Wafungwa kupata msaada wa kisheria magerezani
2 mins read

Wafungwa kupata msaada wa kisheria magerezani

Dar es Salaam. Wafungwa na mahabusu wanatarajiwa kupata huduma za msaada wa kisheria, kufahamu haki zao na kufuatilia hatua za mashauri yao baada ya Wizara ya Katiba na Sheria na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi kusaini makubaliano ya kuimarisha utoaji wa huduma hizo magerezani.

Makubaliano hayo yanalenga kuimarisha uratibu kati ya taasisi zinazohusika na huduma za msaada wa kisheria huku yakisisitiza matumizi ya mifumo ya kidijitali katika usimamizi wa taarifa za mashauri ili kuboresha upatikanaji wa haki kwa wafungwa na mahabusu.

Hili linakuja ikiwa ni siku tatu tangu Jeshi la Magereza Tanzania kutangaza kuanza kuandaa utaratibu wa kutumia bima ya afya kwa wafungwa na mahabusu ili kupunguza gharama za matibabu, madeni yanayotokana na huduma hizo na kuboresha upatikanaji wa huduma za afya ndani ya vituo vya magereza nchini.

Akizungumza leo Jumanne Oktoba 27, 2026 katika hafla ya utiaji saini, Waziri wa Katiba na Sheria, Abdallah Hamis Ulega amesema ushirikiano huo utaimarisha uratibu wa utoaji wa huduma za Msaada wa Kisheria kwa Wafungwa na Mahabusu.

Ili hilo lifanikiwe utaandaliwa mpango kazi utakaobainisha majukumu ya kila taasisi na matokeo yanayotarajiwa sambamba na kuimarisha matumizi ya mifumo ya kidijitali katika usimamizi wa taarifa za mashauri.

“Haki haipaswi kumfuta mtu kiuchumi. Wafungwa na Mahabusu wana haki ya kupata haki kwa usawa bila kujali hali zao za kiuchumi. Hivyo, tuna wajibu wa kusimamia, kuratibu na kuwezesha upatikanaji wa huduma za msaada wa kisheria magerezani,” amesema.

Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Patrobas Katambi amesema makubaliano hayo yatawasaidia wafungwa na mahabusu kuelewa haki zao, taratibu za kisheria na hatua zinazopaswa kuchukuliwa katika mashauri yao.

Hadi Mei 2026, Tanzania ilikuwa na jumla ya wafungwa na mahabusu 23,514 katika magereza yake ambapo wafungwa walikuwa 19,704 na mahabusu walikuwa 3,810.

Kamishna Jenerali wa Jeshi la Magereza Tanzania Bara, Jeremiah Yoram Katungu amesema kupitia Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia, Wafungwa na Mahabusu 19,511 katika mikoa ya Dodoma, Manyara, Shinyanga, Simiyu, Ruvuma, Singida na Njombe wamenufaika na Huduma za Msaada wa Kisheria.

Ameongeza kuwa watumishi 290, wakiwamo maofisa sheria, maofisa urekebu na wasaidizi wa kisheria, wamepatiwa mafunzo ya kuwajengea uwezo wa kutoa huduma hizo kwa ufanisi.

Pia, mwongozo wa uanzishaji na uendeshaji wa madawati ya msaada wa kisheria magerezani umezinduliwa katika hafla hiyo kwa lengo la kuimarisha uratibu na usimamizi wa huduma hizo.

Katika hatua nyingine, Katungu amesema kuanzia Januari mosi hadi Septemba 30, 2026, mashauri 2,809 yalisikilizwa kupitia mfumo wa Mahakama mtandao, huku vituo 84 vya magereza vikiwa na vifaa vinavyowezesha huduma hiyo.

Makubaliano hayo yanatarajiwa kuimarisha ushirikiano kati ya taasisi za haki jinai na kuhakikisha wafungwa na mahabusu wanapata huduma za kisheria kwa kuzingatia utu wa binadamu, usawa mbele ya sheria na misingi ya utawala wa sheria.

Source link

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *