DC Maswa: Msisubiri posho kuwahudumia wakulima
Maswa. Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Dk Vicent Anney, amewataka wataalamu wa kilimo kuacha kutegemea posho ili kutekeleza majukumu yao, akisema utendaji huo unaweza kukwamisha juhudi za kuongeza uzalishaji wa pamba na kuboresha maisha ya wakulima.
Amesema wataalamu wanapaswa kuelekeza nguvu katika kuwafikia wakulima mashambani, kutoa ushauri wa vitendo na kuhakikisha elimu ya kilimo inawasaidia kuongeza mavuno badala ya kusubiri malipo ya ziada kabla ya kutekeleza majukumu yao.
Akizungumza leo Oktoba 28, 2026, katika kikao cha watendaji wa sekta mbalimbali za Serikali wilayani humo, Dk Anney amesema mabadiliko ya mtazamo wa wataalamu ni muhimu katika kufikia malengo ya Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2050.
Baadhi ya wataalamu wa sekta mbalimbali katika halmashauri ya wilaya wakiwa kwenye kikao. Picha na Samwel Mwanga
“Ofisa kilimo ili kuwatembelea wakulima atahitaji posho, hivyo mtazamo huwa kufanya kazi kwa posho. Hatutaweza kufanikiwa na hatutaweza kufikia malengo ya Dira ya Maendeleo ya mwaka 2050,” amesema.
Amesema wataalamu wa Serikali wana wajibu wa kutumia ujuzi wao kutatua changamoto zinazowakabili wananchi na kuboresha uzalishaji kupitia huduma zinazotolewa kwa vitendo.
Dk Anney amesema pamba ni zao muhimu kiuchumi kwa Wilaya ya Maswa na Mkoa wa Simiyu kwa ujumla, hivyo juhudi za kuongeza uzalishaji zinapaswa kupewa kipaumbele.
Katika kuunga mkono juhudi hizo, Mkuu wa Divisheni ya Kilimo, Mifugo na Uvuvi wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa, Hassan Kiseto, amesema halmashauri imepanga kuanzisha mashamba darasa yenye ukubwa wa ekari 15 katika kila moja ya kata 36 za wilaya hiyo.
Amesema kupitia mashamba hayo, wakulima watafundishwa mbinu bora za uzalishaji, huku wakipatiwa mbegu bora na viuatilifu kwa lengo la kuongeza wastani wa mavuno ya pamba kutoka kilo 300 hadi kilo 800 kwa ekari.
“Tutawapatia mbegu bora na viuatilifu wakulima wa zao la pamba wapatao 216,126 ambao tumewaandikisha ili kuongeza uzalishaji wa pamba kwa ekari kutoka kilo 300 hadi kilo 800,” amesema Kiseto.
Mkurugenzi Mtendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa, Maisha Mtipa, amesema halmashauri ina matrekta 52, ambapo 50 yametolewa na Bodi ya Pamba Tanzania na mawili na Wizara ya Kilimo.
Amesema matrekta hayo yatapangiwa maeneo yanayolima pamba ili kurahisisha maandalizi ya mashamba na kuongeza ufanisi wa shughuli za kilimo.
Mtipa amesema Bodi ya Pamba Tanzania (TCB) itasimamia matumizi ya matrekta hayo kuhakikisha yanatumika kwa malengo yaliyokusudiwa na kuwasaidia wakulima kuongeza uzalishaji.
Mkulima wa pamba katika Kijiji cha Senani, wilayani Maswa, Jackson Msomi, amesema elimu ya mbinu bora za kilimo inapaswa kwenda sambamba na bei inayozingatia gharama za uzalishaji.
Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Maswa, Maisha Mtipa, akizungumza na wataalam mbalimbali wa wilaya katika utekekezaji wa Dira ya Maendeleo ya mwaka 2050. Picha na Samwel Mwanga
“Kuongeza mavuno ni muhimu, lakini kunapaswa kwenda sambamba na kuhakikisha bei ya zao hilo inazingatia gharama tunazozitumia kuandaa mashamba, kupalilia na kununua viuatilifu,” amesema.
Naye Emanuel Mboje, mkazi wa Kijiji cha Buyubi, amesema mashamba darasa na upatikanaji wa huduma za matrekta ni hatua zinazoweza kuwasaidia wakulima kuboresha uzalishaji.
Kwa upande wake mkulima, Eliza Simeon amesema juhudi za kuongeza uzalishaji zinapaswa kuambatana na mazingira yatakayomwezesha mkulima kupata faida.
Amesema bila kuzingatia gharama za uzalishaji na bei anayolipwa mkulima, ongezeko la mavuno pekee haliwezi kumaliza changamoto za kiuchumi zinazowakabili wakulima.

