Mpelelezi adai DK Kahyoza alikiri kosa kumshambulia trafiki
3 mins read

Mpelelezi adai DK Kahyoza alikiri kosa kumshambulia trafiki

Dar es Salaam. Mpelelezi wa kesi ya shambulio la kudhuru mwili inayomkabili daktari wa binadamu, Conrad Kahyoza; Koplo Samwel  ameieleza Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni kuwa mshtakiwa huyo alikiri kutenda kosa la kumshambulia askari wa Kikosi cha Usalama Barabarani (trafiki) F.8886 Sajenti (Sgt) Andrew.

Koplo Samwel kutoka Kituo cha Polisi Oysterbay ni shahidi wa tano katika kesi hiyo inayosikilizwa na Hakimua Mfawidhi wa mahakama hiyo, Jacqueline Rugemalira, ametoa ushahidi wake mahakamani hapo leo  Jumatano, Oktoba 28, 2026.

Katika kesi hiyo, Dk Kahyoza kutoka Hospitali ya Taifa Muhimbili (MNH)- Mloganzila anadaiwa kumshambulia Sajenti Andrew, wakati akitekeleza majukumu yake, kinyume na kifungu cha 243 (d) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu, Rekebu ya mwaka 2023.

Dk Kahyoza ambaye alipandishwa kizimbani mahakamani hapo na kusomewa shtaka hilo Septemba 10, 2026, anadaiwa kutenda kosa hilo Septemba 8, 2026, saa 1:30 asubuhi, katika Barabara ya Bagamoyo, eneo la Makongo, Dar es Salaam.

Katika ushahidi wake leo, akiongozwa na Wakili wa Serikali, Abdul-Majid Mtukusye, Koplo Samweli ameieleza mahakama hiyo kuwa Septemba 8, 2026, akiwa kazini kituoni hapo alipokea jalada la kesi kutoka kwa Mkuu wa Upelelezi, aliyemwelekeza kulifanyia kazi.

Ameeleza kuwa baada ya kupokea jalada hilo, alilisoma na kuanza uchunguzi kwa kwenda eneo la tukio, ambako alichora ramani ya mahali hapo tukio lilipotokea na baadaye akamhoji mtuhumiwa (mshtakiwa) kuhusiana na kosa hilo baada ya kukamilisha taratibu zote za mahojiano.

Shahidi huyo amefafanua kuwa baada ya kujitambulisha kwa mtuhumiwa/ mshtakiwa, akamjulisha kosa analotuhumiwa, haki zake na kumuonya kuwa kile atakachokisema na kitaekodiwa na kinaweza kutumika kama ushahidi dhidi yake, mshtakiwa aliridhia na akatoa maelezo yake mwenyewe, bila kuwa na wakili.

“Katika mahojiano hayo mshtakiwa alikiri kutenda kosa analoshtakiwa nalo”, amesema Koplo Samweli akibainisha yaliyojiri wakati akimhoji mshtakiwa huyo kuhusiana na kosa linalomkabili na akaongeza kuwa baada ya kuandika maelezo hayo alimpatia mshtakiwa akayasoma kisha akasaini kuthibitisha kuwa yaliyoandikwa ni sahihi.

Pia mpelelezi huyo ameeleza kuwa mbali na kumhoji mtuhumiwa, pia katika uchunguzi wake aliwahoji na kuandika maelezo ya mashahidi mbalimbali na kukusanya nyaraka muhimu zinazohusiana na kesi hiyo ambazo alizihifadhi kwa ajili ya matumizi ya ushahidi mahakamani hapo.

Koplo amefafanua kuwa kwa uchunguzi wake alibaini kuwa tukio hilo lilitokea Septemba 8, 2026, baada ya mshtakiwa kudaiwa kukaidi amri ya Sajenti Andrew  ya kumtaka asimamishe gari lake alipokuwa akipita katika barabara ya huduma.

Amedai kuwa mhstakiwa huyo alikaidi amri hiyo na kutaka kuondoka na kutokana na hali hiyo, Sajenti Andrew alikwenda kumdhibiti mshtakiwa kwa kuchomoa funguo za gari lake, ndipo mshtakiwa akaanza kumshambulia.

Hata hivyo wakati wa maswali ya dodoso, mshtakiwa huyo alipoulizwa na wakili wa utetezi, Yohana Kibingu kama aliyawasilisha mahakamani maelezo hayo ya mshtakiwa ( kukiri kosa) yapokewe na kuwa kielelezo cha ushahidi wa upande wa mashtaka, shahidi huyo amejibu kuwa hakuyaleta.

Wakili Kibingu alipomuuliza mshtakiwa huyo ni kwa nini hakuona umuhimu ya kuyaleta mahakamani maelezo hayo hakuwa na jibu alikaa kimya tu.

Baada ya shahidi huyo kumaliza kutoa ushahidi wake, Wakili Mtukusye ameieleza mahakama kuwa bado wana mashahidi wengine watatu  zaidi, lakini akasema kuwa kwa leo walikuwa wamemuandaa shahidi huyo mmoja.

Hivyo ameomba ahirisho na mahakama ipange tarehe nyingine kuendelee na ushahidi wa mashahidi hao waliosalia.

Wakili Kibingu ameileza mahakama kuwa hana pingamizi dhidi ya ombi hilo la upande wa mashtaka, na Hakimu Rugemalira alikubaliana nalo akaahirisha kesi hiyo mpaka Novemba 10, 2026.

Mshtakiwa huyo yuko nje kwa dhamana na hakimu Rugemalira amemweleza kuwa dhamana yake inaendelea.

Source link

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *