Serikali Tanga kufuatilia kesi za migogoro ya wakulima, wafugaji
Tanga. Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Dk Batilda Burian, amesema Serikali haitavumilia vitendo vya watu wanaotumia fedha kuingilia mwenendo wa kesi za migogoro ya wakulima na wafugaji, akisisitiza kuwa kesi zitakazofikishwa mahakamani zitafuatiliwa hadi mwisho ili kuhakikisha haki inatendeka.
Kauli hiyo inatolewa wakati migogoro kati ya wakulima na wafugaji ikiendelea, ikihusisha tuhuma za baadhi ya wafugaji kuingiza mifugo katika mashamba ya wakulima na kusababisha uharibifu wa mazao pamoja na mapigano.
Akizungumza na wananchi wa Kwamsisi, wilayani Handeni leo Ijumaa Oktoba 30, 2026, Dk Burian amesema utoaji wa ardhi kwa watu kutoka maeneo mengine kwa ajili ya shughuli za ufugaji unapaswa kufuata taratibu za kisheria.
Amesema taratibu hizo zinahusisha kuwasilisha maombi katika serikali ya kijiji na kuyajadili katika vikao vya pamoja kabla ya kutoa idhini ya kutumia eneo husika.
“Eneo mnalotoa mjiridhishe kabisa kwamba mnakaribisha aina fulani ya shughuli, kusiwe na shughuli nyingine tofauti. Tutaitisha sensa na kuhakikisha kila mmoja yupo kihalali, na wale ambao hawako kihalali watarudi wanakotoka. Ni lazima tujiridhishe kwamba kila shughuli haiendi kuathiri shughuli nyingine,” amesema.
Akizungumzia hatua zilizochukuliwa kukabiliana na migogoro hiyo, Mkuu wa Wilaya ya Handeni, Salum Nyamwese, amesema mwaka 2025 kesi 17 zilifikishwa mahakamani, ambapo 11 ziliondolewa baada ya wakulima na wafugaji kufikia makubaliano nje ya mahakama.
Amesema kuanzia Januari hadi Oktoba 2026, kesi 21 zilifikishwa mahakamani, huku saba zikiondolewa baada ya pande hizo mbili kufikia makubaliano nje ya mahakama.
Ameongeza kuwa baadhi ya wakulima wamekuwa wakikubaliana na wafugaji kuingiza mifugo katika mashamba yasiyo yao, hali inayochangia kuchochea migogoro kati ya pande hizo.
Kwa upande wake, mkulima Saimon Msese, mkazi wa Kwedikabu, amesema amekuwa miongoni mwa waathirika wa mifugo kuingizwa katika mashamba ya wakulima.
Amedai baadhi ya wafugaji waliingiza mifugo katika shamba lake la migomba baada ya baadhi ya majirani zake kupokea fedha kutoka kwa wafugaji hao.
“Eneo la Kwamsisi, eneo la Pozo, halina uwezo wa kuishi wakulima na wafugaji kwa kuwa ni dogo. Wakulima watalimia wapi na wafugaji watalishia wapi? Wafugaji wana silaha, sisi hatuna. Ukisema uwakamate na kuwapeleka mahakamani, mkulima anashindwa kwa kuwa hana fedha,” amesema.

