Mabadiliko ya tabianchi yapunguza samaki, kuvuruga uchumi wa wavuvi Tanga
Tanga. Mabadiliko ya tabianchi yameanza kuathiri shughuli za uvuvi katika ukanda wa Pwani ya Tanga, huku wavuvi wakieleza kuwa upatikanaji wa samaki umekuwa mgumu hata katika vipindi ambavyo awali vilikuwa na mavuno mengi.
Mwenyekiti wa wavuvi wa kanda ya Deep Sea, Bahero Wathio, amesema hali ya uvuvi imekuwa ngumu kutokana na mabadiliko ya misimu ya joto na baridi, ambayo awali yalikuwa yakisaidia wavuvi kutambua vipindi vya kupata samaki wengi.
Amesema katika misimu iliyopita, wavuvi walikuwa na uhakika zaidi wa kupata samaki kulingana na mabadiliko ya misimu, lakini kwa sasa hali hiyo imebadilika na wakati mwingine wanakwenda baharini bila kupata mavuno yanayolingana na gharama walizotumia.
“Zamani tulikuwa tunapata samaki wengi katika misimu fulani, lakini sasa unaweza kwenda baharini na kutumia gharama nyingi bila kupata samaki wa kutosha,” amesema Wathio.
Mwenyekiti wa wavuvi, Bahero Wathio, akiwa ameshikilia samaki mkubwa katika Mwambao wa Deep Sea katika bahari ya Hindi. Picha na Mbonea Herman.
Ameeleza kuwa hali hiyo inaathiri kipato cha wavuvi na wafanyabiashara wanaotegemea shughuli za uvuvi, akisema kupungua kwa samaki kunapunguza uwezo wa wavuvi kumudu gharama za shughuli zao na kuhudumia familia zao.
Kwa upande wake, Nahodha Omari Ally amesema mabadiliko ya hali ya bahari yamekuwa changamoto kwa shughuli za uvuvi, hasa kutokana na mabadiliko ya mazingira ambayo wavuvi wamekuwa wakiyategemea kutambua maeneo yenye samaki.
Amesema hali hiyo inahitaji wavuvi kupata elimu zaidi kuhusu namna ya kukabiliana na mabadiliko hayo, ikiwemo kubaini maeneo mapya ya uvuvi na kutumia maarifa yanayoweza kuwasaidia kuendelea na shughuli zao kwa usalama.
Athari hizo pia zimeonekana katika biashara ya samaki. Makame Juma, mfanyabiashara wa rejareja anayejishughulisha na uchuuzi wa samaki, amesema upatikanaji mdogo wa samaki unaathiri biashara yake kwa sababu bidhaa anazohitaji kuuza sokoni hazipatikani kwa kiwango kinachotarajiwa.
Amesema wafanyabiashara wadogo wanategemea upatikanaji wa samaki kwa bei zinazowawezesha kununua na kuuza kwa faida, lakini hali inapokuwa ngumu, shughuli zao huathirika na kipato hupungua.
Mwenyekiti wa Soko la Samaki la Deep Sea jijini Tanga, Nora Makaranga, amesema soko hilo linakabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa samaki, hali inayowaathiri wafanyabiashara wanaotegemea bidhaa hiyo kama chanzo kikuu cha mapato.
Amesema kupungua kwa samaki sokoni kunaathiri mzunguko wa biashara na kufanya iwe vigumu kwa wafanyabiashara kupata bidhaa za kutosha kwa ajili ya wateja wao.
Naye Mery Juma, ambaye ni mamalishe katika soko hilo, amesema shughuli zake zinategemea upatikanaji wa samaki kwa ajili ya kuandaa chakula cha wateja, hivyo mabadiliko ya upatikanaji na bei ya samaki yanaweza kuathiri gharama za uendeshaji wa biashara yake.
Amesema wafanyabiashara wa chakula wanaotegemea samaki wanalazimika kukabiliana na hali inayobadilika sokoni, huku wakiendelea kutafuta namna ya kuendesha biashara zao.
Wachuuzi wakiendelea na mnada wa samaki kwenye soko la Deep Sea jijini Tanga. Picha na Mbonea Herman
Akizungumzia athari hizo, Gladis Manyika, Ofisa Uvuvi wa Jiji la Tanga, amesema mabadiliko ya tabianchi ni miongoni mwa changamoto zinazoweza kuathiri mazingira ya bahari na mifumo ya maisha ya viumbe wa majini, hali inayoweza kuwa na matokeo katika upatikanaji wa samaki.
Amesema ni muhimu kuimarisha elimu kwa wavuvi kuhusu uvuvi endelevu na utunzaji wa mazingira ya bahari ili kusaidia kulinda rasilimali za uvuvi kwa manufaa ya sasa na vizazi vijavyo.
Kwa upande wake, Omari Mohamed, Ofisa Mfawidhi wa Idara ya Uvuvi katika Wizara ya Mifugo na Uvuvi, Kanda ya Tanga, amesema ongezeko la joto baharini na mabadiliko ya kina cha maji yanaweza kusababisha baadhi ya samaki kuhama kutoka maeneo yao ya kawaida na kwenda maeneo mengine yanayokidhi mahitaji yao ya kimazingira.
Amesema ongezeko la joto duniani linasababisha kuyeyuka kwa barafu na kuchangia kupanda kwa kina cha bahari, huku ongezeko la joto la maji likiweza kuathiri pia mifumo ya ikolojia ya bahari, ikiwemo miamba ya matumbawe ambayo ni muhimu kwa maisha na mazalia ya baadhi ya viumbe wa baharini.
“Samaki wana mazingira maalumu wanayohitaji kwa ajili ya kuishi. Mabadiliko ya kina cha maji yanaweza kusababisha kuhama kutoka eneo moja kwenda jingine, hivyo mvuvi anapofika eneo alilozoea anaweza kukosa samaki aliowatarajia,” amesema Mohamed.
Ameongeza kuwa mabadiliko hayo yanahitaji tafiti zaidi ili kubaini kwa kina namna yanavyoathiri makundi mbalimbali ya samaki na maeneo yao ya kuishi, pamoja na kuweka mikakati ya kuwasaidia wavuvi kukabiliana na hali hiyo.

