Ukosefu elimu ya fedha unavyokwamisha upatikanaji wa mikopo
2 mins read

Ukosefu elimu ya fedha unavyokwamisha upatikanaji wa mikopo

Dar es Salaam. Ukosefu wa elimu ya fedha na utamaduni mdogo wa kurejesha mikopo ni miongoni mwa changamoto zinazowakabili wajasiriamali wadogo, hali inayoweza kuongeza matatizo yao wanapokopa bila kutathmini uwezo wa kulipa.

Hayo yameelezwa leo Jumatano, Oktoba 28, 2026 na Ofisa Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Taifa wa Huduma Ndogo za Kifedha, Santiel Yona alipozungumza na wanahabari katika mkutano ulioandaliwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina.

Amesema baadhi ya wananchi hukimbilia mikopo wanaposikia inapatikana, bila kuzingatia mahitaji yao na uwezo wa kurejesha fedha hizo.

Amesema changamoto hiyo imeifanya taasisi hiyo kuendelea kutoa elimu kwa wateja kabla ya kuwapatia mikopo, ikiwemo kuwajengea uelewa kuhusu wajibu wa kurejesha fedha walizokopa.

“Kuna wakati hili linaleta shida. Mtu anaposikia kuna mkopo unatolewa hapimi, anakwenda tu kuchukua,” amesema.

Santiel amesema wafanyabiashara wengi wadogo hawajarasimisha shughuli zao, hali inayowaweka katika mazingira magumu wanapokumbwa na majanga na kuhitaji msaada wa kuendeleza biashara.

Amesema taasisi hiyo inawahimiza wajasiriamali kupata leseni ili kurahisisha uendelezaji wa biashara zao na kuwawezesha kuendesha shughuli zao katika mazingira rasmi.

“Tunapotaka kwenda kumpa mtu mkopo kama hana leseni akatafute ili biashara yake iwe rasmi na rahisi kuendelea,” amesema.

Katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita, Santiel amesema taasisi hiyo imetoa mikopo yenye thamani ya Sh38 bilioni kwa zaidi ya wananchi 100,000, iliyochangia kuzalisha ajira 262,000.

Amesema katika kipindi hicho, taasisi hiyo imepata faida ya Sh3 bilioni na kulipa Serikali gawio la Sh490 milioni.

Ameeleza kuwa mikopo hiyo inalenga makundi mbalimbali, yakiwemo wajasiriamali, wakulima, wafugaji, wavuvi na watumishi wa umma, huku baadhi ya huduma zikilenga kuwawezesha wananchi kumiliki mali na kujiajiri.

Amesema vijana pia wanaweza kupata mikopo inayowawezesha kumiliki vyombo vya usafiri kama Bajaj na kuvitumia katika shughuli za kiuchumi.

Huduma nyingine ni mikopo ya kukamilisha ujenzi wa nyumba, mikopo ya nishati safi na bima zinazosaidia wanufaika kukabiliana na majanga mbalimbali.

Amesema taasisi hiyo ina matawi 12 yaliyopangwa kuhudumia maeneo tofauti nchini, lakini katika miaka mitano ijayo inalenga kupanua huduma za kidigitali ili kuwafikia wananchi wasiokuwa karibu na matawi.

Santiel amesema Serikali imeipatia taasisi hiyo fedha katika mpango wa mikopo ya Sh200 bilioni kwa makundi mbalimbali, ambazo zitaanza kutolewa mwakani.

Ameongeza kuwa wanaendelea kufuatilia wanufaika ili kutathmini maendeleo yao na kutoa elimu ya fedha kwa lengo la kuimarisha matumizi sahihi ya mikopo na urejeshaji wake.

Akizungumza kwa niaba ya wahariri, Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Jukwaa la Wahariri, Bakari Kimwaga amesema uhusiano mwema kati ya taasisi hiyo na wanahabari unaongeza uelewa wa umma kuhusu huduma inazotoa.

“Hii tunapokutana inasaidia wakati mwingine hata kujua taasisi ambazo kabla hatukuwa tunazijua kabisa. Huu ni utaratibu mzuri na nafikiri tuendelee kushirikiana,” amesema Kimwaga.

Pia, amesema wanahabari nao wanaweza kuwa sehemu ya wajasiriamali au wawekezaji wanaohitaji mikopo kupata mitaji ya biashara, hivyo muhimu wanapopata elimu ya fedha.

Source link

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *