Kamati ya Mkuu wa Mkoa Mara yabaini madudu usimamizi wa usafi maeneo nyeti
Mara. Baadhi ya masoko, minada na machinjio mkoani Mara yamebainika kukosa utaratibu mzuri wa usafi wa mazingira, hali inayosababisha upepo kusambaza uchafu katika maeneo mengine.
Hali hiyo imebainika katika tathmini ya usafi wa mazingira iliyofanywa na timu maalumu iliyoundwa na Mkuu wa Mkoa wa Mara, Brigedia Jenerali Evans Mtambi, kwa lengo la kutathmini hali ya usafi katika halmashauri za wilaya, miji na manispaa za mkoa huo.
Tathmini hiyo imebaini changamoto mbalimbali zinazohusiana na uhifadhi na utupaji wa taka ngumu, zikiwamo takataka kurundikwa katika maeneo yasiyo rasmi, mifereji kujaa makopo na mifumo ya maji taka kutokuwa katika hali nzuri.
Akitoa taarifa ya tathmini hiyo mjini Musoma, Oktoba 26, 2026, Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mara, Dk Zabron Masatu amesema timu hiyo ilitembelea maeneo mbalimbali ya utoaji huduma za umma ili kubaini hali halisi ya usafi wa mazingira na namna halmashauri zinavyotekeleza wajibu wao katika eneo hilo.
Maeneo yaliyofanyiwa tathmini ni pamoja na vyoo vya umma, stendi za mabasi, masoko, machinjio na maeneo ya utoaji huduma za chakula.
Amesema matokeo ya tathmini hiyo yamebaini baadhi ya halmashauri kutokuwa na utaratibu maalumu wa kufanya usafi wa mazingira, hali inayochangia uchafu kuendelea kuwepo katika maeneo yanayotumiwa na wananchi kila siku.
Akieleza hali iliyokutwa katika baadhi ya maeneo hayo, Dk Masatu amesema kuna maeneo ambayo usafi haufanyiki ipasavyo kiasi cha mbwa kula mizoga iliyoachwa, huku upepo ukisambaza uchafu kwenda maeneo mengine.
“Yapo baadhi ya maeneo kama kwenye machinjio, minadani na masoko tumebaini hakuna usafi unaofanyika badala yake mbwa ndio wanasaidia kufanya usafi kwa kula mizoga huku upepo ukipeperusha uchafu na kupeleka maeneo mengine,” amesema.
Matokeo hayo yamekuja wakati Serikali ya Mkoa wa Mara ikitangaza kampeni rasmi ya usafi inayolenga kuhakikisha mazingira yanakuwa safi wakati wote, badala ya usafi kufanyika kwa vipindi maalumu pekee.
Kupitia kampeni hiyo, tathmini ya hali ya usafi katika halmashauri inatarajiwa kufanyika kila mwezi ili kupima utendaji wa maeneo husika na kuhimiza uwajibikaji wa viongozi na watendaji.
Katika tathmini iliyohusisha kipindi cha Septemba hadi Oktoba 2026, Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti imeibuka mshindi kwa kupata asilimia 70, ikifuatiwa na Halmashauri ya Manispaa ya Musoma iliyopata asilimia 68.
Halmashauri ya Wilaya ya Tarime imekuwa ya mwisho baada ya kupata asilimia 25, matokeo yaliyoifanya kukabidhiwa kinyago cha fisi kama ishara ya kushika nafasi ya mwisho katika tathmini ya usafi wa mazingira.
Kwa upande mwingine, Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti imepewa tuzo kwa kuibuka kidedea, huku Manispaa ya Musoma ikipewa cheti kwa kushika nafasi ya pili.
Akizungumza katika kikao hicho, Mkuu wa Mkoa wa Mara, Brigedia Jenerali Evans Mtambi amesema usafi wa mazingira ni suala la lazima na amezitaka halmashauri kuweka mipango mkakati inayotekelezeka katika kusimamia usafi.
Amesema mkoa huo una mifugo mingi na pia una Hifadhi ya Taifa ya Serengeti, hivyo uchafuzi wa mazingira, hususan unaotokana na taka za plastiki, unaweza kuwa na athari kubwa kiuchumi, kijamii na kimazingira.
“Kuna hizi taka za plastiki ambazo zinazagaa mitaani, hizi taka ni hatari kwa mifugo na wanyamapori endapo zitaliwa, zina uwezo mkubwa wa kuua hawa wanyama kuanzia sasa napiga marufuku matumizi ya mifuko hii,” amesema.
Mtambi amesema uchunguzi uliofanyika umebaini mifuko ya plastiki inayotumika kama vifungashio inaingizwa mkoani humo kutoka nchi jirani.
Kutokana na hali hiyo, ameagiza mamlaka husika kufanya msako ili kuwabaini wanaojihusisha na uingizaji na usambazaji wa mifuko hiyo ambayo imepigwa marufuku.
Pia, amemuagiza Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara kuunda timu ya wataalamu itakayofuatilia hali ya usafi katika halmashauri zote na kubaini namna zilivyojipanga kuhakikisha zinatimiza wajibu wao.
“Niliunda kamati kwa ajili ya kufanya tathmini ya hali ya usafi katika halmashauri zetu na matokeo yake ndiyo haya, hii operesheni ya usafi ni endelevu kuanzia sasa, tunatakiwa kutumia sheria zetu ndogo kuhakikisha tunaimarisha hali ya usafi wa mazingira katika maeneo yote ndani ya mkoa,” amesema.
Amesema baada ya kubaini kuwepo kwa takataka zilizozagaa katika maeneo mbalimbali, alianzisha operesheni ya usafi kupitia mpango aliouita Tuisheni.
Kupitia mpango huo, wakuu wa wilaya na watendaji wa Serikali ambao maeneo yao yalikuwa yakikutwa na uchafu waliitwa ofisini kwake alfajiri kabla ya muda wa kazi ili kutoa maelezo kuhusu hali ya usafi katika maeneo yao.
“Uchafu ni ishara ya kuwa na jamii ambayo haijastaarabika, sisi Mara tumestaarabika, viongozi na watendaji wote kila mmoja kwa nafasi yake wajibikeni, suala la usafi wa mazingira ni lazima sio hiari,” amesema.

