Uwajibikaji watajwa kuwa nguzo ya mafanikio ya Bandarini Saccos
Dar es Salaam. Uwajibikaji na uwazi katika uongozi vimetajwa kuwa msingi wa mafanikio na ukuaji wa Chama cha Ushirika wa Akiba na Mikopo cha Bandarini Saccos Limited, huku Bodi ya Uongozi ikiweka wazi mafanikio yaliyopatikana, changamoto zilizopo na mikakati ya kuimarisha chama hicho kuelekea mwaka 2027.
Akizungumza katika Mkutano Mkuu wa 58 wa Bandarini Saccos Limited uliofanyika leo Jumamosi Oktoba 31, 2026 na kuhudhuriwa na wadau mbalimbali wa vyama vya ushirika huku mgeni rasmi akiwa Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Albert Chalamila, Mwenyekiti wa Bodi ya Uongozi aliyemaliza muda wake, Ernest Nyambo amesema ni muhimu wanachama kufahamu hali halisi ya chama, hatua zilizofikiwa na mipango iliyowekwa kwa ajili ya maendeleo endelevu ya taasisi hiyo.
Amesema katika kipindi cha uongozi wake chama kimepiga hatua kubwa kiuchumi huku thamani ya mali ikiongezeka kutoka Sh31.35 bilioni mwaka 2025 hadi Sh37.18 bilioni Septemba 2026.
Pia, amesema kwa kipindi hicho idadi ya wanachama imeongezeka kutoka 2,078 hadi 2,569, hatua inayoashiria kuimarika kwa imani ya wanachama na uwezo wa chama kukua.
Hata hivyo, Nyambo amebainisha changamoto zinazohitaji kupewa kipaumbele, zikiwamo za ukomo wa muda wa mikopo, kushuka kwa uwiano wa mitaji na changamoto za wanachama wanaohama taasisi za ajira.
Amesema bodi na menejimenti zimeandaa mikakati ya kukabiliana na hali hiyo, ikiwamo kuomba kuongeza muda wa mikopo hadi miaka saba, kuimarisha uchangiaji wa hisa na kutumia mifumo ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) ili kurahisisha ukusanyaji wa michango ya wanachama.
“Uaminifu na uwazi ndiyo nguzo iliyotufikisha hapa. Ni wajibu wangu kuainisha changamoto zilizopo na kueleza mikakati thabiti ambayo bodi na menejimenti imeiandaa,” amesema Nyambo.
Amesema mafanikio hayo yamechangiwa pia na mageuzi ya kidijitali kupitia mfumo wa Bandarini Kiganjani, ambao umewezesha kuratibu miamala yenye thamani ya Sh3.1 bilioni na kuiingizia chama mapato ya Sh18.8 milioni.
Pia, amesema chama kimeendelea kupanua wigo wa huduma kwa kuzindua huduma za Mkopo wa ChapChap, C2B na Mfuko wa Faraja kwa lengo la kuongeza urahisi na ufanisi wa huduma kwa wanachama.
Katika mafanikio yaliyopatikana mwaka 2026, amesema Saccos imepata hati inayoridhisha ya ukaguzi kutoka Shirika la Ukaguzi na Usimamizi wa Vyama vya Ushirika (Coasco) kwa hesabu za mwaka 2025, ikiwa ni mwaka wa tano mfululizo.
Mrajisi Msaidizi wa Vyama vya Ushirika Mkoa wa Dar es Salaam, Anjela Nalimi amesema Mkoa wa Dar es Salaam una jumla ya vyama vya ushirika 324, kati ya hivyo, 278 ni Saccos na vyama 46 ni vile visivyo vya kifedha.
Amesema hali hiyo inaonesha kuwa asilimia 86 ya vyama vyote vya ushirika mkoani hapa ni vya Saccos, huku vyama 46 vilivyobaki vikiwa ni vile ambavyo si vya kifedha.
Amesema kati ya vyama 20 vikubwa vya ushirika nchini, vyama 11 vinatoka Dar es Salaam pekee, ikimaanisha kuwa asilimia 55 ya vyama bora vya ushirika na mikopo nchini vipo katika mkoa huo,
Kwa upande wake, Chalamila amewataka viongozi wa Bandarini Saccos kuweka mbele uwajibikaji na usimamizi thabiti wa rasilimali na fedha za wanachama.
Amesema hatua hiyo ni msingi mkuu wa kujenga uaminifu, kulinda masilahi ya wanachama wote na kuhakikisha chama kinapata maendeleo endelevu.
Chalamila amesema viongozi wana wajibu wa kuwa mfano bora katika utendaji kazi kwa kuwa na mtazamo chanya na usimamizi usio na upendeleo.
Amesema uwajibikaji wa kweli utasaidia kuepusha migogoro na changamoto za kifedha zinazoweza kujitokeza kutokana na usimamizi mbovu au ukosefu wa uaminifu.
Chalamila amesema linapokuja suala la usimamizi wa fedha za wanachama, uwajibikaji lazima uwe kipaumbele cha kwanza kwa kuwa, viongozi wanapowajibika ipasavyo na kusimamia rasilimali kwa uwazi, wanajenga msingi imara unaolinda maslahi ya kila mwanachama na kuzuia migogoro ya kifedha.
