Kaushio la jua kutoa matumaini kwa wavuvi wa dagaa
5 mins read

Kaushio la jua kutoa matumaini kwa wavuvi wa dagaa

Mbeya. Hasara inayowakabili wavuvi wa dagaa Ziwa Nyasa kutokana na mvua na mbinu zisizofaa za ukaushaji inaweza kupungua kupitia kaushio linalotumia nishati ya jua lililobuniwa na watafiti wa uvuvi wilayani Kyela, mkoani Mbeya.

Teknolojia hiyo inalenga kuboresha ukaushaji na utunzaji wa dagaa, kupunguza uharibifu wa mazao na kuwawezesha wavuvi kuongeza thamani ya bidhaa zao. Hata hivyo, wavuvi wanasema gharama za upatikanaji wa vifaa hivyo zinaweza kuwa kikwazo kwa wale wenye uwezo mdogo wa kifedha.

Mtafiti mkuu wa bunifu hiyo, ambaye pia ni Kaimu Mkurugenzi wa Kituo cha Utafiti wa Uvuvi Tanzania (Tafiri), Kituo cha Kyela, Nestory Peter, amesema teknolojia hiyo ilibuniwa baada ya kubainika kuwa wavuvi wanahitaji mbinu bora za kupunguza uharibifu wa dagaa baada ya kuvuliwa.

Amesema maandalizi ya utafiti huo yalianza mwaka 2011, wakati watafiti walipowasilisha andiko la kuomba ufadhili kutoka Tume ya Taifa ya Sayansi na Teknolojia (Costech).

“Tuliandaa andiko la kuomba fedha mwaka 2011 ili kuangalia uwezekano wa kusaidia namna ya kupunguza uharibifu wa dagaa katika Ziwa Nyasa. Tuliomba Sh306 milioni, ingawa hatukupata kiasi chote,” amesema Peter.

Jinsi kaushio linavyofanya kazi

Peter amesema watafiti walitengeneza na kujaribu aina nne za vikaushio ili kubaini mfumo unaoweza kukausha dagaa kwa ufanisi zaidi na kukidhi mahitaji ya wavuvi.

Majaribio hayo yalifanyika katika mwalo wa Matema, wilayani Kyela, yakihusisha vikaushio vya muundo wa hema, vikiwamo vilivyotumia nishati ya jua pamoja na mifumo mingine ya ukaushaji.

Amesema baada ya kulinganisha matokeo ya majaribio, kaushio la solar tent dryer lilionyesha matokeo mazuri katika ukaushaji na kuhifadhi joto linalohitajika.

Teknolojia hiyo ina muundo wa kabati maalumu lenye nguzo zilizofunikwa kwa karatasi laini za plastiki zinazowezesha joto kuingia na kusaidia kukausha dagaa.

Muundo huo unalenga kuboresha mazingira ya ukaushaji ikilinganishwa na kutandaza dagaa kwenye maeneo ya wazi ambako wanaweza kuathiriwa na mvua, vumbi na uchafu.

“Baada ya kufanya utafiti tulitengeneza vikaushio vya majaribio vyenye mfumo wa makasha na muundo wa hema, vikiwamo vinavyotumia umeme wa jua na vingine vya kawaida,” amesema.

Baada ya kupata matokeo ya awali, watafiti walianza kuitangaza teknolojia hiyo kwa wadau, ikiwamo kupitia maonyesho ya Nanenane, kwa lengo la kuongeza uelewa kuhusu matumizi yake.

Umuhimu wa kaushio hilo unaonekana zaidi wakati dagaa wanapovuliwa kwa wingi, lakini hali ya hewa inakwamisha ukaushaji.

Peter amesema dagaa wanapaswa kushughulikiwa kwa haraka baada ya kuvuliwa kwa sababu wanaweza kuharibika wasipotunzwa katika mazingira yanayofaa.

Amesema wingi wa dagaa wanaovuliwa kwa wakati mmoja unaweza kuzidi uwezo wa wavuvi kuwakausha kwa wakati, hali inayoweza kusababisha sehemu ya mazao kuharibika na kupunguza mapato yao.

Akielezea shughuli za uvuvi katika mwalo wa Matema, amesema wingi wa dagaa wanaovuliwa unahitaji mifumo inayoweza kukidhi mahitaji ya ukaushaji.

“Kimsingi katika mwalo mmoja unakuta kwa siku mitumbwi 1,000 yenye uwezo wa kubeba kilo 1,000 za dagaa. Endapo hawataandaliwa na kukaushwa kwa wakati, wanaharibika na kuwa hasara kwa mvuvi aliyetumia nguvu kubwa majini,” amesema.

Amesema katika mazingira yasiyofaa ya ukaushaji, upotevu unaweza kufikia nusu ya mzigo, akitoa mfano wa kilo 1,000 ambapo kilo 500 zinaweza kuharibika.

Mbali na kupunguza upotevu, teknolojia hiyo inalenga kuboresha ubora wa dagaa kwa kupunguza uwezekano wa mazao kugusana moja kwa moja na vumbi na uchafu unaopatikana kwenye maeneo ya wazi.

Hata hivyo, matumizi ya kaushio pekee hayatoshi kuhakikisha usalama wa bidhaa. Usafi wa vifaa, utunzaji wa dagaa kabla ya kukaushwa na uhifadhi baada ya kukaushwa ni mambo yanayopaswa kuzingatiwa ili kupata bidhaa bora.

Kwa hiyo, kuenea kwa teknolojia hiyo kunahitaji pia elimu kwa wavuvi kuhusu mbinu bora za usafi na utunzaji wa mazao ya uvuvi.

Peter amesema baada ya matokeo ya awali, utafiti uliendelezwa ili kuchunguza uwezekano wa kutumia teknolojia hiyo katika maeneo mengine ya shughuli za uvuvi.

Amesema matumizi ya kaushio hilo yamefanyika Matema na Kasyosyo, huku teknolojia hiyo ikifika pia Kipumbwi, mkoani Tanga, ambako shughuli za uzalishaji wa dagaa zinafanyika.

Maeneo mengine yanayohusishwa na shughuli za uvuvi katika Ziwa Nyasa ni Wilaya ya Ludewa mkoani Njombe na Nyasa mkoani Ruvuma.

Hata hivyo, amesema fedha zaidi zinahitajika ili kuzalisha vikaushio kwa wingi na kuvisambaza katika maeneo mengi ya uvuvi.

Kwa mujibu wake, ufadhili wa tafiti ni muhimu ili kuhakikisha bunifu zinazopatikana hazibaki katika hatua za majaribio, bali zinafika kwa walengwa na kuleta matokeo yanayotarajiwa.

“Miaka 40 ya Costech imekuwa na manufaa makubwa kwa watafiti, lakini ombi letu ni waendelee kutufadhili na kutusimamia ili tuendelee kufanya tafiti kubwa zaidi,” amesema.

Pamoja na matumaini yanayotokana na bunifu hiyo, gharama za upatikanaji wa vikaushio ni miongoni mwa changamoto zinazoweza kuzuia wavuvi wadogo kunufaika na teknolojia hiyo.

Festo Wille, mvuvi katika eneo hilo, amesema Serikali inapaswa kuangalia uwezekano wa kufadhili au kuwezesha upatikanaji wa kaushio hilo kwa gharama nafuu ili wavuvi wengi waweze kulitumia.

Amesema uwezo mdogo wa kifedha unawafanya baadhi ya wavuvi kushindwa kuwekeza katika vifaa vya kisasa, licha ya kuhitaji mbinu bora za ukaushaji ili kupunguza hasara.

“Kwetu wavuvi, changamoto ni ukata. Ingawa teknolojia zipo na ni nyenzo muhimu, ukosefu wa kipato ndio sababu ya kupata hasara kutokana na uzalishaji mkubwa na mbinu hafifu za ukaushaji,” amesema.

Source link

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *