TBS yaonya wanaochanganya pombe msimu wa sikukuu
4 mins read

TBS yaonya wanaochanganya pombe msimu wa sikukuu

Dar es Salaam. Wakati msimu wa sikukuu za mwisho wa mwaka ukikaribia, Shirika la Viwango Tanzania (TBS) limewaonya wananchi dhidi ya kuchanganya pombe na vinywaji vya kuongeza nguvu vyenye kafeini, likieleza kuwa mchanganyiko huo unaweza kuficha athari za ulevi na kumfanya mtu kunywa pombe nyingi zaidi.

Onyo hilo linakuja wakati wa maandalizi ya sikukuu za mwisho ya mwaka yakianza huku matumizi ya pombe hutajwa kufanyika kwa kiasi kikubwa, huku TBS ikikiri kuwa kipindi hicho hushuhudiwa ongezeko kubwa la uingizaji wa vileo.

Akizungumza leo Oktoba 27, 2026 Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Dk Ashura Katunzi amesema licha ya pombe zinazoingizwa kuwa zimethibitishwa kufaa kwa matumizi lakini ubora wa kinywaji hauondoi hatari za kiafya zinazoweza kusababishwa na unywaji uliopitiliza au matumizi yasiyo salama.

Amesema kafeini iliyomo kwenye vinywaji vya kuongeza nguvu inaweza kumfanya mtu ajihisi yuko macho zaidi, bila kupunguza kiwango cha pombe katika damu au kurejesha uwezo wake wa kufanya maamuzi sahihi.

“Unapochanganya pombe na kinywaji cha kuongeza nguvu chenye kafeini, kafeini inaweza kuficha athari za ulevi. Mtu anaweza kujihisi yuko macho na hajalewa wakati mwili wake umeathiriwa na pombe,” amesema DK Katunzi alipokuwa akizungumza na wahariri katika mkutano ulioratibiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina.

Amesema hali ya kujihisi macho inaweza kumshawishi mtu kunywa pombe zaidi kuliko alivyokusudia na hivyo kuongeza hatari ya madhara yanayohusiana na unywaji wa pombe.

“Mchanganyiko huo unaweza pia kumfanya mnywaji asitambue kwa usahihi kiwango ambacho uwezo wake umeathiriwa na pombe, jambo linaloweza kudhoofisha maamuzi na uratibu wa mwili, kujihisi macho, lakini hakumaanishi kuwa mtu hajalewa au yuko katika hali salama ya kuendesha gari,” amesema.

Ametoa kauli hiyo wakati akieleza kuwa kipindi cha Novemba hadi Januari hushuhudiwa ongezeko la uingizaji wa bidhaa za pombe, peremende na vyakula vilivyofungashwa, wakati wafanyabiashara wanapojiandaa kukidhi mahitaji makubwa ya msimu wa sikukuu.

Amesema kuanzia mwaka 2021 shirika hilo lilikuwa likitoa huduma za usajili wa bidhaa za chakula na vipodozi pamoja na maeneo ya uzalishaji, uuzaji, usambazaji na uhifadhi wa chakula na vipodozi kwa lengo la kuhakiki ubora na usalama wa maeneo hayo ili kuendelea kulinda afya za walaji.

“Katika kipindi husika jumla ya bidhaa 9,731 zilisajiliwa na maeneo 80,836 yalisajiliwa. Pombe ndiyo inaongoza kuwa miongoni mwa bidhaa zilizosajiliwa na TBS, huku uingizaji wake ukiongezeka wakati wa kuelekea msimu wa sikukuu,” amesema.

Ili kuhakikisha bidhaa zinazoingia nchini zinakidhi viwango vinavyotakiwa, TBS hutumia mfumo wa ukaguzi kabla ya kutoka katika nchi husika unaohusisha ukaguzi wa bidhaa husika kabla hazijasafirishwa kuingia nchini.

Takwimu za TBS zinaonesha kuwa shehena 183,186 zilikaguliwa kabla ya kusafirishwa kupitia mfumo huo na shehena 426,842 zilikaguliwa baada ya kuwasili nchini huku magari 249,386 yaliyotumika nayo yakikaguliwa.

“Ukaguzi huo unalenga kuhakikisha bidhaa zinazoingia nchini zinakidhi matakwa ya viwango na usalama kabla ya kuwafikia watumiaji, pamoja na kuzuia Tanzania kuwa soko la bidhaa duni,” amesema.

Amesema katika kuimarisha uwezo wa kuthibitisha ubora wa bidhaa, TBS imepima sampuli 188,952 katika kipindi hicho.

“Serikali pia imetumia takribani Sh12.9 bilioni kununua mashine za kisasa za maabara ili kuwezesha upimaji kufanyika kwa wakati na kwa usahihi,” amesema.

Mbali na pombe, Dk Katunzi amesema Tbs inaendelea kuboresha huduma zake na kufuatilia ubora wa vifaa vya umeme majumbani ili kuhakikisha vinavyotumika na wananchi vinakidhi viwango vinavyotakiwa.

Hata hivyo amesisitiza umuhimu wa kuendelea kutoa elimu kwa umma kuhusu ubora wa bidhaa, akieleza kuwa wananchi na wadau wanapaswa kutumia huduma za maabara za Tbs ili kupata uhakika wa ubora wa bidhaa wanazonunua na kutumia.

“Vifaa vya umeme wa ndani tunaendelea kuboresha huduma zetu na kufuatilia wakati ambao shirika linaendelea kutoa elimu kupitia majukwaa mbalimbali,” amesema.

Mwakilishi wa Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Tausi Mbowe amesema Tbs ina wajibu mpana wa kusimamia ubora katika sekta mbalimbali zikiwemo ujenzi, chakula na vifaa vya umeme kwani udhaifu katika usimamizi wa viwango unaweza kuhatarisha maisha ya watu na kudhoofisha nguvu kazi ya Taifa.

“Watanzania tunawategemea. Nyinyi ndio wasimamizi wa ubora wa bidhaa mbalimbali nchini. Tunapozungumzia ujenzi, chakula na vifaa vya umeme, Tbs ipo kwahiyo, tunawaomba msilegeze kamba, hakikisheni mnafanya kazi yenu vizuri kwa uzalendo,” amesema.

Source link

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *