Watuhumiwa 40 wa ujangili wanaswa Serengeti ndani ya wiki mbili
Tarime. Zaidi ya watuhumiwa 40 wa ujangili wamekamatwa katika kipindi cha wiki mbili zilizopita wakitumhumiwa kujihusisha na vitendo vya ujangili katika hifadhi ya Taifa ya Serengeti (Senapa) kanda ya kaskazini.
Watuhumiwa hao wamekamatwa kupitia doria za mara kwa mara zinazofanyika katika hifadhi hiyo katika kanda ya kaskazini ambayo inapatikana wilayani Tarime Mkoa wa Mara.
Akizungumza katika mkutano wa ujirani mwema leo Oktoba 28,2026 uliohusisha wakazi wa vijiji vinne vya Kata ya Gorong’a na viongozi wa Serikali wilayani Tarime, uliofanyika katika Kijiji cha Masanga, Mkuu wa Hifadhi ya Taifa Serengeti Kanda ya Kaskazini, Ezron Lema amesema watuhumiwa wote wamekabidhiwa polisi kwa ajili ya hatua zaidi.
Amesema doria hizo endelevu zinalenga kuhakikisha hakuna vitendo vya ujangili vinafanyika na kufanikiwa ndani ya hifadhi hiyo ambayo imekuwa bora barani Afrika na duniani kwa ujumla.
Amesema suala la ulinzi wa rasilimali za taifa ikiwemo hifadhi hiyo ni jukumu la kila Mtanzania kwa maelezo kuwa sekta za uhifadhi, wanyamapori na utalii zina mchango mkubwa kwa maendeleo ya jamii na Taifa kwa ujumla. Hivyo kuitaka jamii hiyi kuwa sehemu ya kutokomeza vitendo vya ujangili.
Baadhi ya wakazi wa Kata ya Gorong’a wilayani Tarime, wakiwa kwenye kikao cha ujirani mwema kilichofanyika katika Kijiji cha Masanga wilayani humo kwaajili ya kuimarisha mahusiano kati yao na hifadhi ya Taifa ya Serengeti (Senapa). Picha na Beldina Nyakeke
“Hifadhi ya Serengeti kanda ya kaskazini inatamani sana kuendelea na mahusiano mazuri na jamii inayotuzunguka kwani tunaamini kuwa walinzi namba moja wa hifadhi ni jamii, mahusiano haya pia yatasaidia jamii kupata maendeleo endelevu kupitia mnyororo wa mzima wa uhifadhi,” amesema.
Akizungumza katika mkutano huo, Mkuu wa Wilaya ya Tarime, Meja Edward Gowele amesema lengo la kuhitisha mkutano huo pamoja na mambo mengine ni kutaka kujadili kwa pamoja namna ya kuendelea kuimarisha mahusiano kati ya hifadhi na jamii.
Gowele amesema ushirikiano kati ya jamii na hifadhi utasaidia kukomesha vitendo vya ujangili ambavyo amesema vinafanywa na watu wasioitakia maendeleo endelevu jamii inayozunguka hifadhi na Taifa kwa ujumla.
Ameagiza uongozi wa vijiji na kata kufanya mikutano na kuibua miradi ya maendeleo ili iweze kutekelezwa na hifadhi hiyo kupitia mpango wa ujirani mwema unaotekelezwa na hifadhi hiyo.
Gowele amesema zipo changamoto mbalimbali hususan katika sekta za elimu,maji afya na miundombinu changamoto ambazo Serikali imekuwa ikijitahidi kuzipatia ufumbuzi na kwamba uwepo wa wadau kama hifadhi hiyo ni fursa muhimu pia katika kuleta ufumbuzi wa changamoto hizo kupitia mpango huo wa ujirani mwema hivyo
Pia, ameuagiza uongozi wa hifadhi hiyo kuwa na utaratibu wa kufanya mikutano ya ujirani mwema katika vijiji hivyo kila baada ya miezi mitatu ili wote jwa pamoja waweze kuajdili fursa zilizopo na kuzitumia.
“Kupitia mikutano hii ya ujirani mwema mtakuwa na uwezo wa kubaini changamoto mapema na kuzifanyiakazi kwa pamoja ili kudumisha mahusiano mema kwa maendeleo endelevu ya jamii na hifadhi, ” amesema.
Baadhi ya wakazi wa vijiji hivyo wamesema suala la mahusiano mema kati ya hifadhi na jamii ni la muhimu huku wakisema hakuna maendeleo kama pande hizo hazitakuwa na mahusiano mazuri.
Pia, wameuomba uongozi wa hifadhi kusaidia kuboresha huduma za kijamii ikiwepo suala la upatikanaji wa maji ambalo limekuwa changamoto katika kata nzima.
Baadhi ya wakazi wa Kata ya Gorong’a wilayani Tarime, wakiwa kwenye kikao cha ujirani mwema kilichofanyika katika Kijiji cha Masanga wilayani humo kwaajili ya kuimarisha mahusiano kati yao na hifadhi ya Taifa ya Serengeti (Senapa). Picha na Beldina Nyakeke
“Kata ya Gorong’a tuna shida kubwa sana ya maji, wanawake tunahangaika sana tunaomba Senapa mtuchimbie visima,” amesema Penina Mwita mkazi wa Kijiji cha Masanga.
Paulo Kirambo mkazi wa Kijiji cha, Masurura amesema mbali na visima pia wakazi hao hawana malambo ya kunywesha mifugo hivyo kuomba hifadhi hiyo kusaidia uchimbaji wa malambo.
“Zamani Senapa walituchimbia visima lakini kwasasa vile visima vimeharibika wanawake wanahangaika sana kutafuta maji tunaomba watuchimbie visima na malambo pia kwa ajili ya matumizi ya nyumbani na mifugo yetu,” amesema.
Mmoja wa wazee wa kimila, Abdallah Manga amesema suala la uhifadhi wanyamapori na mazingira kwa ujumla ni jukumu la jamii na kwamba kwa kulitambua hilo wazee wa mila wamekuwa mstari wa mbele katika kuhamasisha uhifadhi endelevu.
Amesema uharibifu wa mazingira unaathiri jamii nzima huku akitolea mfano wa ukataji wa miti hovyo ulivyosababisha wazee kukosa maeneo ya mitambiko.
“Zamani tulikuwa tunafanya mitambiko yetu kule juu mlimani na kulikuwa na miti mikubwa maalum kwa kazi hiyo lakini vijana wamekata hadi miti hiyo kwa hiyo unaweza kuona umuhimu wa uhifadhi na ushirikiano kati ya jamii na Senapa,” amesema.

