Polisi Mwanza kukagua kamera za usalama hosteli za wanafunzi
4 mins read

Polisi Mwanza kukagua kamera za usalama hosteli za wanafunzi

Mwanza. Jeshi la Polisi Wilaya ya Nyamagana mkoani Mwanza linatarajia kufanya operesheni ya kukagua uwepo wa kamera za CCTV katika hosteli za wanafunzi, baada ya kuwataka na kuwahamasisha wamiliki wa hosteli hizo kufunga vifaa hivyo kwa lengo la kuimarisha usalama wa wanafunzi katika vyuo mbalimbali jijini Mwanza.

Mkuu wa Polisi Wilaya ya Nyamagana, Virginia Sodoka amesema uwepo wa kamera hizo ni muhimu katika kusaidia usalama wa wanafunzi pamoja na Jeshi la Polisi kubaini wahusika wa uhalifu na kurahisisha upatikanaji wa ushahidi pale matukio yanapotokea.

Sodoka ametoa kauli hiyo hivi karibuni wakati akitoa elimu ya ulinzi na usalama kwa wanafunzi wa mwaka wa kwanza wa Chuo Kikuu cha Mtakatifu Augustine (Saut), akisisitiza wamiliki wa hosteli wanapaswa kuhakikisha maeneo yao yana mifumo imara ya ulinzi, huku wanafunzi wakitakiwa kuzingatia usalama wakati wa kuchagua maeneo ya kuishi.

“Eneo ambalo unaishi, hakikisha ni kuna usalama…hakikisha madirisha yako vizuri, milango, kamera imefungwa. Tumehamasisha sana wenye hosteli wafunge CCTV kamera, tutapita tena kwenye hosteli zenu..tutafanya operesheni tuone bado zinaendelea,” amesema.

Sodoka amesisitiza kuwa wanafunzi wanapaswa kujilinda wenyewe kwa kuepuka kutembea peke yao usiku katika maeneo yasiyo salama na kuwa waangalifu wanapotumia simu za mkononi wakiwa njiani.

Amesema wanafunzi, pia, wanatakiwa kujiepusha na vitendo vya wizi, uporaji, matumizi ya dawa za kulevya na tabia za biashara za ngono na nyingine zinazoweza kuwafanya washindwe kutimiza malengo yao ya kitaaluma.

Katika hatua nyingine, Sodoka amewaonya wanafunzi dhidi ya kujihusisha na siasa za uchochezi na vitendo vya uanaharakati vinavyoweza kusababisha vurugu na kuvuruga amani, akiwataka kuelekeza nguvu zao katika masomo badala ya kujiingiza katika shughuli zinazoweza kuwatoa kwenye malengo yao ya kitaaluma.

Amesema wanafunzi wanapaswa kutambua kuwa kipindi walichopo chuoni ni cha kujifunza na kujiandaa kwa maisha ya baadaye, huku akisisitiza kuwa fursa ya kushiriki katika shughuli za kisiasa itakuwepo watakapomaliza masomo yao.

 Mkuu wa Dawati la Jinsia na Watoto Mkoa wa Mwanza, Faraja Mkinga amewaomba walimu kuwapa wanafunzi shughuli nyingi za kitaaluma zitakazowafanya wakose muda wa kufanya vitendo vya kihalifu.

Amesema wanafunzi wanahitaji kuelekezwa na kushirikishwa katika shughuli zenye tija ili waweze kuzingatia malengo yao ya masomo na kuepuka kujiingiza katika vitendo vinavyoweza kuathiri maisha yao ya baadaye.

“Tunawaomba walimu muwape wanafunzi kazi na shughuli za kitaaluma zinazowafanya wawe bize. Hatujasema wasipate muda wa kupumzika, lakini ni muhimu wawe na shughuli za kufanya ili watumie muda wao vizuri na waepuke kujiingiza katika vitendo vya uhalifu,”amesema.

Akitoa elimu ya matumizi ya intaneti na mitandao ya kijamii, Mtendaji wa Dawati la Jinsia na Watoto wa Wilaya ya Nyamagana, Stella Ryimo amewaonya wanafunzi kuhusu athari za kushiriki picha na taarifa binafsi bila tahadhari, akiwataka kulinda faragha zao na kuzingatia athari za maudhui wanayochapisha mtandaoni.

Amesema matumizi ya mitandao ya kijamii huacha alama za kidijitali zinazoweza kuathiri taswira ya mtu katika jamii, hivyo wanafunzi wanapaswa kuwa makini na taarifa wanazoweka kwenye akaunti zao na zile wanazowatumia watu wengine.

“Tunapotumia mitandao ya kijamii, tunaacha alama za kidijitali. Hata kama hujachapisha picha au taarifa kwenye akaunti yako, bado unapaswa kujiuliza ni maudhui gani unayotazama, unayoshiriki na unayowatumia watu wengine. Vijana tunapaswa kuwa makini kwa sababu taarifa na picha zinazowekwa mtandaoni zinaweza kutumika kwa namna ambayo hatukuitarajia,” amesema.

Amewataka wanafunzi, hususan wanaoingia katika mahusiano ya kimapenzi, kuepuka kutuma picha za faragha kwa wenza wao, akieleza kuwa picha hizo zinaweza kutumiwa vibaya baada ya uhusiano kuvunjika na kusababisha udhalilishaji wa kidijitali.

 Mlezi wa wanafunzi wa Saut, Father Japhet Njaule ameliomba Jeshi la Polisi kurudisha kesi ndogo ndogo chuoni hapo ambazo siyo za kijinai zinazoripotiwa na wanafunzi pale wanapotofautiana wenyewe kwa wenyewe ili zitatuliwe chuoni hapo.

Amewataka wanafunzi wakumbuke kilichowapeleka chuoni na kuwa wazazi na walezi wao wana matarajio makubwa kwao, hivyo wanapaswa kuepuka vitendo vinavyoweza kuwakatisha tamaa au kuathiri masomo yao.

Source link

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *