Mradi wa umeme Songea –Tunduru kufungua fursa za kiuchumi kusini
Songea. Mradi wa kusafirisha umeme wa msongo wa kilovoti 220 kutoka Songea hadi Tunduru, wenye urefu wa kilomita 214 utasaidia kuimarisha Gridi ya Taifa.
Hivyo, Waziri wa Nishati, Dk Juma Homera amemtaka mkandarasi anayetekeleza mradi huo aongeze kasi ya kazi ili ukamilike kwa wakati.
Mradi huo unajumuisha pia ujenzi wa Kituo cha Kupokea, Kupoza na Kusambaza Umeme cha Tunduru, huku ukitarajiwa kuboresha upatikanaji wa umeme kwa wananchi wa mikoa ya Ruvuma, Lindi na Mtwara.
Utekelezaji wake unatarajiwa kuchochea shughuli za kiuchumi na kijamii katika mikoa hiyo ya kusini mwa Tanzania.
Hayo yamesemwa na Waziri Homera leo Jumatatu Oktoba 26, 2026, wakati wa ziara ya kukagua maendeleo ya mradi huo unaotekelezwa katika sehemu kuu mbili.
Sehemu ya kwanza inahusisha ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme wa msongo wa kilovoti 220 kutoka Songea hadi Tunduru, yenye urefu wa kilomita 214, pamoja na ujenzi wa kituo cha kupokea, kupoza na kusambaza umeme cha Tunduru.
Sehemu ya pili ni ujenzi wa njia ya kusafirisha umeme wa msongo huo kutoka Tunduru hadi Masasi, yenye urefu wa kilomita 177.
Waziri wa Nishati, Dk Juma Homera (wa kwanza kulia), wakati akipewa maelekezo katika ukaguzi wa mradi wa kusafirisha umeme wa msongo wa kilovoti 220 kutoka Songea hadi Tunduru, wenye urefu wa kilomita 214 utasaidia kuimarisha Gridi ya Taifa.
“Nimeona maendeleo ya mradi. Tanesco, msimamieni mkandarasi ili aweze kuongeza kasi ya utekelezaji wa mradi. Dhamira ya Serikali ni kuona wananchi wa mikoa ya kusini wananufaika na uwekezaji katika sekta ya umeme, ambayo imekuwa na mchango mkubwa katika shughuli za kiuchumi na kijamii,” amesema Homera.
Akizungumza kwa niaba ya Mkurugenzi Mtendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco), Naibu Mkurugenzi Mtendaji anayeshughulikia Mipango, Utafiti na Uwekezaji, Mhandisi Amos Kaihula, amesema utekelezaji wa mradi wa njia ya kusafirisha umeme kutoka Songea hadi Masasi umefikia asilimia 56, huku sehemu ya Tunduru hadi Masasi ikiwa imefikia asilimia 34.
“Utekelezaji wa miradi hii ni muhimu kwa kuwa inalenga kuhakikisha wananchi wa mikoa ya kusini wananufaika na umeme wa uhakika. Tunafanya jitihada kubwa za kumsimamia mkandarasi ili aweze kukamilisha kazi kwa wakati na kwa ufanisi, kwa maslahi ya maendeleo ya nchi na Taifa kwa ujumla,” amesema Kaihula.
Mradi huo unatekelezwa na Kampuni ya Kalpataru Projects International Limited kutoka India.
Sehemu ya kwanza, inayohusisha njia ya Songea hadi Tunduru, inagharimu Sh150.78 bilioni, huku sehemu ya pili ya Tunduru hadi Masasi ikigharimu Sh157.69 bilioni.

