Heroin ilivyomweka mahabusu miaka 12, Jopo la majaji lamwachia huru
Moshi. Haijaisha mpaka iishe, ndivyo ilivyotokea kwa Rukia Mohamed ambaye ameachiwa huru baada ya miaka 12 akipigania haki yake ya kuwa huru, baada ya kuhukumiwa kifungo cha maisha mara mbili na Mahakama Kuu.
Desemba 21, 2013 katika uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Kilimanjaro (KIA), Rukia alituhumiwa kukamatwa akisafirisha gramu 1,478.15 za dawa za kulevya aina ya Heroin Hydrochloride zenye thamani ya Sh66.2 milioni.
Aprili 10,2018, Mahakama Kuu kanda ya Moshi ikamtia hatiani na kumhukumu kutumikia kifungo cha maisha jela, akakata rufaa Mahakama ya Rufani, ambapo mahakama ikaamuru kesi hiyo isikilizwe upya kwa sehemu.
Shauri hilo lilirejeshwa ili kusikilizwa kuanzia katika hatua ya kuhitimisha na kuwasilisha muhtasari wa ushahidi kwa washauri wa mahakama (assessors) , kutokana na mapungufu yaliyojitokeza katika uwasilishaji huo wa muhtasari.
Kufuatia kutii agizo hilo, Mahakama Kuu ilitoa hukumu yake mpya Septemba 15, 2023, ikimhukumu tena mrufani na kumpatia adhabu ya kifungo cha maisha.
Hakuridhika, akakata rufaa tena mahakama ya Rufani ambapo safari hii jopo la majaji watatu, Ferdinand Wambali, Agnes Ngeyekwa na Yose Mlyambina katika hukumu yao waliyoitoa Oktoba 26,2026 wamemwachia huru.
Hapo sasa ndio uhalisia wamsemo wa Haijaisha mpaka iishe unapoingia unaomaanisha jambo au mapambano yoyote hayajafikia kikomo rasmi hadi pale hatua ya mwisho kabisa inapokamilika. Ndicho kilichotokea kwa Rukia.
Kulingana na ushahidi wa upande wa mashitaka, ulidai Desemba 21, 2013 katika Uwanja wa KIA), mrufani alikutwa akisafirisha gramu 1,471.15 za dawa za kulevya aina ya heroin hydrochloride, zenye thamani ya Sh66.2 milioni.
Kimsingi, shahidi namba 4 na 7 wa upande wa mashtaka walidai siku hiyo saa 8 usiku walikuwa zamu ya usiku Uwanja wa Ndege KIA.
Shahidi namba 4 alidai muda huo alimuona abiria, ambaye baadaye alitambulika kama Rukia akionekana na wasiwasi wakati akielekea kwenye kaunta za uhamiaji.
Kwa upande wake, shahidi namba 7 yeye alidai ni Ofisa wa usalama wa uwanja wa ndege anayesimamia mashine ya kukagua mizigo (HBS) kwa ajili ya safari ya ndege ya Shirika la Ethiopian Airlines.
Alidai aligundua begi la kahawia lenye kutia shaka ambalo yaliyomo ndani yake hayakuweza kutambuliwa wazi kupitia kifaa cha kukagua kwa mionzi ya X-ray.
Kwa mujibu wa shahidi huyo, begi hilo, akabaini jina la ukoo la mmiliki, Mohamed, kutoka kwenye lebo, na akampata mshtakiwa (Rukia) akiwa pamoja na shahidi wa upande wa mashtaka namba 4.
Kulingana na mashahidi, walidai mshtakiwa alithibitisha umiliki wa begi hilo mbele ya shahidi wa mashtaka namba wa 4, shahidi wa mashtaka namba 7, mkaguzi msaidizi shufaa, na Koplo Amini.
Baada ya begi hilo kufunguliwa na nguo zake binafsi kutolewa, mashahidi wa upande wa mashitaka walidai begi hilo tupu lilipitishwa tena kwenye mashine ya ukaguzi, ambapo kitu kilichofichwa ndani yake kilionekana.
Shahidi namba 4 alikagua kwa mikono sehemu ya ndani ya begi hilo na kwa ridhaa ya mrufani, alikata sehemu ya chini iliyokuwa imetengenezwa kwa hila kwa kutumia kisu kidogo.
Ndani yake, walitoa ubao wa plastiki na bahasha ya rangi ya kaki iliyofungwa kwa utepe wa plastiki (cello tape) wa rangi ya njano, ambayo ilikuwa na unga wa rangi ya kahawia unaodhaniwa kuwa dawa za kulevya.
Ni katika hatua hiyo, mshitakiwa alikamatwa na kupelekwa kituo cha Polisi KIA ambapo uchunguzi baadaye ulibaini unga huo ulikuwa ni Heroini.
Katika utetezi wake, Rukia alikana shtaka hilo na kupinga maelezo ya upande wa mashtaka na kueleza kuwa usiku wa Desemba 20, 2013, alikwenda KIA kupanda ndege kwenda Nigeria kumtembelea mchumba wake.
Alisema kwamba mzigo wake ulikuwa begi lenye mistari nyeusi na nyeupe, ambalo aliliacha na mhudumu kabla ya kuendelea kwenda uhamiaji.
Rukia alijitetea kwamba alipokuwa akisubiri eneo la kukaa abiria, Ofisa wa polisi ambaye ni shahidi namba 4 alimpeleka kwenye chumba cha mahojiano chenye mifuko mitatu ya kahawia iliyo wazi.
Alidai shahidi huyo kuwa moja ya mifuko yenye jina Mohamed ilikuwa yake na ilikuwa na dawa za kulevya, ambazo Rukia alikana, akidai kwamba begi lake lilikuwa na mistari na halikuwa miongoni mwa zile zilizoonyeshwa.
Alidai hakuwepo wakati begi hilo lilipochunguzwa, kufunguliwa au kukatwa.
Zaidi ya hayo alikataa kusaini cheti chochote cha kukamatwa au bahasha ya maonyesho, akidai sahihi yake ilikuwa ya kughushi, na akaomba aachiliwe huru kwa misingi kwamba alihusishwa kwa uwongo.
Hata hivyo, mahakama ilimtia hatiani na kumhukumu kifungo cha maisha.
Kupitia kwa wakili wa kujitegemea, Patrick Paul, mshitakiwa huyo alipinga vikali hukumu pamoja na adhabu aliyopewa akiegemea sababu kuu tano.
Alilalamika kuwa kielelezo P6 (kwa ujumla wake) kilitumiwa kimakosa kama ushahidi kwa sababu hakikutajwa wakati wa hatua za awali za maandalizi ya kesi (committal proceedings) wakati wa mchakato wa ukabidhi.
Pili, hakukuwa na uhusiano wowote kati ya begi lililokutwa na dawa hizo zilizokamatwa na mrufani.
Tatu, cheti cha kukamatwa kwa vitu (kielelezo P8) kilitumiwa kimakosa kwa kuwa hakikusainiwa na mrufani na saini iliyopo ilipingwa vikali na mrufani.
Nne, kesi ya upande wa mashtaka ilitegemea ushahidi dhaifu, usio na mashiko, unaojipinga, usio thabiti, usioaminika na usiofaa kutegemewa; na tano, kesi dhidi yake haikuthibitishwa pasipo kuacha mashaka yoyote.
Katika usikilizwaji wa rufaa hiyo, upande wa Jamhuri uliwakilishwa na wakili mwandamizi wa Serikali Isack Mangunu, akisaidiwa na mawakili wa Serikali Sospeter Mdee na Angela Mshana.
Akijibu hoja hizo, wakili Mangunu alikiri wazi kuwa hatua za awali za maandalizi ya kesi (committal proceedings) ziliendeshwa kwa njia isiyo sahihi kuhusiana na uorodheshaji na usimamizi wa vielelezo.
Hata hivyo, alisisitiza kuwa kosa hili la kiutaratibu halikuwa na athari ya kuharibu kesi ya upande wa mashtaka, wala halikusababisha kupindishwa kwa haki au madhara yoyote ambayo yangehalalisha kufutwa kwa hukumu ya hatia bila kuwepo kwa suluhisho lingine mwafaka.
Wakili huyo alieleza kuwa vielelezo hivyo hatimaye vilijumuishwa wakati wa kuorodhesha mashahidi na vielelezo ambavyo upande wa mashtaka na upande wa utetezi walikusudia kuvitumia.
Kwa hivyo, wakili huyo alihimiza kuwa kasoro hiyo ya kiutaratibu iliyotokea katika hatua ya maandalizi ya kesi haipaswi kusababisha kufutwa kabisa kwa mwenendo wa kesi hiyo, na akaomba Mahakama izingatie kutoa amri inayofaa kama vile kuamuru kesi isikilizwe upya ili kurekebisha kasoro hiyo ya kiutaratibu.
Katika hukumu yao iliyowekwa katika tovuti ya Tanzlii leo Oktoba 27,2026, jopo la majaji hao watatu walisema Kifungu cha 263(2) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA) kinataka upande wa mashtaka, katika hatua za maandalizi ya kesi (committal proceedings), kuwasilisha maelezo na nyaraka zenye kiini cha ushahidi wa mashahidi ambao upande wa mashtaka unakusudia kuwaita.
“Katika kesi hii, suala linatokana na namna ambavyo dawa za kulevya zinazodaiwa kuwa heroini, pamoja na mfuko ambao inasemekana zilikutwa ndani yake vilivyowekwa wazi wakati wa hatua za maandalizi ya kesi,”walisema.
“Ni dhahiri kwamba, si dawa hiyo inayodaiwa kuwa heroini au mfuko huo, havikuwemo katika orodha husika ya vielelezo”
“Kinyume chake, vitu vyote viwili vilijumuishwa katika orodha iliyofuata, iliyohusu mashahidi na vielelezo vilivyokusudiwa kutumiwa na upande wa mashtaka pamoja na upande wa utetezi,”walieleza majaji.
“Baada ya kuchunguza sehemu ya rekodi ya rufaa, inaonekana kwamba heroini inayodaiwa kuwa na uzito wa gramu 1,471.15 na mfuko huo hazikuwa miongoni mwa vielelezo vilivyofichuliwa awali kwa mrufani wakati wa kesi ya kuwasilisha kesi kama inavyotakiwa na sheria kwa mujibu wa kifungu cha 263 cha CPA kilichotajwa na kunakiliwa hapo juu,”waliongeza kusema.
“Kuingizwa kwao baadaye katika orodha ya vielelezo kunaibua swali kama utaratibu uliopitishwa ulifuata mahitaji ya kisheria yanayosimamia ufichuzi wa vielelezo hivyo, kama kielelezo P6 kilikubaliwa ipasavyo katika kesi hiyo”.
“Tumebaini kuwa kuachwa kwa kile kinachodaiwa kuwa heroini pamoja na mfuko huo kutoka kwenye orodha ya vielelezo haikuwa kasoro ndogo ya kiutaratibu”.
“Dawa za kulevya zinazodaiwa kuhusika zilikuwa na umuhimu wa msingi katika kuthibitisha asili na ukubwa wa maudhui yanayounda msingi wa shtaka hilo.”
“Hatimaye, tunakubali rufaa, tunatengua hukumu ya hatia na kuondoa adhabu ya kifungo cha maisha iliyotolewa na Mahakama Kuu dhidi ya mrufani.”
Majaji hao wakahitimisha kwa kuamuru kwamba mrufani, Rukia Khamis Mohamed, aachiwe huru kutoka gerezani mara moja, isipokuwa kama anashikiliwa kwa sababu nyingine halali kisheria.

