Nakisi ya megawati 40 inavyoua biashara, utalii Zanzibar
4 mins read

Nakisi ya megawati 40 inavyoua biashara, utalii Zanzibar

Unguja. Mahitaji ya umeme visiwani Zanzibar yamefikia megawati 165, huku kiasi kinachopokewa kutoka Tanzania Bara kupitia kebo ya baharini kikiwa ni megawati 135.7 pekee.

Hali hiyo inasababisha upungufu wa megawati 30 hadi 40 na ndio imetajwa chanzo cha umeme kukatikakatika bila mpangilio.

Hali hiyo inajiri wakati kasi ya ukuaji wa shughuli za kiuchumi, hasa uwekezaji wa hoteli, viwanda vidogo na majengo ya kisasa, ikiongezeka kwa kasi visiwani humo.

Upungufu huo tayari umeanza kuumiza sekta muhimu za uchumi wa Zanzibar kama wadau katika sekta hizo walivyozungumza na Mwananchi kwa nyakati tofauti.

Katika sekta ya utalii ambayo ni uti wa mgongo wa uchumi, wamiliki wa hoteli wamesema kukatika kwa umeme kunaharibu taswira ya nchi mbele ya wageni.

“Unapokuwa na wageni kutoka Ulaya na umeme unakatika ghafla, hata kama una jenereta, mteja anaona kama huduma ni duni.

“Jenereta linachukua dakika moja kuwaka, lakini ndani ya dakika hiyo tayari mteja ameshapoteza imani,” amesema Ali Yussuf, Meneja Masoko wa moja ya hoteli kisiwani hapa.

Ameongeza kuwa gharama za kuendesha jenereta kwa saa sita hadi nane kwa siku zimepanda kutoka Sh500, 000 hadi milioni moja kwa siku, gharama ambayo hatimaye inaangukia kwa mtalii.

Kwa wafanyabiashara wadogo, athari ni ya moja kwa moja mfukoni, ambapo Asha Kombo, mmiliki wa saluni na mashine za kusaga amesema biashara yake imeshuka kwa asilimia 40.

“Umeme ukikatika saa 12 jioni, ndio kipindi ambacho wateja wengi wanatoka kazini kuja kusuka. Nikimwambia subiri jenereta, anakwambia hana muda. Siku nikikosa wateja watano, ni hasara ya Sh50,000,” amelalama Asha.

Mchambuzi wa masuala ya uchumi, Salim Mohammed alionya kuwa tatizo hilo linaweza kurudisha nyuma kasi ya ukuaji wa uchumi wa Zanzibar unaokadiriwa kufikia asilimia saba.

“Uwekezaji unaongezeka, lakini uwekezaji unahitaji umeme wa uhakika. Kama viwanda vidogo vya kusindika mwani, karafuu na samaki havipati umeme wa uhakika, tutashindwa kuongeza thamani ya mazao yetu,” amesema.

Ametumia fursa hiyo kuishauri Serikali kuharakisha miradi yake kabla ya msimu wa utalii wa Desemba.

Meneja Mkuu wa Shirika la Umeme Zanzibar (Zeco), Haji Muhammad Haji amekiri kuwepo kwa changamoto hiyo na kueleza kuwa ndio maana Serikali imeamua kutokutegemea tena umeme wa Bara pekee.

“Mahitaji yanaongezeka kila siku. Leo tunazungumza megawati 165, lakini msimu wa sikukuu ukifika mahitaji yanafikia hata megawati 175. Hii inamaanisha tunabakiwa na nakisi ya megawati 30 hadi 40. Ndio maana umeme unakatikakatika,” amesema Haji.

Haji ametoa kauli hiyo wakati wa ziara ya kutembelea kituo cha kupokea na kupoza nishati hiyo Oktoba 29, 2026.

Ili kumaliza tatizo hilo, Haji alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Zeco inatekeleza Mradi wa Zesta (Zanzibar Energy Sector Transformation and Access Project), unaofadhiliwa kwa mkopo wa Dola za Kimarekani milioni 140 (Sh370.7 bilioni) kupitia Benki ya Dunia na kupitia Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Amesema kupitia mradi huo, Serikali inatekeleza miradi miwili ya uzalishaji wa ndani ya umeme wa jua: Bambi itakayozalisha megawati 40 na Matemwe megawati 30.

“Kwa sasa hatutegemei tena umeme wa Bara pekee. Jumla ya megawati 70 kutoka Bambi na Matemwe zitaingizwa moja kwa moja kwenye gridi ya Taifa na kusambazwa kulingana na mahitaji, hatua inayolenga kumaliza kabisa upungufu,” amefafanua Haji.

Kwa upande wake, Meneja wa Mradi wa Zesta, Maulid Shirazi amesema mradi huo upo katika hatua za mwisho na umelenga kuhakikisha upatikanaji wa umeme unakuwa wa uhakika na endelevu, sio tu kuongeza wingi.

“Tunalenga kuimarisha miundombinu ili isibebe tu umeme mwingi, bali umeme usikatike. Pia tunawekeza kwenye nishati ya jua ambayo ni rafiki kwa mazingira,” amesema Shirazi.

Naye, Msimamizi wa kampuni inayotekeleza mradi huo ya Sieyuan Electrical, Johong She, amesema kazi inaendelea kwa kasi na kwa ubora uliotakiwa ili wananchi wanufaike haraka.

“Mradi uko hatua za mwisho, tumefanya kazi kwa ubora kama malengo ya Serikali ya Mapinduzi yalivyoelekeza,” amesema Johong.

Wakati ahadi ya megawati 70 za jua ikisubiriwa kutimia, wananchi na wafanyabiashara wanasubiri kwa hamu kuona nishati hiyo inakuwa na utulivu bila zima waka na kuathiri mfumo wa biashara na jamii.

Source link

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *