Sekta binafsi kubeba Sh62.3 trilioni za Mpango wa Maendeleo 2027
4 mins read

Sekta binafsi kubeba Sh62.3 trilioni za Mpango wa Maendeleo 2027

Dar/Dodoma. Mpango wa Serikali wa 2027/28 unatarajia kubebwa na Sekta binafsi inayotarajia kugharamia Sh62.3 trilioni, sawa na takribani asilimia 70 ya Sh89.3 trilioni zinazokadiriwa kukusanywa na kutumika kutekeleza Mpango wa Maendeleo wa Taifa kwa mwaka huo.

Utekelezaji wa mpango huo umejikita katika maeneo sita ya kipaumbele ambayo yatasaidia uchumi kukua kwa asilimia 6.6, ambayo ni uchumi imara, jumuishi na shindani, uwezo wa watu na maendeleo ya jamii, uhifadhi wa mazingira na ustahimilivu wa mabadiliko ya tabia nchi.

Maeneo mengine ni vichocheo vya maendeleo, kuimarisha utekeleza wa sekta za mageuzi na kuimarisha misingi ya uendelevu wa Taifa.

Hayo yameelezwa bungeni jijini Dodoma leo, Oktoba 28, 2026 na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo, alipowasilisha mapendekezo ya mpango wa maendeleo wa taifa, unaokusudiwa kutekelezwa na Serikali kwa mwaka wa fedha 2027/28.

Amesema Serikali inatarajia kuchangia Sh20.7 trilioni kutoka bajeti yake, huku mashirika ya umma yanayojiendesha kibiashara yakitarajiwa kuwekeza Sh6.3 trilioni kwenye bajeti hiyo.

Kwa mujibu wa Waziri, mkakati huo unaweka sekta binafsi kama mshirika mkuu wa uwekezaji na utekelezaji wa vipaumbele vya maendeleo, chini ya Mpango wa Nne wa Maendeleo wa Taifa wa miaka mitano (2026/27–2030/31).

Waziri amesema katika mpango huo, Serikali inatarajia wastani wa ajira mpya kufikia milioni 1.7 mwaka 2027, kutoka ajira 981,000 mwaka 2025.

“Dira 2050 itahukumiwa kwa kuzingatia kama inaboresha fursa zao, kipato, maisha na ustawi wao,” amesema Profesa Mkumbo, akisisitiza kuwa utekelezaji wa mipango ya maendeleo lazima uonyeshe matokeo yanayopimika.

Kwenye mpango huo wanufaika wa Bima ya Afya wanatarajia kuongezeka hadi kufikia asilimia 32.38 mwaka wa fedha 2027/28, kutoka makadirio ya asilimia 25 mwaka 2026/27 huku eneo la usafirishaji kwa njia ya Reli ya Kati likitarajiwa kufikia tani milioni moja kutoka tani 810,000 mwaka 2026/27.

Viwanda, kilimo vyapewa kipaumbele

Waziri amesema Serikali imeweka kipaumbele maeneo matano ya minyororo ya thamani yanayotarajiwa kuongeza uzalishaji, thamani ya bidhaa na mauzo ya nje ikiwemo kilimo cha maua na mazao ya bustani, ufugaji wa viumbe maji, utafiti na uchimbaji wa madini na kuongeza thamani, uzalishaji wa mafuta ya kula na uzalishaji wa nguo.

Amesema Serikali itaendeleza uzalishaji na uongezaji thamani wa mazao ya kilimo, yakiwamo korosho, sukari na ngano ambapo uwekezaji katika maeneo hayo utahusisha hatua zote za minyororo ya thamani, kuanzia uzalishaji, uchakataji na uhifadhi hadi usafirishaji na masoko.

Katika enepo la ufugaji Serikali inalenga kuimarisha uzalishaji wa mbegu na chakula cha viumbe hai, vifaa vya ufugaji, miundombinu ya kuhifadhi bidhaa katika ubaridi na matumizi ya teknolojia za kidijitali.

Akizungumzia eneo la elimu ya sekondari kwa watu wote kuanzia 2028, amesema Serikali itaendelea kujiandaa kutekeleza elimu ya sekondari kwa wote, ikilenga kuboresha elimu na mafunzo ya ujuzi yanayokidhi mahitaji ya soko la ajira, hususan katika sayansi, teknolojia, uhandisi na hisabati.

Profesa Mkumbo, amesema mafanikio ya dira hiyo hayatategemea ubora wa nyaraka pekee, bali maamuzi, rasilimali zitakazokusanywa, uwezo wa taasisi na uwajibikaji katika utekelezaji ya malengo yaliyowekwa.

Waziri anasema mpango wa mwaka 2027/28 utatekelezwa kupitia programu saba za kielelezo, miradi shikizi 38 na maeneo 34 ya minyororo ya thamani huku akisisitiza kuwa Bunge, sekta binafsi, mamlaka za serikali za mitaa, taasisi za elimu na utafiti, asasi za kiraia na wananchi wana wajibu katika kufanikisha malengo hayo.

Waziri Kitila amesema mpango wa 2027/28 unatarajia kutekelezwa kupitia programu saba zinazolenga kuunganisha miradi ya maendeleo na minyororo ya thamani ambazo zitajumuisha uendeleaji wa mji wa ikolojia ya Bahari ya Bagamoyo na usafirishaji fungamanishi.

Nyingine itakuwa ni uchimbaji na uchakataji wa makaa ya mawe Mchuchuma na chuma cha Liganga, pamoja na kiwanda cha kuchakata gesi asilia kuwa kimiminika mkoani Lindi.

“Programu nyingine ni uendelezaji wa kitovu cha teknolojia na uchakataji wa madini adimu Dodoma, mpango wa kitaifa wa umwagiliaji na mageuzi ya viwanda vya kuchakata mazao ya kilimo, kitovu cha viwanda na uchumi wa buluu katika ukanda wa maziwa makuu na uendelezaji wa miji nchini,” amesema.

Source link

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *