Uvuvi haramu, uchafuzi vyatia hofu Ziwa Tanganyika
Dar es Salaam. Katibu Mkuu Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), Dk Richard Muyungi, amezitaka nchi nne zinazopakana na Ziwa Tanganyika kuimarisha ushirikiano katika kukabiliana na uvuvi haramu, uchafuzi wa maji, kupungua kwa ubora wa maji na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Amesema maazimio ya mkutano wa 15 wa Kamati ya Usimamizi ya Mamlaka ya Ziwa Tanganyika (LTA) yanapaswa kuwa na mapendekezo yanayotekelezeka ili kuwezesha baraza la mawaziri la nchi hizo kufanya maamuzi yatakayolinda ziwa hilo na rasilimali zake.
“Maazimio haya yatasaidia katika kulinda bayoanuai ya ziwa, kuhifadhi shughuli za kiuchumi na fursa za uchumi wa buluu zinazopatikana kwenye ziwa hili,” alisema Dk Muyungi.
Alisema Ziwa Tanganyika lina umuhimu mkubwa kwa maisha ya wananchi, usalama wa chakula na maendeleo ya kiuchumi, likitegemewa na zaidi ya watu milioni 13 katika nchi nne zinazolizunguka ambazo ni Tanzania, Burundi, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) na Zambia.
Mkutano huo wa siku nne ulianza Oktoba 25, 2026, ukiwa na lengo la kupitia utekelezaji wa shughuli za uhifadhi na kuandaa mapendekezo yatakayowasilishwa katika mkutano wa baraza la mawaziri wa nchi hizo, unaotarajiwa kufanyika Oktoba 29 na 30 mwaka huu.
Mkurugenzi wa Mazingira kutoka Ofisi ya Makamu wa Rais, Kemilembe Mutasa, ambaye pia ni mkuu wa ujumbe wa Tanzania katika mkutano huo, alisema maamuzi yatakayofikiwa na kamati hiyo yatakuwa na mchango mkubwa katika kulishauri baraza la mawaziri kuhusu usimamizi wa ziwa hilo.
“Ushauri kwa baraza la mawaziri utategemea zaidi maazimio ya mkutano huu,” alisema Mutasa, akisisitiza umuhimu wa wajumbe kuzingatia masuala yanayohitaji maamuzi ya kikanda ili kulinda rasilimali za ziwa na kunufaisha jamii zinazolitegemea.
Dk Richard Muyungi, Katibu Mkuu wa Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira), akizungumza wakati wa mkutano wa 15 wa Kamati ya Usimamizi ya Mamlaka ya Ziwa Tanganyika (LTA), ulioanza Oktoba 25, 2026, jijini Dar es Salaam. Aliwataka wajumbe kuandaa mapendekezo yanayotekelezeka yatakayosaidia kulinda ziwa hilo dhidi ya uchafuzi, uvuvi haramu na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Kamati ya Usimamizi ya LTA na mwakilishi kutoka Zambia, Richard Lungu, alisema ziwa hilo linakabiliwa na changamoto zinazoongezeka kutokana na uvuvi usio endelevu, uharibifu wa makazi ya viumbe hai, uchafuzi na athari za mabadiliko ya tabianchi.
Alisema hali hiyo inazitaka nchi wanachama kuharakisha utekelezaji wa programu za kikanda, ikiwemo Programu ya Maendeleo Jumuishi ya Kikanda na Programu ya Kimkakati ya Utekelezaji, ili kuimarisha uhifadhi na usimamizi endelevu wa rasilimali za ziwa.
Lungu alisisitiza umuhimu wa kutumia taarifa za kisayansi katika kusimamia rasilimali za uvuvi, kulinda bayoanuai na kudhibiti uchafuzi wa maji.
Aliongeza kuwa nchi wanachama zinapaswa kutimiza ahadi zao za kifedha na kutafuta washirika wa maendeleo ili kuhakikisha programu za mamlaka hiyo zinapata fedha za kutosha.
Mkurugenzi Mtendaji wa LTA, Dk Emma Liwenga, alisema mamlaka hiyo imeanza kupitia upya programu yake ya kimkakati ya utekelezaji, ambayo ilifanyiwa mapitio mara ya mwisho mwaka 2012, kutokana na kuongezeka kwa changamoto za kimazingira.
Alisema mamlaka hiyo imewasilisha mapendekezo ya miradi kwa African Water Facility na Shirika la Umoja wa Mataifa la Chakula na Kilimo (FAO), yakilenga kuimarisha usimamizi wa rasilimali za maji na uvuvi wa ndani ya nchi.
Dk Liwenga alisisitiza kuwa ushirikiano kati ya nchi hizo nne na washirika wa maendeleo ni muhimu katika kukabiliana na changamoto hizo na kuhakikisha ziwa linaendelea kutoa manufaa kwa vizazi vya sasa na vijavyo.

