazohitajika katika sekta hiyo. Vijana pia watapata mafunzo kwa vitendo kupitia shughuli za kilimo, ikiwamo kushiriki katika jamii za wakulima wa shayiri na mtama wanaoshirikiana na TBL.

Akizungumza katika hafla ya utiaji saini leo Ijumaa Oktoba 30, 2026, Kasore amesema mpango huo utasaidia kuziba pengo la ujuzi katika sekta ya kilimo inayobadilika kutokana na matumizi ya teknolojia na mbinu za kisasa za uzalishaji.

Wadau kutoka nchi nne zinazopakana na Ziwa Tanganyika, ambazo ni Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Tanzania na Zambia, wakifuatilia Mkutano wa 14 wa Kawaida wa Baraza la Mawaziri la Mamlaka ya Ziwa Tanganyika (LTA), unaofanyika jijini Dar es Salaam, Oktoba 30, 2026, kujadili ushirikiano wa kikanda na usimamizi endelevu wa rasilimali za ziwa hilo. Picha na Said Powa

Amesema ushirikiano huo utafungua fursa kwa vijana wasiokuwa na uwezo wa kugharamia mafunzo, huku ukiwapatia ujuzi unaoendana na mahitaji ya soko la ajira.

“Kadiri sekta yetu ya kilimo inavyoendelea kuwa ya kisasa, tunahitaji vijana wenye ujuzi ambao wanaweza kusaidia uzalishaji, kuboresha mbinu za kilimo, kutunza na kukarabati vifaa pamoja na kutoa huduma muhimu za kiufundi,” amesema.

Kwa upande wake, Kilpin amesema uwekezaji huo ni sehemu ya dhamira ya kampuni hiyo ya kuimarisha ushirikiano na wakulima wa ndani na kukuza mnyororo wa thamani wa kilimo nchini.

Amesema shughuli za TBL zinategemea kwa kiasi kikubwa mazao yanayozalishwa na wakulima wa Tanzania, hivyo kuwawezesha vijana kupata ujuzi kutachangia maendeleo ya wakulima na kampuni.

Takwimu za mpango huo zinaonyesha kilimo kilichangia asilimia 26.3 ya Pato la Taifa mwaka 2024 na kuendelea kuajiri zaidi ya nusu ya watu wanaofanya kazi nchini.

Wakati huohuo, Kamati ya Bajeti ya Bunge imeeleza kuwa zaidi ya vijana 800,000 huingia katika soko la ajira kila mwaka. Utafiti wa ufuatiliaji wa wahitimu wa Veta umebaini kuwa asilimia 75 walikuwa wameajiriwa au kujiajiri.

Kwa sasa, TBL hununua shayiri na mtama kutoka kwa wakulima wadogo zaidi ya 2,500 katika mikoa ya Arusha, Kilimanjaro, Manyara na Dodoma.

Kilpin amesema mafanikio ya mpango huo hayatapimwa kwa idadi ya vijana waliofunzwa pekee, bali pia uwezo wao wa kutumia ujuzi kujenga taaluma, kuanzisha biashara na kuboresha maisha yao.

Source link

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *