Wakazi Mbozi waiangukia Tarura ukarabati wa barabara kukabiliana na El-Nino
2 mins read

Wakazi Mbozi waiangukia Tarura ukarabati wa barabara kukabiliana na El-Nino

Songwe. Wakazi wa Kitongoji cha Ichenjezya Mama, Wilaya ya Mbozi mkoani Songwe, wameuomba Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (Tarura) kufanyia matengenezo barabara yao, wakihofia kukatika kwa mawasiliano wakati wa mvua za El-Nino zinazotarajiwa kunyesha.

Wakizungumza hivi karibuni, wakazi hao wamedai kuwa, ubovu wa barabara hizo umekuwa kikwazo katika shughuli zao za kila siku, ikiwamo usafiri, usafirishaji wa mazao na upatikanaji wa huduma muhimu, huku wakihofia mvua zinazotarajiwa kunyesha kuharibu kabisa mawasiliano.

Mkazi wa Kitongoji cha Ichenjezya Mama, Michael Katembo amesema hali ya barabara hiyo inahitaji kushughulikiwa kabla mvua hazijawa nyingi ili kuzuia uwezekano wa kukatika kwa mawasiliano.

“Barabara hii inahitaji kufanyiwa matengenezo mapema kabla mvua hazijawa nyingi, tuna hofu kuwa, hali inaweza kuwa mbaya zaidi na kutusababishia kushindwa kupita katika baadhi ya maeneo,” amesema Katembo.

Amesema wakazi wengi wanategemea barabara hiyo kwa shughuli mbalimbali, hivyo kuharibika kwake zaidi kunaweza kuathiri usafiri na shughuli za kiuchumi zinazowategemea.

Mkazi mwingine wa eneo hilo, Maria Mwashiuya amesema hali ya barabara inaweza kuwa kikwazo kwa wananchi wanaohitaji kusafiri kwa shughuli za biashara, kupata huduma za afya na kutekeleza majukumu ya kijamii.

“Tunaiomba mamlaka inayohusika kuangalia hali ya barabara hii na kuchukua hatua mapema ili mvua zikianza kunyesha kwa wingi tusikumbane na tatizo la kukosa njia ya kupita,” amesema Mwashiuya.

Mkazi mwingine, Aneth Fumbo amesema miundombinu ya barabara katika kitongoji hicho ipo katika hali mbaya, hivyo hatua za mapema zinahitajika ili kupunguza uwezekano wa kukatika kwa mawasiliano wakati wa mvua.

“Tunachohitaji ni barabara inayoweza kupitika hata wakati wa mvua, kwa sababu maisha yetu ya kila siku yanategemea njia hii kufika maeneo mbalimbali na kufanya shughuli zetu,” amesema Fumbo.

Meneja wa Tarura Wilaya ya Mbozi, Jane Mdula amekiri kuwa barabara hiyo ina hali mbaya licha ya umuhimu wake kwa wananchi, akisema imejumuishwa katika mpango wa matengenezo wa mwaka wa fedha 2026/27.

Mdula amesema matengenezo hayo yanatarajiwa kutekelezwa katika awamu ya pili ya mpango huo, unaohusisha barabara ya kutoka Vwawa Day kuelekea Sumbaluwela, yenye urefu wa kilomita tano.

Amesema utekelezaji wa matengenezo ya barabara hizo umegawanywa katika awamu mbili, ya kwanza inahusisha asilimia 60, huku awamu ya pili ikihusisha asilimia 40.

“Niwahakikishie wananchi wa Ichenjezya Mama kwamba barabara hiyo itatengenezwa awamu ya pili, tunatarajia wananchi wasipate shida kipindi cha mvua zinazotarajiwa kunyesha,” amesema Mdula.

Source link

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *