COPRA yasukuma kilimo endelevu kuhifadhi mazingira
Kibaha. Mkurugenzi Mkuu wa Mazingira wa Wizara ya Kilimo, Mwanaisha Tumbo, amesisitiza umuhimu wa kuhifadhi mazingira katika shughuli za kilimo, akiwataka wadau kuzingatia matumizi ya mbegu bora, pembejeo zinazofaa na uzalishaji endelevu.
Amesema msisitizo huo unaendana na mkakati wa mwaka 2026/27 wa Mamlaka ya Udhibiti wa Nafaka na Mazao Mchanganyiko (COPRA), unaolenga kuboresha usimamizi wa sekta hiyo huku ukizingatia uhifadhi wa mazingira.
Tumbo ameyasema hayo leo Oktoba 27, 2026, katika mkutano wa COPRA uliofanyika Kibaha, Mkoa wa Pwani, ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya miaka mitatu tangu kuanzishwa kwa mamlaka hiyo.
Amesema Serikali imeipa sekta ya kilimo nafasi ya kimkakati katika kufikia malengo ya Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, kwa kusisitiza uzalishaji wenye tija unaozingatia uendelevu na kulinda mazingira.
“Serikali imeiweka sekta ya kilimo kwenye sekta za kimkakati katika kufikia malengo ya Dira 2050, ikisisitiza kilimo endelevu kinachoongeza tija ya uzalishaji na kulinda mazingira,” amesema.
Katika kutekeleza mkakati huo, COPRA imeshirikiana na Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kuandaa rasimu za viwango vya Kanuni Bora za Kilimo (GAP) kwa mazao ya nafaka, yakiwemo kunde, pamoja na mazao ya bustani.
Hatua hiyo inalenga kuhakikisha uzalishaji unazingatia kanuni zinazolinda mazingira na kudumisha rutuba ya udongo.
Akifafanua kuhusu mpango mkakati huo, Kaimu Mkurugenzi wa Huduma za Taasisi wa COPRA, Martin Sapanjo, amesema umeainisha maeneo matano ya kipaumbele ambayo ni ushindani na ubunifu katika masoko, uzalishaji wenye tija, matumizi ya mifumo ya kidijitali, ufanisi wa utendaji na kuweka mazingira wezeshi.
Amesema vipaumbele hivyo vimeandaliwa kwa kuzingatia uzoefu wa nchi nyingine zilizopiga hatua katika usimamizi wa sekta ya kilimo.
“Katika kuandaa mpango mkakati huu, tumejifunza kutoka kwa wenzetu wa Afrika Kusini ambao wanafanya vizuri zaidi, hivyo tumeainisha vipaumbele muhimu katika kufikia malengo tuliyojiwekea,” amesema Sapanjo.
Ameongeza kuwa mafanikio ya mkakati huo yanategemea kilimo endelevu, upatikanaji wa masoko ya uhakika na ushirikiano wa wadau ili kuhakikisha ukuaji shirikishi katika sekta hiyo.
“Haya yatafikiwa kupitia kilimo endelevu, masoko ya uhakika, ushirikiano na wadau na kuhakikisha ukuaji wa pamoja na shirikishi katika kila tunachokifanya,” amesema.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya COPRA, Profesa Sifuni Mchome, amesema kubadilishwa kwa maeneo ya kilimo kuwa makazi na maeneo ya viwanda ni miongoni mwa changamoto zinazoathiri uzalishaji wa mazao, ikiwemo minazi katika Mkoa wa Pwani.
Amesema hali hiyo inaonyesha umuhimu wa kuwa na mipango bora ya matumizi ya ardhi inayozingatia mahitaji ya maendeleo bila kuathiri maeneo muhimu ya uzalishaji wa kilimo.
Hatua hizo zinaendana na Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050, inayosisitiza usimamizi endelevu wa rasilimali za asili, uhifadhi wa mazingira na kuongeza ustahimilivu dhidi ya mabadiliko ya tabianchi.

