Wadau Maswa wataka hatua zaidi marufuku ya mifuko ya plastiki  
3 mins read

Wadau Maswa wataka hatua zaidi marufuku ya mifuko ya plastiki  

Maswa. Wakati Serikali ikiendelea kusisitiza marufuku ya matumizi ya mifuko ya plastiki nchini, baadhi ya wafanyabiashara mjini Maswa mkoani Simiyu, wametaka hatua zaidi zichukuliwe kudhibiti uzalishaji na usambazaji wa mifuko hiyo, wakieleza kuwa bado inapatikana katika maeneo ya biashara.

Mifuko hiyo imeendelea kuonekana ikitumika kufungia bidhaa katika baadhi ya maduka na masoko, zikiwemo nyama, mbogamboga na bidhaa nyingine zinazouzwa kwa wateja.

Wakizungumza na Mwananchi Oktoba 30, 2026 baadhi ya wafanyabiashara wameibua mjadala kuhusu namna ya marufuku hiyo inavyotekelezwa na kuitaka serikali kuhakikisha mifuko hiyo haipatikani sokoni na kutoa mwongozo kuhusu njia mbadala za kufungashia bidhaa.

Michael Amos, mfanyabiashara wa bucha ya nyama mjini Maswa, amehoji sababu za wafanyabiashara kuzuiwa kutumia mifuko hiyo wakati bado inaendelea kupatikana katika maeneo mbalimbali ya biashara.

Amesema kuwa mifuko hiyo imekuwa ikitumika kufungia bidhaa zinazouzwa kwa wateja, hivyo Serikali inapaswa kuweka wazi njia mbadala zinazoweza kutumiwa na wafanyabiashara hao.

Mkuu wa wilaya ya Maswa, Dk Vicent Naano .Picha na Samwel Mwanga

“Serikali ndiyo inayopaswa kueleza namna mifuko hii inavyoendelea kupatikana, lakini sasa inatuzuia kuitumia kufungia bidhaa tunazowauzia wateja wetu,” amesema.

Kwa upande wake, Edina Edward, mfanyabiashara katika soko la jioni mjini Maswa, amesema kuwa serikali inapaswa kudhibiti uzalishaji na usambazaji wa mifuko hiyo ili kuhakikisha haipatikani sokoni.

“Kuwazuia wafanyabiashara kuitumia mifuko hii ya plastiki bila kudhibiti upatikanaji wake kunaweza kuwaweka katika mazingira magumu wanapohudumia wateja wao,” amesema.

Naye, Ibrahim Hassan amesema kuwa utekelezaji wa marufuku hiyo unapaswa kuhusisha pia bidhaa zinazozalishwa viwandani na kufungashwa katika mifuko ya plastiki, akitolea mfano mikate, maandazi na bidhaa nyingine.

Amesema ni muhimu kuangalia namna bidhaa hizo zinavyofungashwa ili hatua za kudhibiti mifuko ya plastiki zizingatie pia upatikanaji wa vifungashio mbadala vinavyokubalika kisheria.

“Baadhi ya wafanyabiashara wadogo tumekuwa tukitegemea mifuko hiyo kurahisisha ufungashaji na usafirishaji wa bidhaa tunazowauzia wateja,” amesema.

Akizungumzia hatua zinazochukuliwa, Ofisa Mazingira wa Halmashauri ya Wilaya ya Maswa, Duttu Lubinza amesema kuwa tayari wametoa elimu kwa wafanyabiashara katika soko la Maswa kuhusu utekelezaji wa sheria za mazingira.

Mifuko ya plastiki ikiwa imefungiwa kitoweo cha nyama. Picha na Samwel Mwanga

Amesema kuwa elimu hiyo inalenga kuwajengea uelewa kuhusu masharti ya Sheria ya Usimamizi wa Mazingira, Sura ya 191, ikiwemo marufuku ya matumizi ya mifuko ya plastiki.

Ameongeza kuwa baada ya kutoa elimu hiyo, halmashauri inajiandaa kufanya operesheni ya kuwabaini na kuwachukulia hatua wanaoendelea kusambaza na kutumia mifuko hiyo.

“Baada ya elimu kutolewa sasa tutafanya operesheni kabambe ya kuhakikisha tunawakamata watu wote ambao bado wanasambaza na kutumia mifuko hiyo na kisha kuwafikisha kwenye vyombo vya sheria,” amesema.

Hata hivyo, Mkuu wa Wilaya ya Maswa, Dk Vicent Naano Anney, amesema kuwa mifuko ya plastiki ni miongoni mwa vitu vinavyochangia uchafuzi wa mazingira, akisisitiza kuwa serikali katika wilaya hiyo haitaruhusu matumizi yake kuendelea.

“Hii mifuko tumeshaipiga marufuku kwa matumizi ya aina yoyote na ambaye atakamatwa akiendelea kuitumia atachukuliwa hatua kali za kisheria. Hivyo, wananchi wanapaswa kukataa kutumia mifuko hiyo kama kifungashio kwani vifungashio vipo ambavyo tayari serikali ilishavipitisha na vinatumika kote nchini,” amesema.

Source link

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *