Wakazi Mwanza walalamikia honi za bodaboda, RPC atangaza operesheni
4 mins read

Wakazi Mwanza walalamikia honi za bodaboda, RPC atangaza operesheni

Mwanza. Wakazi wa Kata ya Luchelele jijini Mwanza wamelalamikia baadhi ya bodaboda zinazofanyiwa marekebisho ya mifumo ya honi na kusababisha kutoa sauti kubwa zinazofanana na milipuko, wakisema hali hiyo inawashtua na kuwafanya kudhani ni mabomu yanayolipuka au eneo lao limevamiwa, hasa nyakati za usiku.

Wakieleza changamoto zao za kiusalama katika mkutano wa Ongea na Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza uliofanyika Jumamosi Oktoba 24, 2026, wamesema honi hizo husikika kuanzia jioni hadi usiku, wakati wakazi wengi wamepumzika majumbani mwao.

Mkazi wa eneo hilo, Josephina Anthony, amesema baadhi ya wananchi huchukua hatua za kujilinda wakidhani wamesikia mlipuko wa bomu, lakini baadaye hugundua kuwa sauti hizo zimetokana na bodaboda.

“Hizi honi za bodaboda zinazotoa sauti kama milipuko, hasa nyakati za usiku, zinatushtua sana. Wakati mwingine mtu anasikia sauti hiyo ghafla na kudhani ni bomu limelipuka au kuna watu wamevamia eneo letu.

“Unasikia inalia puuh, puuh, unashtuka! Unadhani ni bomu limelipuka au kuna watu wamevamia. Tunaomba mamlaka zichukue hatua ili hali hii ikomeshwe na wananchi waishi kwa amani bila hofu,” amesema Anthony huku umati wa watu ukimshangilia, kuonyesha ukubwa wa kero hiyo.

Akijibu malalamiko hayo, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbrod Mutafungwa, amesema operesheni dhidi ya pikipiki zinazofanyiwa marekebisho yanayosababisha sauti zisizo za kawaida zinaendelea, huku akielekeza askari wa usalama barabarani kuwachukulia hatua wanaokiuka sheria.

“Wataendeleza misako kwa nguvu katika maeneo haya. Pia, askari wa usalama barabarani watahakikisha wote wanaokiuka sheria wanakamatwa,” amesema.

Hata hivyo, amesema elimu kwa waendesha pikipiki inapaswa kutolewa kabla ya hatua za ukamataji ili kuwasaidia kubadili tabia hiyo.

Katika mkutano huo, Mutafungwa pia ameelekeza kufanyika kwa operesheni dhidi ya pombe haramu aina ya gongo baada ya kubaini baadhi ya washiriki wakiwa wamelewa.

“Fanyeni operesheni ya matumizi ya unywaji wa pombe haramu aina ya gongo. Watu kuanzia asubuhi wamelewa chakari, mchana wamelewa,” amesema.

Mutafungwa amesema ulevi unaathiri afya, familia na uzalishaji wa nguvu kazi ya taifa, huku akibainisha kuwa unaweza kuchangia vitendo vya uhalifu.

Mkuu wa Polisi Wilaya ya Nyamagana, Virginia Sodoka akizungumza na wakazi wa Kata ya Luchelele katika mkutano wa Ongea na Kamanda wa Polisi.

Amewataka viongozi wa eneo hilo kushirikiana na polisi kukabiliana na tatizo hilo na kuhakikisha sheria zinafuatwa.

Mkuu wa Polisi Wilaya ya Nyamagana, Virginia Sodoka, amewataka wakazi wa Luchelele kupunguza unywaji wa pombe na kuzingatia muda uliowekwa kisheria wa kuendesha biashara za vileo.

Kauli hiyo imekuja baada ya baadhi ya wananchi kueleza kuwa wanakunywa pombe kwa lengo la kujifurahisha.

Sodoka amesema ni muhimu wananchi kufurahia maisha bila kuathiri shughuli za uzalishaji na majukumu yao ya kila siku.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa kwenye habari hii, Sheria ya Vileo, Sura ya 77, inaweka muda wa kuuza vileo kwa matumizi ndani ya baa katika maeneo ya mijini kuwa saa 12 jioni hadi saa 5 usiku Jumatatu hadi Ijumaa. Jumamosi, Jumapili na sikukuu, muda huo ni saa 5 asubuhi hadi saa 8 mchana, kisha saa 12 jioni hadi saa 6 usiku.

Katika mkutano huo, wakazi pia wamewasilisha changamoto ya kutokamilika kwa ujenzi wa kituo cha polisi katika kata hiyo.

Mkazi wa eneo hilo, Zabron Juma, amesema ujenzi wa kituo hicho umedumu kwa takribani miaka 25 bila kukamilika, hali inayozua maswali kuhusu upatikanaji wa huduma za kipolisi katika eneo hilo.

Kwa upande wake, Mtendaji wa Kata ya Luchelele, Shadrack Mboje, amesema eneo hilo pia linakabiliwa na tatizo la fisi ambao wamekuwa wakiwasababishia wakazi hasara kwa kuvamia mabanda na kuondoka na mifugo.

Akizungumzia ujenzi wa kituo cha polisi, Mutafungwa amewataka viongozi wa eneo hilo kuweka kipaumbele katika kukikamilisha kwa kushirikisha wananchi na wadau wa maendeleo.

Amesema ushirikiano huo unaweza kusaidia kutatua changamoto iliyodumu kwa muda mrefu na kuimarisha huduma za kiusalama katika kata hiyo.

Mutafungwa amesisitiza kuwa jukumu la kudhibiti uhalifu halipaswi kuachwa kwa polisi pekee, bali viongozi wa mitaa na vijiji wanapaswa kuanzisha na kuimarisha vikundi vya ulinzi shirikishi ili kusaidia kubaini vitendo vya uhalifu mapema na kutoa taarifa kwa vyombo vya usalama.

Ameongeza kuwa wananchi wanapaswa kuendelea kushirikiana na polisi kwa kutoa taarifa kuhusu vitendo vya uhalifu, akisema taarifa hizo zitasaidia uchunguzi na kuchukuliwa kwa hatua za kisheria dhidi ya wanaobainika kuhusika.

Source link

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *