Maziwa yanavyotumika kukata pombe baa
Dar es Salaam. Huenda siku za hivi karibuni, ukiingia katika baa umekuwa ukikutana na dumu la maziwa na kujiuliza linafanya nini humo.
Huenda ukadhani baadhi ya wateja huagiza maziwa hayo kama mbadala wa vileo, lakini kwa mujibu wa maelezo yaliyotolewa na baadhi ya watu, maziwa hayo hutumiwa na wanywaji wanaoamini yanaweza kuwasaidia kupunguza athari za pombe ili waendelee kunywa.
Matumizi hayo yanatajwa kuibuka baada ya baadhi ya wanywaji kuzoea kutumia vinywaji vya kuongeza nguvu maarufu energy drinks, wakiamini vinaweza kuwasaidia kuendelea na starehe.
Hata hivyo, matumizi ya maziwa na vinywaji vingine kwa lengo la kukata pombe kunaonywa na wataalamu wa afya na Shirika la Viwango Tanzania kuwa yanaweza kusababisha athari mbalimbali ikiwemo magonjwa ya Ini, saratani na magonjwa ya mfumo wa upumuaji.
Mbali na maziwa pia baadhi ya baa zimekuwa zikiweka kahawa na vitu vingine vinavyosadikika kusaidia kupunguza mning’inio wa pombe.
Akizungumza na Mwananchi mmoja wa watu waliowahi kutumia maziwa kukata pombe, Shadrack Lyimo amesema ujuzi huo aliupata kwa rafiki yake.
“Nilipoambiwa ilibidi nijaribu siku moja, nikiwa nakunywa konyagi na rafiki zangu ambao wanataka tukae muda mrefu ilibidi niende nikatafute maziwa kwa sababu niliona nimeanza kulewa,” amesema.
Amesema alipokunywa maziwa na kutulia kwa muda wa nusu saa bila kunywa pombe alihisi ahueni ndipo alianza kunywa tena.
Amesema aliona njia hiyo kama rahisi kwake katika kupunguza mning’inio aliokuwa akiuhisi mwanzoni awali kila alipoamka baada ya kunywa usiku.
Maneno yake hayatofautiani sana na Lameck Mlimi ambaye aliliambia Mwananchi kuwa amekiwa akifanya hivyo kila wakati anapohisi kuzidiwa akiwa baa kwa kutafuta maziwa katika eneo husika au duka la karibu.
“Nikifika hapo dukani nanunua pakiti moja ya maziwa freshi nakunywa, nikirudi natulia kwa muda naendelea kunywa, hapo tunaweza kunywa hadi asubuhi nikiwa mzima kama sikunywa usiku,” amesema.
Hata hivyo, hakuna utafiti wa kisayansi unaoonyesha kuwa unywaji wa maziwa unaweza kumsaidia mtu kukata mning’inio wa pombe.
Wakati hali hiyo ikionekana kuwa namna nzuri ya kukabili mning’inio mtaalamu wa afya anaonya kuwa suala hilo linaweza kuathiri afya ya mtanzania.
Akizungumza na Mtaalamu wa masuala ya chakula na lishe, Dk Daudi Gambo amesema kabla ya mtu kutumia maziwa kukata pombe ni muhimu kuelewa muundo wa kemikali wa pombe na virutubisho vilivyomo kwenye maziwa ili kubaini kinachotokea vinapoingia mwilini kwa pamoja.
Amesema maziwa yana protini na virutubisho vingine huku pombe ikiwa na kemikali zake hivyo mtu anapokunywa maziwa baada ya pombe, kuhisi nafuu na kurudi tena kunywa pombe haimaanishi kuwa ulevi umekwisha au pombe imeondoka mwilini bali anatengeneza matatizo ndani ya mwili.
Amesema kuchanganya vinywaji kwa lengo la kupunguza athari za pombe kunaweza kuleta madhara ya kiafya kwani zinakwenda kutengeneza kemikali isiyojulikana ndani ya tumbo kwani kila kimoja kilitengenezwa ili kitumiwe kwa wakati wake.
“Pombe inywewe kama pombe, maziwa kama maziwa na vinywaji vya kuongeza nguvu kama vilivyo. Unapovichanganya kwa imani kwamba vinakata pombe unatengeneza kemilikali isiyojulikana tumboni inayoweza kukuathiri ikiwa hili utalifanya kwa muda mrefu,” amesema.
Amesema mchanganyiko huo unaweza kumfanya mtu kupata matatizo mbalimbali ini, figo, moyo na mfumo wa chakula huku akisema huenda hiyo ndiyo sababu kumekuwa na ongezeko la watu wanaotaka kuchuja damu kufuatia ugonjwa wa figo.
Dk Gambo anayasema hayo ikiwa ni siku moja tangu, Mkurugenzi Mkuu wa TBS, Dk Ashura Katunzi amesema licha ya pombe zinazoingizwa kuwa zimethibitishwa kufaa kwa matumizi, lakini ubora wa kinywaji hauondoi hatari za kiafya zinazoweza kusababishwa na unywaji uliopitiliza au matumizi yasiyo salama.
Amesema kafeini iliyomo kwenye vinywaji vya kuongeza nguvu inaweza kumfanya mtu ajihisi yuko macho zaidi, bila kupunguza kiwango cha pombe katika damu au kurejesha uwezo wake wa kufanya maamuzi sahihi.
“Unapochanganya pombe na kinywaji cha kuongeza nguvu chenye kafeini, kafeini inaweza kuficha athari za ulevi. Mtu anaweza kujihisi yuko macho na hajalewa wakati mwili wake umeathiriwa na pombe,” amesema DK Katunzi alipokuwa akizungumza na wahariri katika mkutano ulioratibiwa na Ofisi ya Msajili wa Hazina.
Amesema hali ya kujihisi macho inaweza kumshawishi mtu kunywa pombe zaidi kuliko alivyokusudia na hivyo kuongeza hatari ya madhara yanayohusiana na unywaji wa pombe.
“Mchanganyiko huo unaweza pia kumfanya mnywaji asitambue kwa usahihi kiwango ambacho uwezo wake umeathiriwa na pombe, jambo linaloweza kudhoofisha maamuzi na uratibu wa mwili, kujihisi macho, lakini hakumaanishi kuwa mtu hajalewa au yuko katika hali salama ya kuendesha gari,” amesema.
Tafiti mbalimbali ambazo zimewahi kufanysa zinahusisha matumizi ya pombe na changamoto za kisaikolojia, kijamii na kiuchumi, zikiwemo msongo wa mawazo, migogoro ya mahusiano na ugumu wa maisha kwa mujibu wa utafiti uliofanywa na TBS.

