Wanafunzi watatu wafariki dunia baada ya kugongwa na gari
2 mins read

Wanafunzi watatu wafariki dunia baada ya kugongwa na gari

Arusha. Wanafunzi watatu wa kidato cha tatu katika Shule ya Sekondari Mringa, iliyopo Wilaya ya Arumeru mkoani Arusha, wamefariki dunia papo hapo baada ya kugongwa na gari katika Barabara ya Bypass iliyopo katika Kijiji cha Kiushini.

Ajali hiyo imetokea jana Oktoba 30, 2026 saa 10 jioni katika barabara hiyo iliyopo Kata ya Olorien ambapo lori hilo linadaiwa kuacha njia na kugonga gari ndogo aina ya Toyota Rumion, kisha kuwagonga watembea kwa miguu hao watatu (wanafunzi) ambao walifariki papohapo.

Kwa mujibu wa taarifa ya Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha, Justine Masejo, waliofariki kuwa ni Bianka Juma, Catherine Pius na Jesca Sabore, ambao wote walikuwa wanafunzi wa kidato cha tatu katika shule hiyo.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva la lori hilo lililokuwa likiendeshwa na Abdul Seleman, mkazi wa Arusha, ambaye alikuwa anayapita magari mengine bila kuchukua tahadhari.

“Chanzo cha ajali hiyo ni uzembe wa dereva wa lori ambaye alikuwa anayapita magari mengine bila kuchukua tahadhari, hali iliyosababisha kwenda kugonga gari dogo lililokuwa limepaki pembeni ya barabara na kukosa uelekeo,” ameeleza Kamanda Masejo.

“Jeshi la Polisi Mkoa wa Arusha linawataka madereva wote kuzingatia sheria na kanuni za usalama barabarani ikiwemo kufuata alama za barabarani, kuwa makini na watumiaji wengine wa barabara na kuchukua tahadhari zote zinazohitajika kuepusha ajali na vifo.”

Kwa mujibu wa baadhi ya mashuhuda wa tukio hilo, gari dogo lilipaki pembeni kwa ajili ya kuwapa lifti wanafunzi hao kabla ya lori hilo kupita magari mengine bila kuchukua tahadhari na kugonga gari hilo lililokuwa limepaki pembeni.

“Hili gari kubwa lilitokea upande wa huku chini, lilikuwa lina overtake (kuyapita) magari mengine mawili na ile Rumion ilikuwa imesimama pembeni ya barabara kwa lengo la kuwapa wale watoto lifti. Lile gari kubwa likashindwa kumaliza ku-overtake, likagonga hilo gari dogo,” amesema mmoja wa mashuhuda.

“Wale watoto walikuwa wanakimbia, ni uzembe wa dereva hii ni barabara kuu. Alipokuwa anajaribu kurudi upande wake, mahindi aliyokuwa amebeba yakamvuta na akapoteza mwelekeo, akawagonga wale watoto na mmoja wao aliangukiwa na mahindi,” amesema.

Naye, Godson Ayubu ameeleza kuwa wanafunzi hao walikuwa wakiongozana watatu mara kwa mara, na kwa bahati mbaya wamepoteza maisha wakiwa pamoja.

“Miili ya wawili tumeipata, mmoja ndio tunataka kuutoa, lakini huyu wa gari kubwa ndiyo alikuwa na makosa. Huyu mama wa gari dogo alikuwa anataka kuwapa watoto lifti, sasa huyo akaja moja kwa moja, alipoona ameshindwa, akagonga gari lililokuwa limepaki pembeni ya barabara,” ameeleza.

Source link

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *