Sababu wanawake kuongezeka vyuoni | Mwananchi
Dar es Salaam. Kuongezeka kwa fursa za elimu kwa wasichana, juhudi za kupunguza pengo la kijinsia na mabadiliko ya mitazamo kuhusu nafasi ya mwanamke, ni miongoni mwa mambo yanayotajwa kuongezeka kwa wanawake wanaofikia elimu ya juu, hatua inayozidi kubadili taswira ya vyuo vikuu nchini.
Mjadala huo umeibuka baada ya Mkuu wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM), Rais mstaafu Jakaya Kikwete, kuonesha mshangao kuhusu idadi ya wanawake waliohitimu katika mahafali ya 56, duru ya pili, yaliyofanyika Oktoba 13, 2026.
Katika mahafali hayo, kati ya wahitimu 2,774, wanawake walikuwa asilimia 53.4. Aidha, katika mahafali ya jumla ya wahitimu wa mwaka kwa mujibu wa taarifa ya chuo hicho, mwaka wa masomo 2023/2024, wanawake 5,599 walihitimu kati ya wahitimu 11,148, huku wanaume wakiwa 5,549.
Mwaka 2025, idadi ya wahitimu wanawake ilifikia 6,090 kati ya wahitimu 11,609, sawa na asilimia 52.5, ikilinganishwa na wanaume 5,519.
Hilo ni ongezeko la wanawake 491, sawa na takribani asilimia 8.8, ikilinganishwa na mwaka wa masomo 2023/2024. Takwimu hizo zinaashiria kuimarika kwa ushiriki wa wanawake katika elimu ya juu, ingawa hazitoshi peke yake kuthibitisha kuwa hali hiyo inafanana na vyuo vikuu vyote nchini.
Akizungumzia takwimu hizo, Kikwete alisema hali imebadilika ikilinganishwa na miaka ya nyuma, ambapo wanawake waliohitimu vyuo vikuu walikuwa wachache.
“Tumepiga hatua. Zamani tulikuwa tunahitimu wanawake kidogo, mnawahesabu, lakini leo tunahesabu wanaume kidogo. Eeh, haya twendeni tu,” alisema.
Kauli hiyo imefungua mjadala kuhusu mambo yanayochangia wanawake kuongezeka katika elimu ya juu, pamoja na iwapo hali hiyo inamaanisha kuwa wamewapiku wanaume katika mfumo mzima wa elimu nchini.
Ingawa wanawake wamekuwa wengi katika kundi la wahitimu wa mahafali yaliyotajwa UDSM, hali hiyo haimaanishi moja kwa moja kuwa wanawake wamewapiku wanaume katika vyuo vikuu vyote nchini.
Ripoti ya Ofisi ya Taifa ya Takwimu (NBS), Women and Men in Tanzania 2025, ikitumia takwimu za elimu za mwaka 2025, inaonesha mwaka 2024 wanawake walikuwa asilimia 49 ya wahitimu wa vyuo vikuu nchini, huku wanaume wakiwa asilimia 51.
Takwimu hizo zinaonesha kuwa pengo lilikuwa limepungua ikilinganishwa na mwaka 2020, ambapo wanaume walikuwa asilimia 55.5 ya wahitimu na wanawake asilimia 44.5.
Hivyo, takwimu za UDSM zinaonesha mabadiliko katika kundi la wahitimu wa chuo hicho.
Akizungumza na Mwananchi, mtafiti wa elimu Dk Muhanyi Nkoronko, anasema dera za elimu zinazolenga kutoa fursa sawa, uwekezaji katika shule na kampeni za kupinga mila zinazomkandamiza mtoto wa kike, ni miongoni mwa sababu zinazochangia kuongezeka kwa idadi ya wanawake wanaohitimu elimu ya chuo kikuu kuliko wanaume.
Akifafanua sababu hizo, mtaalamu huyo anqsema juhudi za Serikali kupanua upatikanaji wa elimu, ikiwamo ujenzi wa shule katika maeneo ya vijijini na kuongezeka kwa shule za wasichana, zimechangia kupunguza vikwazo vilivyokuwa vikizuia watoto wa kike kupata elimu kuanzia ngazi za chini hadi elimu ya juu.
Anasema hatua hizo zimeongeza idadi ya wasichana wanaomaliza elimu ya sekondari na kujiunga na vyuo mbalimbali, huku kampeni za Serikali na asasi za kiraia zikisaidia kubadili mtazamo wa baadhi ya familia kuhusu elimu ya mtoto wa kike.
“Mtoto wa kike au mwanamke sasa anachukuliwa kama uwekezaji, si mzigo kama ilivyokuwa awali. Familia nyingi zimeanza kuhakikisha watoto wao wa kike wanasoma hadi kufikia viwango vya elimu ya juu,” anaeleza.
Anaongeza kwamba kupungua kwa baadhi ya mila na desturi zinazowakwamisha wasichana, pamoja na juhudi za kupambana na ndoa za utotoni, kumechangia kuongeza nafasi zao za kuendelea na masomo.
Sababu nyingine aliyotaja ni upatikanaji wa mikopo ya elimu ya juu na programu nyingine za kuwasaidia wanafunzi kumudu gharama za masomo na maisha chuoni.
Anasema mikopo hiyo inapowafikia wanafunzi wenye mahitaji ya kifedha, huwasaidia kuendelea na masomo badala ya kuacha kutokana na kushindwa kumudu ada, malazi, chakula na mahitaji mengine ya kujifunzia.
Kwa mujibu wa DK Nkoronko, wakati wasichana wakinufaika na fursa zinazowawezesha kuendelea na masomo, baadhi ya wavulana hukumbana na changamoto za kiuchumi zinazoweza kuwafanya kuacha chuo kabla ya kuhitimu.
Anasema baadhi ya vijana wa kiume huingia katika biashara au kutafuta ajira wanapopata fursa za kujipatia kipato, hali inayoweza kuvuruga mwenendo wao wa masomo na kupunguza idadi ya wanaokamilisha elimu ya chuo kikuu.
Wavulana nao wanahitaji kuangaliwa
Dk Nkoronko, anasema upunguji wa uwiano wa wanafunzi wa kiume katika baadhi ya ngazi za elimu, unahitaji kufuatiliwa kuanzia elimu ya sekondari hadi vyuo vikuu.
Anasema awali mjadala mkubwa ulihusu vikwazo vilivyowakabili wasichana katika kupata elimu, lakini sasa kuna umuhimu wa kuchunguza sababu zinazofanya wavulana washindwe kuendelea na masomo au kuhitimu kwa wakati.
Anaeleza pamoja na changamoto za kifedha, kukata tamaa wanapokabiliwa na masomo magumu na shinikizo la kutafuta kipato, kunaweza kuchangia baadhi ya wanafunzi wa kiume kuacha masomo.
“Vijana wa kiume wanapokutana na changamoto za gharama za maisha na masomo, baadhi yao hukata tamaa na kuacha. Hili likiendelea bila hatua stahiki, linaweza kuathiri uwiano wa kijinsia katika elimu ya juu siku zijazo,” anasema.
Hata hivyo, anasisitiza kuwa kuongezeka kwa idadi ya wanawake wanaohitimu hakumaanishi kuwa vikwazo vyote vinavyowakabili wasichana vimeondoka. Bado wapo wanaokabiliwa na changamoto zinazoweza kuwazuia kuendelea na masomo, hasa katika maeneo yenye fursa chache.
Wito wa kuongeza ufadhili, ushauri
Kutokana na hali hiyo, anapendekeza kuongezwa kwa ufadhili wa masomo, mikopo na programu nyingine za kuwasaidia wanafunzi wa jinsi zote, kwa kuzingatia mahitaji yao halisi.
Anasema vyuo vikuu vinapaswa kuimarisha programu za ushauri na malezi ya kitaaluma, ili kuwasaidia wanafunzi wanaoanza mwaka wa kwanza kukabiliana na changamoto za masomo na maisha ya chuo.
Kwa maelezo yake, programu hizo zinapaswa kuwawezesha wanafunzi kupata mwongozo wa kitaaluma, msaada wa kijamii na taarifa kuhusu fursa za ufadhili, ili kuongeza uwezekano wa kukamilisha masomo.
Anasema lengo si kupunguza mafanikio ya wanawake katika elimu ya juu, bali kuhakikisha wavulana na wasichana wanapata mazingira yanayowawezesha kujiunga na vyuo, kuendelea na masomo na kuhitimu.
Hata hivyo, miongoni mwa hatua zinazoweza kueleza mabadiliko hayo ni jitihada za kupanua nafasi za wasichana kupata elimu, ikiwamo sera na programu zinazolenga kupunguza vikwazo vinavyowakabili wanapohitaji kujiunga na vyuo vikuu.
Utafiti uliochapishwa mwaka 2006 kuhusu programu za kuongeza udahili wa wanawake UDSM, ulibaini kuwa hatua za upendeleo maalumu zilichangia kuongeza ushiriki wa wanawake, ikiwamo katika baadhi ya fani ambazo kwa muda mrefu zilihusishwa zaidi na wanaume.
Utafiti huo ulionesha uwiano wa wanawake katika Kitivo cha Sayansi uliongezeka kutoka asilimia 16 mwaka 1996 hadi asilimia 27 mwaka wa masomo 2003/04. Katika fani za uhandisi, uwiano huo uliongezeka kutoka asilimia saba hadi 13 katika kipindi hicho.
Hata hivyo, matokeo hayo ni ya kihistoria na hayawezi kutumika peke yake kueleza sababu za takwimu za mahafali ya mwaka 2026.

